October 6, 2024

Thamani ya hisa za Kenya Airways zashuka soko la hisa Dar

Thamani ya hisa za kampuni ndege la Kenya Airways (KA) katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) zimeshuka kwa asilimia 8.33 na kuwafanya wawekezaji waliowekeza katika kampuni hiyo kupoteza Sh5 kwa kila hisa.

  • Hadi soko linafungwa leo jioni, thamani hisa moja ya KA ilikuwa Sh55 kutoka Sh60 iliyorekodiwa jana sawa. 
  •  Wawekezaji wa kampuni hiyo wamepoteza Sh5 kwa kila hisa moja leo sokoni.
  • Thamani ya hisa za kampuni za NMG na EABL zapanda kwa viwango tofauti. 

Dar es Salaam. Thamani ya hisa za kampuni ndege la Kenya Airways (KA) katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) imeshuka kwa asilimia 8.33 na kuwafanya wawekezaji waliowekeza katika kampuni hiyo kupoteza Sh5 kwa kila hisa.

Ripoti ya siku iliyotolewa leo (Oktoba 15, 2019) na DSE inaeleza kuwa hadi soko linafungwa leo jioni, thamani hisa moja ya KA ilikuwa Sh55 kutoka Sh60 iliyorekodiwa jana. 

Hiyo ina maana kuwa wawekezaji wa kampuni hiyo watalala na maumivu kwa sababu wamepoteza Sh5 kwa kila hisa moja leo sokoni.

Wakati thamani ya hisa za KA ikishuka, kampuni ya habari ya NMG na kampuni ya bia ya Afrika Mashariki (EABL) zina kila sababu ya kutabasamu kwa sababu thamani ya hisa zao zimepanda kwa viwango tofauti. 

Thamani ya hisa za NMG zimepanda kwa asilimia 2.20 ambapo mpaka soko linafungwa thamani ya hisa moja ilikuwa Sh930 kutoka Sh910 iliyorekodiwa jana na kuweka kibindoni Sh20 kwa kila hisa.

EABL nayo thamani ya hisa zake zimepanda kwa asilimia 0.47 hadi kufikia Sh4,260 leo jioni ukulinganisha na jana ambapo thamani yake ilikuwa Sh4,240. 


Zinazohusiana: 


Wakati thamani ya hisa za NMG na EABL zikipanda na zile za KA zikishuka, kampuni zilizobaki viwango vyake vibaki kama vilivyokuwepo jana zikiwemo Vodacom, na benki ya CRDB, DCB na Acacia. 

Hata hivyo, benki ya CRDB ndiyo iliyofanya vizuri zaidi leo baada ya kuongoza kwa kuuza kiwango kikubwa cha hisa. 

Vodacom imeuza hisa 66,905 sawa na asilimia 92.3 ya hisa zote zilizouzwa sokoni leo huku ikifuatiwa kwa mbali na kampuni ya uwekezaji ya  NICO ambayo imeuza hisa 5,000 na kampuni ya bia ya TBL (500).