October 6, 2024

Kwanza Tv yakata rufaa kufungiwa miezi sita

Televisheni ya mtandaoni ya Kwanza Tv imekata rufaa kwa Baraza la Ushindani Tanzania (FCT) dhidi ya adhabu ya kufungiwa kwa muda wa miezi sita iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kukiuka kanuni za utangazaji.

  • Televisheni hiyo ya mtandaoni  imekata rufaa kwa Baraza la Ushindani Tanzania (FCT) dhidi ya adhabu hiyo iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
  • Imesema  Kamati ya Maudhui ya TCRA ilikuwa haina vielelezo vya kutosha kufikia uamuzi wa kutoa adhabu hiyo.
  • Yataka ifunguliwe na kulipwa fidia ya hasara iliyopata baada ya kusimamisha biashara. 

Dar es Salaam. Televisheni ya mtandaoni ya Kwanza Tv imekata rufaa katika Baraza la Ushindani Tanzania (FCT) dhidi ya adhabu ya kufungiwa kwa muda wa miezi sita iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kukiuka kanuni za utangazaji. 

Kamati ya maudhui ya TCRA iliifungia televisheni hiyo Septemba 27, 2019 baada ya kukutwa na hatia ya kutoa taarifa inayohusu Dk Gwajima kupata ajali bila kutaja jina la kwanza jambo lililoelezwa kufanywa kwa makusudi kuikuza habari.

Katika tangazo lilitolewa leo (Oktoba 18, 2019) na Msajili wa FCT katika gazeti la The Guardian, linaeleza kuwa Kwanza Tv imekata rufaa dhidi ya maamuzi yote yaliyotolewa na TCRA ya kuzuiwa kuchapisha na kusambaza maudhui ya mtandaoni. 

Mkata rufaa ambaye ni Kwanza Tv, ameeleza kuwa kamati ya TCRA ilikuwa haina vielelezo vya kutosha kufikia uamuzi wa kutoa adhabu hiyo na anataka uamuzi huo ubatilishwe na alipwe gharama zote na fidia ya hasara iliyotokana na kusimamishwa kuendelea na biashara yake.

Hata hivyo, Msajili wa FCT ameeleza katika tangazo hilo kuwa kama kuna mtu yeyote ana maslahi ya maamuzi yatakayotolewa na dhidi ya rufaa iliyowasilishwa, anaweza kuomba  kuingilia kati wakati shauri linaendelea ndani ya siku saba tangu notisi kutolewa. 


Zinazohusiana:


FCT ni chombo maalum na huru cha kisheria kinachojumuisha wataalam wa uchumi, biashara na sheria ambao kazi yao ni kusikiliza na kuamua kesi zinazohusu ushindani na masuala ya kisheria yanayotokana na maagizo na maamuzi ya Tume ya Ushindani Tanzania (FCC), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji  (EWURA) na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

Wakati akitoa adhabu hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA, Joseph Mapunda alisema Kwanza Tv walikutwa na kosa la kukiuka misingi ya uandishi wa habari na kanuni za utangazaji kwa kuchapisha habari iliyolenga kupotosha.

Alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook, Kwanza Tv iliweka video iliyobebwa na kichwa cha habari “Dk Gwajima apata ajali”.

Mapunda alisema kwa makusudi habari hiyo haikutaja jina la kwanza la Dk Gwajima hivyo kuzua taharuki hasa ikizingatiwa kuna mtu mwingine maarufu anayetumia jina hilo.

“Uongozi wa Kwanza Tv uliitwa mbele ya kamati kutoa utetezi wao, baada ya kusikiliza kamati ilijiridhisha kuwa wamefanya kosa hilo kwa makusudi ili kuikuza habari hiyo,”alisema Mapunda.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA, Joseph Mapunda alipokuwa akitoa uamuzi wa kamati hiyo kuifungia televisheni ya mtandaoni ya ‘’Kwanza Tv’’ pamoja na kutoza faini ya Sh5 milioni kwa televisheni za  Watetezi Tv na Ayo Tv Septemba 27, 2019. Picha|Mtandao. 

Pia Kwanza Tv ilikutwa na kosa la kutochapisha sera na mwongozo kwa watumiaji wake jambo linalowapa uhuru wa kuweka maudhui yoyote bila kujali athari zinazoweza kujitokeza.

Kwa makosa hayo mawili kamati ilifikia uamuzi wa kuifungia Kwanza Tv kwa muda wa miezi sita.

Kosa la kutochapisha mwongozo kwa watumiaji walikutwa nalo pia televisheni za mtandaoni za Millard Ayo na Watetezi Tv ambazo zote zilitozwa faini ya Sh5 milioni na kupewa onyo.

Siku mbili baada ya adhabu hiyo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kiliishauri Kamati ya Maudhui ya TCRA kutumia njia ya majadiliano na onyo kabla ya maamuzi ya kusimamisha au kupiga faini chombo cha habari ili kuondoa mkanganyiko wa maamuzi yanayotolewa.