Unayoweza kufanya kuushinda ugonjwa wa gauti
Njia rahisi za kuushinda ugonjwa huo unaoathiri maungio ya mwili ni kupunguza ulaji wa nyama na unywaji wa pombe lakini ongeza kasi ya kufanya mazoezi.
- Ni moja kati ya magonjwa yanayoathiri sana maungio ya mwili wa mwanadamu.
- Husababishwa zaidi na ulaji wa nyama hasa ya mbuzi.
- Njia rahisi za kuushinda ni kupunguza ulaji wa nyama na unywaji wa pombe lakini ongeza kasi ya kufanya mazoezi.
Nikiwa nimekaa na wadau tunakula nyama choma ya mbuzi, ghafla anapita barubaru mmoja mdogo kwetu sote anasimama karibu yangu na kunigusa begani akicheka kwa bashasha na kusema “Dokta! Siamini kama nawe unashiriki dhambi hii ya kuwafanya vijana hawa kupata gauti wakiwa bado wachanga sana” kisha akaondoka.
Waungwana hawa wakabaki wananiangalia na kucheka kisha wakanisihi hebu tupe madini kidogo kuhusu hii gauti “mzee” na mimi bila hiyana nikaweka pembeni kipande cha nyama nilichokuwa nakula ili niwaeleze kuhusu ugonjwa huo. Nikaanza…
Gauti (Gout) ni moja kati ya magonjwa yanayoathiri sana maungio ya mwili wa mwanadamu. Huhusishwa kwa ukaribu na jamii ya magonjwa ya maumivu ya viungo vya mwili (arthritis).
Gauti hutokea sana kwa watu ambao hula vyakula ambavyo huonekana ni vyakula vya kitajiri (rich foods) kama keki, nyama, viungo vingi pamoja na pombe.
Watu ambao huwa na uzito mkubwa wana uwezekano wa kupata shambulio la gauti. Baadhi ya tafiti zinahusisha ugonjwa huo na urithi ndani ya familia yenye historia ya kuwa na gauti.
Zinazohusiana:
- Fanya haya kuboresha ulaji wa chakula
- Jinsi unavyoweza kuishinda sonona isiharibu maisha binafsi, kazi.
- Mambo yatakayokusaidia kupunguza hatari ya kupata saratani.
Visababishi vya Gauti
Gauti hutokana na kujengeka na kujikusanya kwa wingi kwa tindikali asilia (uric acid) ndani ya damu ambayo hupendelea kujikita kwenye maungio (joints).
Uric Acid ni kemikali asilia inayopatikana katika mwili wa binadamu. Kemikali hii hupatikana baada ya kuvunjwa vunjwa kwa vyakula ambavyo ndani yake kuna kundi la kemikali aina ya Purine ambayo baada ya kuvunjwa ndipo huzalisha tindikali hiyo.
Viwango vya tindikali hiyo vinapozidi kile kiwango ambacho mwili una uwezo wa kutoa kupitia figo zake, tindikali asilia huanza kujenga vibonge vidogo na vibonge hivi hupendelea kukaa katika maungio na kisha husababisha maumivu makali.
Wakati mwingine huweza kujikusanya ndani ya viungo muhimu vya mwili na kuleta madhara makubwa zaidi.
Nyama nyekundu ina kiwango kikubwa cha kemikali aina ya purines. Baada ya kumengenywa ndani ya mwili hupatikana bidhaa ya mwisho aina ya uric acid.
Na hii ndiyo sababu nyama huuhusishwa na gauti, japokuwa nyama ya mbuzi ina kiwango cha juu zaidi uric acid.
Hata hivyo, mwili hauwezi kuhimili viwango vikubwa vya madini haya hivyo hujirundika ndani ya damu na hupendelea kukaa kwenye maungio madogo na hasa vidole gumba.
Hii ni kwa sababu katika maeneo hayo kuna joto dogo kulinganisha na sehemu nyingine za mwili.
Gauti huathiri sana wanaume wenye umri zaidi ya miaka 30 katika asilimia 90 ya kesi zote zinazoguliwa.
Gauti hutokana na kujengeka na kujikusanya kwa wingi kwa uric acid ndani ya damu ambayo hupendelea kujikita kwenye maungio (joints). Picha|Mtandao.
Dalili na athari za Gauti?
Shambulio la gauti ni la kushtukiza na wakati mwingine hutokea usiku. Maumivu yanakuwa ni makali na mtu hupata uvimbe katika maungio ya vidole na hasa kidole gumba cha mguu.
Inaweza kuathiri enka, viwiko na maungio mengine pia. Ukipata shambulio la gauti, maumivu huongezeka zaidi pale unaposimama au kutembea.
Mara nyingi, mtu aliyepata shambulizi la gauti hukosa hamu ya kula, hupata maumivu ya tumbo na homa pia kiwango kidogo cha mkojo.
Jinsi ya kutibu gauti
Hali hii hutibika hospitali, kama umeona dalili kama hizo, nenda kamuone daktari. Lakini kinga ni bora kuliko tiba.
Ni vyema mtu aliyepata shambulizi la gauti kuchukua hatua stahiki ikiwemo kupunguza ulaji wa nyama. Kunywa wa maji mengi pamoja kuepuka vyakula vyenye mafuta. Unywaji wa pombe nao siyo rafiki kwa gauti.
Kupunguza uzito kwa mpangilio husaidia kupunguza uwezekano wa kupata shambulio lingine la gauti. Fanya mazoezi kila wakati na badilisha mtindo wa maisha ikiwemo unywaji wa pombe na vyakula visivyo na ubora mwilini.
Dk Joshua Lameck Sultan ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba katika Chuo cha Tiba na Sayansi Shirikishi Moshi (KCMC) pamoja na hospitali ya KCMC. Pia ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) ambapo hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.