October 6, 2024

Hii ndiyo mikoa 10 ya mwisho mtihani wa darasa la saba 2019

Mara waendelea kushika mkia kwa mara ya pili mfululizo ukiwa na wastani wa ufaulu wa takriban asilimia 70.

  • Mara waendelea kushika mkia kwa mara ya pili mfululizo ukiwa na wastani wa ufaulu wa takriban asilimia 70.
  • Kiwango cha ufaulu wa wasichana mkoani Mara ndiyo kidogo zaidi nchini kwa jinsia hiyo ya kike.
  • Mikoa nane ukiwemo Mara yaendelea kubaki kwenye orodha hiyo ya aibu.
  • Sinyanga na Singida yapomoroka na kuingia kwenye orodha ya mikoa 10 ya mwisho kitaifa.

Dar es Salaam. Siku mbili baada ya walimu na wakazi wa mikoa 10 kitaifa iliyofanya vema katika matokeo ya darasa la saba mwaka 2019 kusherekea mafanikio yao, wenzao wa mikoa ya mwisho ukiwemo mkoa wa Mara leo wameanza ‘kugugumia maumivu’ baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kutangaza takwimu za ufaulu wao.

Katika mkutano wake na wanahabari Jumatano hii, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alitangaza orodha ya mikoa 10 bora lakini hakuweka bayana mikoa iliyoshika mkia.

Kucheleweshwa kwa orodha hiyo ya mikoa 10 ya mwisho kitaifa, kulileta hamasa miongoni mwa wadau wa elimu waliotaka kufahamu iwapo kuna mabadiliko yeyote kutoka katika orodha iliyotolewa mwaka jana.

Necta, katika matokeo ya mwaka 2019, imebainisha kuwa mkoa wa Mara ndiyo mkoa wa mwisho kitaifa baada ya kupata wastani wa ufaulu wa asilimia 69.7 ikiwa ni mara ya pili mfululizo. Mwaka jana Mara pia ilishika mkia katika mtihani huo muhimu katika kujenga msingi wa elimu kwa watoto nchini.

Ufaulu wa Mara upo chini kwa asilimia zaidi 10 kutoka ule wa kitaifa wa asilimia 84.7. Ukichana na wastani wa ufaulu wa kimkoa, ufaulu wa wasichana wa asilimia 65.2 mkoani Mara ndiyo mdogo kuliko yote nchini kijinsia.

Hii ina maana kuwa theluthi au sawa na kusema kuwa wasichana 35 kati ya 100 waliofanya mtihani wa kumaliza darasa la saba mkoani Mara wamefeli hivyo kushindwa kutimiza ndoto zao za masomo za kuendelea na elimu ya sekondari.  


Zinazohusiana: 


Kiwango hicho cha ufaulu kwa wasichana mkoani humo ni cha chini ikilinganishwa na wenzao wa kiume ambao ufaulu wao ni asilimia 74. Kwa ni wanafunzi 26 tu kati ya 100 wamefeli mtihani au sawa na robo ya watahiniwa wavulana.

Mara unafuatiwa kwa karibu na Manyara wenye ufaulu wa takriban asilimia 72, Tabora, Dodoma, na Singida wenye ufaulu wa asilimia 75.

Mikoa mingine iliyoingia katika orodha hiyo ya aibu ni Songwe, Kigoma, Tanga, Lindi, na Shinyanga.

Kati ya mikoa 10 ya mwisho iliyoingia katika orodha ya mwaka huu, mikoa nane imeendelea kubaki katika nafasi hizo huku miwili ya Singida na Sinyanga ikiwa ni mipya.

Mikoa ya  Rukwa na  Simiyu imejinasua  kutoka  katika katika orodha  hiyo ya mikoa ya mwisho. Mkoa wa Simiyu wenye umefanya vyema baada ya kupanda hadi nafasi ya nane kitaifa mwaka huu kutoka nafasi ya 22 mwaka 2018. 

Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa iliyojipatia umaarufu miaka ya hivi karibuni kutokana na Mkuu wa mkoa huo Anthony Mtaka kutumia makambi ya kujifunza kujiandaa na mitihani hiyo. 

Rukwa wenyewe umepanda kwa nafasi tano hadi nafasi ya 13 kutoka nafasi ya 18 mwaka 2018 katika matokeo hayo.

Mikoa minne ya Manyara, Dodoma, Songwe  na Kigoma imebakia katika orodha hiyo ya mikoa ya mwisho tangu mwaka 2017.