October 6, 2024

Alichokisema Magufuli baada ya kumuapisha CAG Kichere

Rais John Magufuli ametoa maagizo mbalimbali kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ikiwemo kufanya kazi kulingana na maagizo anayopewa na mihimili mitatu ya nchi ikiwemo Bunge na anatakiwa kutekeleza majukumu yake ukaguzi kwa uadili

  • Amemtaka CAG huyo kufanya kazi kulingana na maagizo ya mihimili ya Serikali, Bunge na Mahakama.
  • Amesema anaweza kumuondoa katika nafasi hiyo wakati wowote kwa sababu zipo taratibu za kufanya hivyo. 
  • Awataka majaji walioapishwa kutoa hukumu za haki. 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametoa maagizo mbalimbali kwa  Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ikiwemo kufahamu kuwa  nchi ina mihimili mitatu ikiwemo Bunge na anatakiwa kutekeleza maagizo anayopewa ya ukaguzi kwa uadilifu bila kuonea watu. 

Rais Magufuli alimteua Charles Kichere kuwa CAG jana akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Profesa Mussa Assad ambaye anamaliza muda wake leo. 

Akizungumza leo (Novemba 4, 2019) Ikulu Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amemtakia kazi njema CAG Kichere na kumtaka anapotekeleza majukumu yake asijifanye ni mhimili kwa sababu nchi ina mihimili mitatu inayotambulika na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

“Kwa CAG mpya nakutakia kazi njema, usije ukaenda huko ukajifanya na wewe ni muhimili. Mihimili ni mitatu tu na umeiona hapa; kuna mahakama, Bunge na sisi wengine wa Serikali.

“Na katika kiapo chako nilikuwa nakisikiliza, nafasi yako ni Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Kwa hiyo mwenye Serikali yupo, kafanye vizuri kazi zako za ukaguzi bila kuonea watu,” amesema Rais.  

Amemtaka kufahamu kuwa yeye ni mtumishi na akipewa majukumu na mihimili hiyo anatakiwa kutekeleza bila kubishana. 

Katika hatua nyingine, amemtaka kupanga vizuri safu ya watendaji katika ofisi ya CAG ili kuhakikisha inafanya kazi vizuri na mapungufu yaliyopo yanayoondolewa kabisa.

Akitolea mfano baadhi ya mapungufu hayo, Rais amesema wapo baadhi ya wafanyakazi wa ofisi ya CAG wanapotumwa kwenda kufanya ukaguzi kwenye balozi wanalipwa hapa nchini lakini wakifika kwenye hizo balozi nako wanaomba pesa. 

“Ofisi ya CAG siyo clean (safi) kama mnavyofikiria, sasa nenda kachambue, ukapange nafasi za watu wako ili mauchafu chafu haya ukayasafishe,” amesisitiza Rais Magufuli. 

Hata hivyo, amemtahadharisha CAG Kichere kuwa anaweza kumuondoa katika nafasi hiyo wakati wote kwa sababu taratibu za kumuondoa zipo huku akisema siyo kwamba anamtisha bali anamtaka akatekeleze majukumu yake kikamilifu. 

“Katiba inazungumza, sheria zinazungumza, unaweza kukaa miaka mitano ya mkataba wako, unaweza ukakaa hata mwaka mmoja kwa sababu taratibu za kukutoa zipo na zinafanywa na Rais lakini sikutishi wewe nenda kachape kazi,” amesema Rais.


Zinazohusiana:   


Akizungumzia uteuzi wa CAG, Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema CAG ni jicho la Taifa na ana majukumu mazito ya kukagua hesabu za Serikali na kutoa ushauri pale inapohitajika.

Amesema Bunge linamkaribisha Kichere na litampa ushirikiano wote katika kutimiza majukumu ya kazi zake. 

“Karibu sana, tunakutegemea sana kama jicho letu kwa maana jicho ndiyo kila kitu kwa mwanadamu. Ukikosa jicho siyo rahisi kujua unaelekea wapi. CAG ni mtu muhimi, ni jicho la Taifa letu unaangalia namna gani ya kushauri matumizi mbalimbali, namna yanavyokwenda, kushauri namna ya kurekebisha,” amesema Spika Ndugai.

Kabla ya Kichere kuteuliwa kuwa CAG alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe na kabla ya hapo alikuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na nafasi yake ilichukuliwa na  Edwin Mhede.

Kichere ana Shahada ya Sheria (LL.B) kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini, Dar es salaam Tanzania (TUDARCO) na Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara (MBA) katika Fedha kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm).

Pia ana shahada ya Biashara katika Uhasibu (B.Com Uhasibu) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm).

Maagizo kwa majaji

Rais Magufuli amewataka Majaji 12 aliowateua na kuwaapisha leo Ikulu kutoa hukumu za haki kwa sababu Taifa linawategemea na wamepewa mamlaka makubwa ya kutoa haki huku akiwataka wasizicheleweshe kwa sababu changamoto ziko katika maeneo mbalimbali. 

Amewataka watimize wajibu wao kwa kuwatumikia Watanzania ambao haki zao nyingi zinapotea ili kuipunguzia mzigo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB). 

Pia amegiza Katibu Tawala Mkoa wa Njombe, Katarina Revocati ambaye amechukua nafasi ya Kichere kufanya kazi na viongozi wa mkoa huo ili kuibua fursa mbalimbali zilizopo zitakazoboresha maisha ya wananchi.

Kabla ya Revocati kuteuliwa kuwa RAS alikuwa Msajili Mkuu wa Mahakama Tanzania. 

CAG Charles Kichere akiapa mbele ya Rais John Magufuli  leo Ikulu Jijini Dar es Salaam. Picha|Mtandao.

Wakati huo huo, Magufuli amemtaka Kamishana wa Kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu aliyeapishwa leo, Francis Ronald Mbindi kushughulikia tatizo la vibali hewa vinavyotolewa kwa wageni ambao wakati mwingine wanafanya kazi zisizoanishwa kwenye vibali husika. 

“Ile ofisi kaisimamie kweli kweli, nisije nikawa tumekupeleka pale mwanajeshi, halafu kazi zikawa za hovyo utakuwa umewahaibisha wanajeshi pamoja na CDF (Mkuu wa Majeshi). Kwa hiyo vibali vya hovyo hoivyo, wapo watu wanatoa forgery (ghushi) na wanashirikiana na watu wizara zingine kasimamie,” amesema Rais.

Hafla hiyo ya uapisho ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan. Naye Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema majaji 12 walioteuliwa na Rais wanaongeza nguvu ya mahakama katika utekelezaji wa majukumu yake. 

“Mheshimiwa Rais nashukuru kwa kutupatia majaji 12, nguvu yetu imeongezeka kutoka majaji 66 waliokuwepo asubuhi ya leo hadi 78. Tukiwaondoa majaji wawili ambao wana majukumu maalum, nguvu kazi yetu ni majaji 76. Na hadi mwisho wa mwaka huu majaji wawili watastaafu kwa hiyo nguvu kazi itashuka hadi majaji 74,” amesema Profesa Juma na kubainisha kuwa, 

“Mzigo wa kazi baada ya kuwapata hao majaji, kila jaji atakuwa na mzigo wa mashauri 518 na uwezo wa kila jaji ni mashauri 220. Mhe Rais bado tutaendelea kurudi kwako kutaka nyongeza ya nguvu kazi.”