November 24, 2024

Waziri Kigwangalla aeleza jinsi ya kuendeleza tamasha la urithi wetu

Waandaaji wa Tamasha la Urithi Wetu wametakiwa kuwa wabunifu kwa kuongeza michezo mbalimbali ya jadi ambayo itasaidia kukuza kazi za sanaa na utamaduni wa Mtanzania ili kukuza fursa za utalii na kuwaongezea wananchi kipato.

  • Awataka waandaji kuwa wabunifu kwa kuongeza michezo mbalimbali ya jadi ili kukuza fursa za utalii.
  • Tamasha la Urithi wetu lilianza Oktoba 31 na limehitimishwa Novemba 2, 2019 ambapo liliongozwa na kauli mbiu “Urithi wetu, Fahari yetu”.

Dar es Salaam. Waandaaji wa Tamasha la Urithi Wetu wametakiwa kuwa wabunifu kwa kuongeza michezo mbalimbali ya jadi ambayo itasaidia kukuza kazi za sanaa na utamaduni wa Mtanzania ili kukuza fursa za utalii na kuwaongezea wananchi kipato. 

Tamasha hilo la kila mwaka linalenga kuenzi na kutangaza utamaduni wa kitanzania duniani na hufanyika katika maeneo mbalimbali nchini.

Waziri wa Mali Asili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla aliyekuwa akizungumza wakati wa kufunga tamasha hilo kwa mwaka 2019 mwishoni wa wiki jijini Mwanza, amesema tamasha hilo linapaswa kuwa endelevu ili lilete matokeo yaliyokusudiwa. 

Ili kulifaya tamasha la urithi liwe endelevu, Dk Kigwangalla amesema kuwa ni lazima wananchi wawe na furaha ambapo tamasha hilo linaongeza hamasa katika michezo, sanaa na utamaduni hatua itakayowapelekea wananchi wawe wabunifu, wenye mawazo mazuri yanayowashirikisha wadau wote wa maendeleo ikiwemo sekta binafsi.


Soma zaidi: 


Kigwangalla amesema kuwa Tanzania ina fursa nyingi za kiutamaduni ambapo amebainisha kuwa ni nchi pekee barani Afrika inayojumuisha zaidi ya makabila 128 ambayo yapo kwenye makundi makuu manne ya makabila yanayopatikana Afrika yanayojulikana kama Wakushi, Khoisan, Wabantu na Waniloti.

Amesema tamasha hilo lina lengo la kuendeleza falsafa ya nchi ambayo Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kulinda utamaduni wa Mtanzania.

Tamasha la Urithi wetu lilianza Oktoba 31 na limehitimishwa Novemba 2, 2019 ambapo liliongozwa na kauli mbiu “Urithi wetu, Fahari yetu”.

Tamasha hilo lilipambwa na kushereheshwa kwa michezo mbalimbali ikiwemo ngoma za asili, kwaya, mbio za baiskeli, mbio za mitumbwi pamoja na mchezo wa bao.