November 24, 2024

Mambo muhimu ya kuzingatia unapotengeneza maudhui mtandaoni

Kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa kwa kushirikiana kampuni ya Ona Stories jana (Novemba 30,2019) waliandaa warsha ya siku moja kuhusu zana muhimu zinazoweza kutumiwa na vyombo vya habari vinavyoibukia Afrika kutengeneza maudhui yenye manufaa

  • Kuifikiria hadhira yako na kugusa hisia zao ni ufunguo muhimu.
  • Kujifunza zaidi na kukubali mabadiliko ni chachu ya mafanikio.

Dar es Salaam. Kila siku Martha Ngwanda akishika simu yake kutengeneza maudhui ya video, hutumia nusu saa au zaidi kufikiria ni nini afanye kwa ajili ya watazamaji wake.

Binti huyo ambaye ni mchekeshaji na mtengeneza video za vichekesho (comedy), hufikiri sana ni nini cha kufanya ili azidi kuwavutia watazamaji kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii ikiwemo Instagram.

Huenda changamoto anazopata  Martha zikawa historia kwa sababu wataalam wa mawasiliano wameeleza mambo ya msingi ambayo mtengeneza maudhui ya mtandaoni anatakiwa kuzingatia ili kuwafikia na kukidhi matarajio ya wafuasi wake.

Kampuni ya habari na teknolojia ya Nukta Africa kwa kushirikiana kampuni ya Ona Stories jana (Novemba 30,2019) waliandaa warsha ya siku moja kuhusu zana muhimu zinazoweza kutumiwa na vyombo vya habari vinavyoibukia Afrika kutengeneza maudhui yenye manufaa kwa jamii. 

Mwanzilishi wa Ona Stories, Princely Glorious aliyekuwa akizungumza katika warsha hiyo amesema ili maudhui yalete maana, mtengenezaji anapaswa kwanza kuwafikiria juu ya watumiaji kwanza. ​

Amesema vyombo vya habari hasa vinavyochipukia vitapa mafanikio kama vitawekeza nguvu kubwa kuwapatia watu kile wanachotaka. 

“Ni muhimu kuangalia ni nini hadhira yako itafurahia na siyo kile wewe unafurahia,” amesema Glorious.

Maudhui yenye kuleta matokeo chanya ni yale yanayogusa hisia za watu uliowatengenezea, kwa maana ya kuzingatia utu wa mtu na mazingira yanayomzunguka. 

“Kama utaweza kumgusa mtu, ni lazima atasambaza maudhui yako,” amesema Glorious.

Kwanini unatengeneza maudhui hayo? 

Ni swali ambalo unatakiwa kujiuliza kabla ya kuanza chochote. Na haitakiwi kuishia hapo unahitaji kuifanya “kwa nini” yako kuwa kubwa kwa kila hatua unayoiendea wakati wa kutengeneza maudhui.

Lengo la maudhui yako ni nini? Unataka watakaona, kusoma au kusikia kile ulichokitengeneza wachukue hatua gani katika maisha yao.

Mwanzilishi wa Ona Stories, Princely Glorious aliyekuwa akizungumza katika warsha hiyo. Picha|K15 Photos.

Gusa kila mtu

Fikiria kama umeandaa maudhui ambayo yanagusa hadhira ya Dar es Salaam pekee. Ni kwa kiasi gani mtu wa Tabora au wa Mwanza ataweza kuhusiana na maudhui hayo?

Kwa kufahamu hilo, ni vyema kila unapotengeneza maudhui uyafanya yahusiane na wasomaji wengi zaidi na yafanane na yale ya watu wengine ulimwenguni.

Maudhui yako ni muhimu yalenge kueleweka na mtu wa kawaida kwa kutumia lugha nyepesi yenye masimulizi yanayovutia na yenye uhalisia.

“Unapotengeneza maudhui, unatakiwa kufikiria ni jinsi gani mtu wa kigoma vijijini anaweza kuelewa,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen katika warsha hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Dausen amesema “mara nyingi waandishi wa habari na watengeneza maudhui wengine hushindwa kuhusianisha walichotengeneza au kuandika na hadhira yao”, jambo linalosababisha watu washindwe kupata ujumbe uliokusudiwa.


Zinazohusiana


Hata hivyo, Dausen ameshauri watengeneza maudhui kutokuacha kujifunza mambo mapya hasa ya zana za kidijitali ili kuendana na jamii ambazo wanazihudumia.

“Wengi wetu husahau kuwa kuna mambo ya kuangalia zaidi yakiwemo takwimu na habari picha (infographics) ambazo zinaweza kuyapa maisha maudhui yetu,” amesema Dausen.

Warsha hiyo ya siku moja ililenga kuwaleta pamoja wadau wa habari kujadili teknolojia mpya zinazoweza kutumika na vyombo vya habari kuihudumia jamii.

Pia zana ambazo taasisi na mashirika mbalimbali yanaweza kutumia kuimarisha na kuendeleza vitengo vyao vya habari na mawasiliano ili kuwafikia kirahisi wateja wao.