Tanzania yapendekeza Kiswahili kuwa lugha rasmi ya UN
Wakati vikao vya kamati ya nne ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) vikiendelekea nchini Marekani, Tanzania imeendelea kuipigia chapuo lugha ya Kiswahili iwe miongoni mwa lugha rasmi za chombo hicho chenye wanachama 193.
- Iwe miongoni mwa lugha rasmi za chombo hicho chenye wanachama 193.
- Kama Kiswahili kitakubaliwa, itakuwa ni lugha ya saba rasmi ya UN baada ya Kiarabu, Kichina, Kiengereza, Kirusi, Kifaransa na Kihispania.
- Kiswahili ni lugha rasmi kwenye Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Dar es Salaam. Wakati vikao vya kamati ya nne ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) vikiendelekea nchini Marekani, Tanzania imeendelea kuipigia chapuo lugha ya Kiswahili iwe miongoni mwa lugha rasmi za chombo hicho chenye wanachama 193.
Akihutubia kikao hicho jana (Oktoba 21, 2019), mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Modest Mero amesema wito huo wa Taifa lake unazingatia ukweli kuwa Kiswahili hivi sasa ni lugha ya kiafrika inayozungumzwa na takribani watu milioni 500 kote duniani.
“Na kama hiyo haitoshi tayari lugha ya Kiswahili ni lugha rasmi kwenye Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Bunge la Afrika na hivi karibuni ilitangazwa kuwa lugha rasmi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC),” amesema Mero wakati akihutubia wajumbe wa kamati hiyo ya nne ambayo ilikuwa na mjadala kuhusu hoja ya masuala ya habari.
Amesema Kiswahili pia hutumika kwenye matangazo ya vyombo vikubwa vya habari vya televisheni na redio barani Afrika, Ulaya, Urusi, Amerika, Asia na Mashariki ya Mbali.
Akizungumzia mitihani ya kila mwaka ya mpango wa kuajiri vijana wabobezi kwenye Umoja wa Mataifa (YPP), Balozi Mero amesema kuna umuhimu wa kuweka kwenye orodha ya nchi shiriki, mataifa yanayozungumza lugha ya Kiswahili ili kujenga uwezo wa kitengo cha habari za Kiswahili ndani ya Umoja wa Mataifa.
“Hii itawezesha kitengo hicho kufanya kazi yake kwa ufanisi kwa ajili ya wazungumzaji wa Kiswahili kupitia televisheni, redio na mitandao ya kijamii,” amenukuliwa Mero na redio ya Umoja wa Mataifa.
Soma zaidi:
- Kiswahili ndiyo mpango mzima wa kusaka wateja Tanzania: Ripoti
- Wageni kufunzwa Kiswahili katika Chuo cha Diplomasia
- Kiswahili chapendekezwa kuwa lugha rasmi ya SADC
Kama Kiswahili kitakubaliwa, itakuwa ni lugha ya saba rasmi ya UN baada ya Kiarabu, Kichina, Kiengereza, Kirusi, Kifaransa na Kihispania ambazo zinatumika sasa.
Redio na televisheni bado zinahitajika
Katika hotuba yake, Balozi Mero amesisitiza kuwa pamoja na kuwepo kwa teknolojia za kisasa za upashanaji habari ikiwemo mitandao ya kijamii, bado redio na televisheni ni vyombo muhimu kuwafikia wananchi hasa wa vijijini.
“Tanzania inaungana mkono na wanachama wengine juu ya umuhimu wa teknolojia za kisasa zilizopo katika mawasiliano duniani ambako matumizi ya njia za zamani kama matangazo ya redio na televisheni yanasalia kuwa mbinu inayotumika zaidi kwa vizazi vingi duniani,” amesema.
Hata hivyo, kuna umuhimu wa mataifa yote kuweka kanuni za udhibiti hususan matumizi holela ya taarifa za umma na upashaji habari usio sahihi, ambavyo amesema vinaweza kuwa na madhara makubwa kwa jamii.
Ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa na nchi wanachama zizingatie maazimio na maamuzi yaliyopitishwa na kuweka maadili ambayo yanaweza kuhakikisha uzingatiaji wa viwango vya juu vya usahihi, maadili na uwajibikaji ili kuepusha matumizi holela ya taarifa na njia za mawasiliano kinyume na sheria ya kimataifa.
Kamati ya nne ya Baraza Kuu la UN inahusika na masuala kadhaa ikiwemo habari, hoja ya Palestina na kutokomeza ukoloni.