November 24, 2024

Maisha ya msanii Harmonize mtandaoni nje ya Wasafi

Amekuwa na mwenendo wa kupanda na kushuka katika mitandaoni hasa Youtube huku akionyesha kuendelea kufanya vizuri katika kazi ya muziki wake.

Kwa sasa, Nyimbo za Harmonize  zinazoongoza kwa kutizamwa kwenye YouTube ni Kwangwaru (Milioni 52) na Bado (Milioni 23) ambazo zote amemshirikisha Diamond Platnumz. Picha|Mtandao.


  • Nyimbo zinazomuweka kwenye chati za juu bado ni zile alizorekodi akiwa WCB.
  • Bado msanii huyo emekuwa gumza mtandaoni kutokana muziki wake. 

Dar es Salaam. Ni takribani siku 46 tangu uvumi wa kutoka kwa “hit maker” Harmonize kwenye lebo ya Wasafi (WCB) usambae kwenye mitandao ya kijamii ambapo ripoti juu ya fununu za kutoka kwake zilianza Agosti 16. 

Fununu hizo zilianza kusambaa katika tamasha la wasafi lililofanyika mjini Mwanza, kwamba Harmonise alitumia usafiri wake binafsi kufanya baadhi ya mambo yaliotoa tafsiri kwamba amejitenga.

Taarifa zinaeleza kuwa tangu Agosti 22, Harmonize alikuwa ameandika barua ya kuvunja mkataba na lebo ya Wasafi huku Meneja wa wasafi Sallam Mendes akisema msanii huyo alikuwa tayari kufuata taratib zote zakisheria kukatisha mkataba wake. 

Msanii huyo kwa jina halisi la Rajab Abdul Kahal ambaye ni kigogo nyuma ya nyimbo za Kwangwaru, Never give up na Aiyola ni kati ya wasanii ambao watu mbalimbali wakiwemo Msanii mkongwe wa Bongo Fleva, Joseph Haule maarufu kama Professor Jay wamemtaja kama mwakilishi na balozi mzuri wa Tanzania nje ya nchi.

Hata hivyo, “U Turn” ambayo Harmonize ameipiga baada ya kuondoka Wasafi ni maamuzi ambayo siyo tu yameacha maswali kwa wadau wa muziki bali hata mashabiki wake wamebaki na viulizo vya namna gani ataweza kubaki kwenye mstari aliokuwa nao kimuziki na kiuchumi.

Nukta imefanya uchambuzi wa takwimu za “Google trends” na “YouTube” za umaarufu wake tangu alipojitoa katika lebo ya Wasafi. Takwimu hizo ni zile za kuanzia Agosti 16 hadi Oktoba 2, 2019.

Chati za Google

Kwa kipindi chote cha minong’ono iliyosababishwa na Harmonize, safari yake kimtandao imekuwa ya kupanda na kushuka kwa umaarufu wake.

Kwa mujibu wa taarifa za “Google Trends” hizo, Harmonize Alikua kwenye hali ya umaarufu zaidi Agosti 28 ambapo hali ya ufuatiliwaji wake mtandaoni kwa ujumla iligota kwenye 100 (kilele cha juu zaidi kwenye google charts).

Katika kipindi hicho, msanii huyo amefuatiliwa sana na watu kutoka Tanzania ambapo wengi wametoka mikoa ya Ruvuma, Mtwara, Pwani, kagera na Singida.

Kimataifa, Harmonize amesakwa na watu kutoka Burundi, Kenya na Zambia kuliko sehemu nyingine yoyote duniani ambapo kati yao kiwango kikubwa zaidi kimetokea Burundi. Mwenendo wa Harmonise katika anavyofuatiliwa mtandaoni kama ilivyoripotiwa na Google Trends kati ya Agosti 16 hadi Oktoba 3, 2019. Picha|Google.

YouTube inasemaje?

Takwimu za mtandao wa YouTube zinaweka wazi kuwa baada ya Harmonize kutoka Wasafi, hajaweza kufika vilele kama mbavyo amevifikia pale alipokuwa kundini.

Takwimu za mtandao huo zinaonyesha Harmonize alikuwa na umaarufu zaidi Agosti 25 hadi Agosti 31 ambapo kwa kipindi hicho, kiwango cha kutafutwa kiligota kwenye kilelel cha alama 100.

Hata hivyo, tangu hapo mstari unaoonyesha ukubwa wa ufuatiliwaji wa Harmonize umeendelea kushuka hadi kufikia alama 66 mnamo Septemba 29 hadi mwanzo wa Oktoba baada ya kutoka kwenye 75  Septemba 22 hadi Sepetemba 28.


Zinazohusiana


Hivyo ni kusema, baada ya kutoka WCB, Harmonize hajaweza kufanya vizuri kwenye nyimbo alizozitoa hivi karibuni jambo ambalo halijazoeleka pale alipokuwa WCB.

Mfano mzuri ni wimbo wa Inabana  ambao umetoka Agosti 28, 2019 (akiwa nje ya wasafi) una watazamaji milioni 1.33 mpaka sasa, kasi ya kutazamwa ambayo ni ya chini ikilinganishwa na pale alipokuwa Wasafi.

Kwa upande wa kuongoza kwenye chati za YouTube, Harmonize ameporomoka hadi nafasi ya tatu kutoka nafasi ya kwanza.

Kwa sasa, nafasi ya msanii anayefuatiliwa zaidi inashikwa na Innos B akifuatiwa na Diamond kisha Harmonize.

Hali kimuziki ikoje?

Kwa sasa, Nyimbo za Harmonize  zinazoongoza kwa kutizamwa kwenye YouTube ni Kwangwaru (Milioni 52) na Bado (Milioni 23) ambazo zote amemshirikisha Diamond Platnumz.

Kwa nyimbo ambazo yupo Solo, Harmonize anabebwa na “Happy birthday” (Milioni 17) na Aiyola (Milioni 15). Nyimbo hizo zote amezirekodi akiwa chini ya lebo ya Wasafi.

Je, Harmonize atasimama na kuendeleza umaarufu wake na kustawi kimuziki? Hayo na mengine ni hapa hapa www.nukta.co.tz.