October 6, 2024

MCT yafuta tuzo tatu za umahiri wa uandishi wa habari

Baraza la Habari Tanzania (MCT) limefuta tuzo tatu ikiwemo tuzo ya uandishi wa habari za afya kutoka katika orodha ya tuzo za umahiri wa uandishi wa habari (EJAT) baada ya kukosekana kwa wadhamini wa tuzo hizo.

  • Tuzo hizo ni pamoja na tuzo ya uandishi wa habari za afya; kodi na mapato; na usalama na ubora wa chakula.
  • Baraza hilo limeongeza makundi matatu ikiwemo tuzo za  habari za hedhi salama.
  • Yasema ina mpango wa kuanzisha mfumo wa maombi mtandaoni.

Dar es Salaam. Baraza la Habari Tanzania (MCT) limefuta tuzo tatu ikiwemo tuzo ya uandishi wa habari za afya kutoka katika orodha ya tuzo za umahiri wa uandishi wa habari (EJAT) baada ya kukosekana kwa wadhamini wa tuzo hizo.

Tuzo nyingine zilizofutwa ni pamoja na habari za usalama na ubora wa chakula na habari za kodi na mapato.

Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Kajubi Mukajanga amesema kutokujitokeza kwa wadhamini katika makundi hayo ni sababu kuu iliyosababisha baraza hilo kuzifuta tuzo hizo. 

“Makundi yaliyokuwepo mwaka jana, lakini hayatashindanishwa mwaka huu ni pamoja na habari za usalama na ubora wa chakula, habari za kodi na mapato na habari za afya,” amesema Mukajanga wakati akiongea wanahabari katika uzinduzi wa tuzo za EJAT 2019.

Kwa mwaka huu tuzo hizo zitahusisha makundi 20 yakiwemo makundi matatu ambayo ni mapya.

Makundi mapya ambayo yameingia kwenye tuzo hizo ni pamoja na habari za hedhi salama; uandishi wa habari za ubunifu na maendeleo ya watu; na habari za afya ya uzazi.

Mukajanga amesema makundi hayo tayari yana wadhamini ambao ni Mfuko wa Ubunifu na Maendeleo ya Watu (HDIF) na Mtandao wa Hedhi Salama.​“Waandishi wa habari za mtandaoni na wapiga picha za video wa kike na kiume, walete kazi zao kwa wingi ili kuleta ushindani katika tuzo hizo,” amesema Mukajanga. Picha| Mtandao.

Mwakilishi wa HDIF, Hannah Mwandoloma ambaye ni mtaalamu wa mawasiliano kwenye mfuko huo, amesema ipo sababu kubwa ya kudhamini tuzo hizo ni kuangazia wanahabari ambao wanagusa maisha ya watu mablimbali ambao hawana sauti lakini wana mchango mkubwa kwenye maendeleo.

Amesema HDIF inatoa fedha kwa watu mbalimbali ambao wana miradi yenye kuleta maslahi kwa jamii lakini bado watu wengi hawafahamiki kwa sababu ya kukosa sauti jambo ambalo waandishi wa habari wanaweza kulisuluhisha.

Hii itakuwa mara ya 11 kwa kamati ya maandalizi ya EJAT kuandaa tuzo hizo za umahiri tangu zilipoanza kutolewa 2009 zikilenga kuwatambua na kuwatuza wanahabari waliofanya kazi zao vizuri katika makundi mbalimbali ya kushindaniwa.


Zinazohusiana


Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Hedhi Salama, Mhandisi Wilhemina Malima amesema kinachosukuma mtandao huo kuunga mkono juhudi za MCT ni kuwezesha jamii kufikia katika uelewa mpana wa masuala ya hedhi na kutokuwepo na aibu kwenye kuzungumzia masuala ya hedhi.

Malima amewahimiza wanahabari kusaidia kuangazia suala la hedhi kwani “hata mtoto wa kike mwenye ulemavu ana haki ya kufikiwa na huduma hiyo.”

Katika hatua, nyingine MCT imesema ina mpango wa kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa maombi wa tuzo hizo ili kuwarahisishia waombaji, lakini suala hilo litategemea muamko wa wanahabari wa habari za mtandaoni kuchangamkia fursa hiyo. 

“Waandishi wa habari za mtandaoni na wapiga picha za video wa kike na kiume, walete kazi zao kwa wingi ili kuleta ushindani katika tuzo hizo,” amesema Mukajanga.