Thamani ya mauzo soko la hisa Dar yapaa mara tatu
Thamani ya mauzo ya wiki nzima katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) imepanda zaidi ya mara tatu hadi Sh1.17 bilioni kutoka Sh357.4 milioni iliyorekodiwa juma lililopita huku wachambuzi wakitabiri mwenendo chanya siku zijazo.
- Thamani ya mauzo ya wiki nzima katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) imepanda zaidi ya mara tatu hadi Sh1.17 bilioni kutoka Sh357.4 milioni iliyorekodiwa juma lililopita.
- Wachambuzi waeleza soko hilo huenda likafanya vizuri zaidi siku zijazo kutokana na matarajio ya matokeo ya robo ya tatu ya mwaka ya benki.
Dar es Salaam. Thamani ya mauzo ya wiki nzima katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) imepanda zaidi ya mara tatu hadi Sh1.17 bilioni kutoka Sh357.4 milioni iliyorekodiwa juma lililopita huku wachambuzi wakitabiri mwenendo chanya siku zijazo.
Uchambuzi wa soko kwa wiki iliyoanzia Septemba 30 hadi Oktoba 4 uliofanywa na kampuni ya udalali ya masoko ya mitaji na dhamana, Zan Securities, unabainisha kuwa thamani ya mauzo katika soko hilo iliongezeka kwa asilimia 228 kutoka yale ya wiki iliyopita.
Wiki za DSE hujumuisha siku za kazi pekee yaani Jumatatu hadi Ijumaa.
Mauzo ya soko la hisa yamekuwa na mwenendo wa kupanda na kushuka ambapo wiki jana thamani ya mauzo ilishuka hadi Sh357.43 milioni kutoka takriban Sh505 bilioni iliyorekodiwa katika wiki iliyoishia Septemba 20.“TBL (Kampuni ya bia Tanzania) ndiyo kampuni iliyochagiza zaidi ongezeko la mauzo hayo baada ya kurekodi asilimia 79.37 ya thamani ya mauzo yote ikifuatiwa na benki ya CRDB yenye asilimia 16.04,” imesema taarifa iliyotolewa leo (Oktoba 4, 2019) na Mtendaji Mkuu wa Zan Securities, Raphael Masumbuko.
Zinazohusiana:
- M-pesa, intaneti vyachangia Vodacom Tanzania kupata faida ya Sh90 bilioni
- Wawekezaji wa Acacia soko la hisa Dar tabasamu tupu
- Maumivu kwa wawekezaji wa kampuni ya bia soko la hisa Dar
Masumbuko amesema soko la mitaji lilionyesha matumaini makubwa baada ya thamani ya mauzo kuvuka kikomo cha bilioni.
“Matokeo ya kifedha ya robo ya tatu ya mwaka ya taasisi za kibenki yanatarajiwa kutoka siku chache zijazo…tunaamini kuwa yatachochea kwa kiwango kikubwa utendaji wa soko,” amesema Masumbuko katika utabiri wa hali ya soko wiki ijayo.