November 24, 2024

Tanzania yapanda nafasi tatu urahisi wa kufanya biashara duniani

Imeshika nafasi ya 141 kati ya nchi 190 katika urahisi wa kufanya biashara duniani baada ya kupanda kwa nafasi tatu kutoka 144 mwaka 2018/2019.

  • Imeshika nafasi ya 141 kati ya nchi 190 katika urahisi wa kufanya biashara duniani baada ya kupanda kwa nafasi tatu kutoka 144 mwaka 2018/2019. 
  • Tanzania iko juu kidogo ya wastani wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wa alama 51.8 huku ikiwa chini ya wastani wa dunia wa alama 63. 
  • Wachambuzi washauri sheria na wingi wa kodi viangaliwe upya ili kuwapa ahueni wafanyabiashara. 

Dar es Salaam. Ripoti mpya iliyotolewa na Benki ya Dunia (WB) inaeleza kuwa Tanzania imepanda kidogo katika viwango vya urahisi wa kufanya biashara duniani, jambo lililochagizwa na mabadiliko yaliyofanywa na Serikali mwaka mmoja uliopita ikiwemo kufuta na kupunguza kodi zilizokuwa kero kwa wafanyabiashara.

Ripoti hiyo ya Urahisi wa kufanya Biashara (Doing Business 2020) imeeleza kuwa Tanzania imeshika nafasi ya 141 kati ya nchi 190 katika urahisi wa kufanya biashara duniani ikiwa imepanda kwa nafasi tatu kutoka 144 katika ripoti ya mwaka 2019. 

Ripoti hizo, licha ya kuwa na matokeo ya mwaka husika wa utafiti, huwa zina jina lenye mwaka unaofuata. 

Katika ripoti hiyo mpya iliyotolewa mwezi huu wa Oktoba, Tanzania imepata alama 54.5 ikiwa imepanda kidogo kutoka alama 53.6 iliyopata mwaka jana.

Tanzania iko juu kidogo ya wastani wa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wa alama 51.8 huku ikiwa chini ya wastani wa dunia wa alama 63. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo alama 100 ni sawa na ‘Frontier score’ inayotambulisha nchi zenye utendaji mzuri zaidi kwenye uchumi hasa urahisi wa  kufanya biashara na sifuri maana yake ni vibaya.

Upangaji wa kuupa nafasi uchumi wa nchi katika urahisi wa kuanzisha na kufanya  biashara unapatikana kwa kuangalia umbali wake kufikia ‘Frontier score’ ambapo ni kiwango bora kinachoshikiliwa na nchi zilizoendelea ambazo zina mazingira mazuri ya uwekezaji.

Utafiti huo uliangazia vigezo 12 vya mazingira ya kuanzisha biashara, kupata kibali cha ujenzi, upatikanaji wa umeme, usajili wa bidhaa, kuwalinda wawekezaji, makato katika kodi, uingizaji wa bidhaa mipakani, uingiaji wa mikataba, kuajiri wafanyakazi, pamoja na mikataba kati ya wawekezaji na serikali.

Serikali nayo imeeleza katika nyakati tofauti kuwa itaendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini ikiwemo kuainisha mikakati mbalimbali ya mfumo na sera inayokusudia kutekeleza katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 unaoanza julai mwaka huu. Picha|Mtandao.

Uboreshaji wa mazingira ya kufanyia biashara ikiwemo uboreshaji wa miundombinu; kupambana na urasimu na rushwa; na kufutwa kwa baadhi ya kodi kumeipandisha Tanzania kwa nafasi tatu ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita. 

Baadhi ya mabadiliko yaliyofanyika ni majukumu ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na kuwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).

Pia Tanzania imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa kusajili biashara na kampuni, kitabu cha maboresho kwa wafanyabiashara (Brueprint) ikiwa ni hatua kuweka mazingira bora ufanyaji biashara kwa wafanyabiashara na kuvutia wawekezaji wengi. 

Hata hivyo, bado ina kibarua kigumu cha kuboresha na kuimarisha mfumo manunuzi ya umma na utoaji huduma bora ili kuvutia wawekezaji wengi, kurekebisha mifumo ya kodi na kuongeza wigo wa biashara na nchi jirani, kwa sababu ripoti hiyo inaonyesha Tanzania haifanyi vizuri katika maeneo hayo.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya uchumi na kodi, wameiambia nukta.co.tz, ili Tanzania ipande zaidi katika viwango vya urahisi wa kufanya biashara, inapaswa kuongeza kasi ya utoaji wa vibali vya ujenzi na biashara ili kuvutia wawekezaji na kutanua wigo wa biashara nchini. 

Mkurugenzi wa huduma za kodi kutoka kampuni ya ukaguzi wa mahesabu ya Auditax International, Shabu Maurus amesema changamoto inayoikumba Tanzania ni uwepo wa kodi nyingi ambazo haziendani na kasi nzuri ya elimu ya mlipa kodi, jambo linalopelekea watu wengi kutokuwa na muamko wa kulipa kodi.

“Ni muhimu turahisishe sheria za kodi na kupunguza mlolongo wa kodi kuwawezesha wafanyabiashara kulipa kodi zinazoendana na uzalishaji wao. Hii inaweza kusaidia hasa kama itaenda sambamba na elimu ya mlipakodi,” amesema Maurus.


Zinazohusiana: 


Serikali nayo imeeleza katika nyakati tofauti kuwa itaendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini ikiwemo kuainisha mikakati mbalimbali ya mfumo na sera inayokusudia kutekeleza katika mwaka wa fedha wa 2019/2020 unaoanza julai mwaka huu. 

Katika hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2019/2020 iliyowasilishwa Bungeni Juni 13, 2019 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, imeeleza kuwa Serikali itaanza kutekeleza mpango unaolenga kuwapa nafuu wanyabiashara hapa nchini.

“Napenda niwahakikishie wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi kwa ujumla kuwa kuanzia mwaka ujao wa fedha, Serikali itaanza kutekeleza kwa nguvu zaidi mpango kazi wa kuboresha mazingira ya biashara (Blueprint for the Regulatory Reforms to improve the Business Environment) ili mazingira ya biashara nchini yawe rafiki zaidi na yenye gharama nafuu,”alisema Dk Mpango.

Urahisi wa kufanya biashara Afrika Mashariki

Kwa upande wa nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Tanzania imeshika nafasi ya nne baada ya Rwanda, Kenya na Uganda.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa Rwanda imeshika nafasi ya 29 kati ya nchi 190 zilizoshiriki katika utafiti huo ikiwa imepanda kutoka nafasi ya 41 iliyoshika mwaka jana, huku Kenya ikiporomoka hadi nafasi ya 80 ikitoka nafasi ya 61 mwaka 2018. Kenya imerudi tena kwenye iliyowahi kushika mwaka 2017. 

Uganda imeshika nafasi ya 127 na Burundi 168, huku New Zealand ikiongoza duniani kwa kuwa na mazingira rafiki zaidi kwa wafanyabiashara kufanya biashara.