November 24, 2024

Mikoa kanda ya ziwa inavyopokezana umwamba 10 bora matokeo darasa la saba

Kwa miaka mitatu mfululizo, mikoa hiyo imekuwa ikichuana vikali kuingiza shule nyingi katika orodha hiyo ya dhahabu huku mwaka huu kanda hiyo imeingiza shule zote 10 katika orodha hiyo.

  • Kwa miaka mitatu mfululizo, mikoa hiyo imekuwa ikichuana vikali kuingiza shule nyingi katika orodha hiyo ya dhahabu.
  • Mwaka huu kanda hiyo imeingiza shule zote 10 kwenye orodha ya10 bora kitaifa. 
  • Pia imekuwa kinara wa kutoa wanafunzi wengi kwenye 10 bora kitaifa. 

Dar es Salaam. Wakati tafakari ya matokeo ya kumaliza elimu ya msingi (PSLE) mwaka 2019 ikiendelea, gumzo bado liko kwenye mikoa ya kanda ya ziwa ambayo imeendelea kuonyesha umwamba wa kutawala orodha ya dhahabu ya shule 10 bora kitaifa.

Shule zote 10 katika orodha hiyo mwaka huu zimetoka katika kanda hiyo yenye mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Kagera, Mara, Simiyu na Geita.

Akitangaza Matokeo hayo jana (Oktoba 15, 2019), Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonda, amezitaja shule zilizoingia 10 bora kuwa ni Graiyaki iliyoshika nafasi ya kwanza ikifuatiwa na Twibhoki; zote za mkoani Mara huku Shule za Msingi za  Musabe(5); Tulele(6), Peaceland(8) na Mugini(9) zikitokea mkoa wa Mwanza. 

Shule nyingine ni Little Treasures iliyoshika nafasi ya nne, Kwema Modern (7) na Rocken Hill (10) zinatokea Shinyanga huku Mkoa wa Kagera ukitoa shule moja ya Kemebos ilishika nafasi ya tatu kitaifa.

Wakati Mara ikiingiza shule mbili katika orodha hiyo, pia mkoa huo umetoa mwanafunzi bora kitaifa, Grace Mori Manga aliyetoka katika shule ya Graiyaki. 

Ufaulu huo wa kanda ya ziwa siyo wa kubahatisha, kwa sababu katika kipindi cha miaka miwili iliyopita imekuwa ikichauna vikali na kanda zingine kuingiza shule nyingi kwenye orodha hiyo. 

Lakini mikoa hiyo nayo imekuwa ikibadilisha kuingia katika orodha hiyo, kuhakikisha inabaki kuwa vinara katika matokeo ya darasa la saba kila mwaka. 

Kwa mwaka 2018, kanda hiyo ilifanikiwa kuingiza shule sita kati ya 10 kitaifa huku mkoa wa Kagera ukiwa baba wa matokeo hayo.

Kagera alikuwa baba wa matokeo kwa sababu iliingiza shule nne za JKibira ambayo ilishika nafasi ya saba, St. Achileus Kiwanuka (8), St. Severine (9) na Rweikiza ilifunga orodha hiyo katika nafasi ya 10. 

Mkoa wa Shinyanga nao uliingiza shule mbili za  Kwema Modern iliyoshika nafasi ya nne na Rocken Hill (5) na Mwanza ikipenyeza shule moja ya Nyamuge katika nafasi ya pili.


Zinazohusiana


Pamoja na hayo, Kwema Modern na Rocken Hill za Shinyanga zimeiona tena orodha ya 10 bora kwa mwaka 2019, huku shule zilizobaki zikitoa nafasi kwa shule zingine kutawala orodha hiyo. 

Hali kama hiyo pia ilijidhihirisha mwaka 2017 ambapo kanda hiyo aliingiza shule sita katika orodha ya dhahabu; Shule ya Msingi ya St Peter, Mwanga, Rweikiza na St Severine  za Kagera, Alliance ya  Mwanza na Palikas ya Shinyanga.

Mwaka huu, kanda hiyo ilizidisha ubabe na kuamua kuingiza shule zote 10 katika orodha hiyo na kuzipiku kanda zingine. Hata hivyo, mafanikio hayo yanachangiwa zaidi na shule zinazomilikiwa na watu binafsi.

Mchuano hauishii tu kwenye kanda lakini mikoa hiyo ya kanda ya ziwa nayo inachuana vikali kuingiza shule nyingi kwenye orodha ya dhahabu.

Mathalani, Kagera iliyoongoza mwaka 2017 na 2018 kwa kuingiza shule nne kwenye orodha ya 10 bora, imeingiza shule moja tu mwaka 2019 huku Mwanza ikijipa umwamba kwa kuingiza shule nne baada ya kuchechemea mwaka 2018 kwa kuwa ilikuwa na shule moja na mwaka 2017 iliingiza shule mbili.

Kwa matokeo ya mwaka huu, kanda ya ziwa itaendeleza ubabe wake katika mtihani wa darasa la saba mwaka 2020? Picha| Mtandao.

Hata wanafunzi bora wanatoka kanda ya ziwa

Kanda ya ziwa siyo tu inafanya vizuri katika ngazi ya shule, bali inafanya kila liwezalo kuingiza wanafunzi wengi kwenye orodha ya wanafunzi 10 bora kitaifa kila mwaka. Mwaka 2018, kanda hiyo iliingiza wanafunzi sita kwenye orodha hiyo.

Lakini mwaka huu imevunja rekodi, imeiingiza wanafunzi tisa waliotoka katika mikoa ya Mara, Shinyanga, Geita na Mwanza huku mwanafunzi mmoja aliyebaki akitoka Jijini Dar es Salaam; mkoa mmojwapo wa kanda ya mashariki. 

Kwa matokeo ya mwaka huu, kanda ya ziwa itaendeleza ubabe wake katika mtihani wa darasa la saba mwaka 2020?