Mhandisi Manyanya aeleza faida za mfumo wa utoaji taarifa za kibiashara Tanzania
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya amesema ikiwa mfumo wa kielektroniki wa utoaji taarifa za kibiashara nchini Tanzania utatumiwa vizuri utaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya biashara ikiwemo kupunguza muda anaotumiwa kupata
- Naibu Waziri huyo wa Viwanda na Biashara, amesema utaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya biashara nchin,
- Utaongeza uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma kwa taasisi za umma.
- Utapunguza muda wanaotumia wafanyabiashara kupata leseni na vibali mbalimbali kwa sababu taarifa zote zitapatikana mtandaoni.
Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya amesema ikiwa mfumo wa kielektroniki wa utoaji taarifa za kibiashara nchini Tanzania utatumiwa vizuri utaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya biashara ikiwemo kupunguza muda anaotumiwa kupata leseni na vibali mbalimbali.
Mhandisi Manyanya aliyekuwa akizungumza jana (Septemba 30, 2019) katika mkutano wa wadau kuhusu mfumo huo, amesema katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania upatikanaji wa taarifa za leseni na vibali mbalimbali vya kufanyia biashara umekuwa ni changamoto kwa sababu taarifa nyingi bado hazipo mitandaoni ambako mtu anaweza kuzipata kirahisi na kwa pamoja.
“Hivyo, uwepo wa taarifa hizi za biashara mahali pamoja utasaidia wafanyabiashara kujua mahitaji, taratibu na mahali pa kupata vibali na leseni mbalimbali ili kuweza kusafirisha mazao na bidhaa zao kupeleka masoko ya nje ambako ndiyo kuna ushindani mkubwa na bei nzuri,” amesema Naibu Waziri huyo.
Aidha, taarifa hizo zinawawezesha wafanyabiashara kujua taratibu na masharti ya kuingiza bidhaa zao nchini au kuzipitisha nchini kuelekea kwenye masoko lengwa nje ya nchi na kuwezesha Taifa kupata fedha za kigeni.
Manyanya amesema mfumo ambao unajulikana kama “Trade Information Module” ukitumiwa vizuri utaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya biashara nchini ikiwemo kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma kwa taasisi za umma.
Zinazohusiana:
- Kwanini ufuatilie mjadala wa bei ya korosho?
- Wakulima kuwezeshwa kuuza pamba kwa bei wanayotaka
- Karafuu yachangia kushuka kwa mauzo ya nje Zanzibar
Pia utapunguza watu wa kati wenye nia ovu maarufu kama “Vishoka” kwa sababu mfanyabaishara atakuwa anajua hatua kwa hatua namna ya kupata kibali fulani anapotaka kupeleka bidhaa zake nje ya nchi, kuingiza bidhaa ndani ya nchi, au kuzipitisha nchini.
“Utaongeza ukaribu baina ya wafanyabiashara na Ofisi za Umma maana mtu anaweza kutoa maoni, malalamiko au kupendekeza ya maboresho kuhusu masuala ya biashara kupitia mfumo huu kwa ajili ya serikali kufanyia kazi,” amesema Mhandisi Manyanya
Wafabiashara nao watafaidika nao kwa sababu utapunguza muda wanaotumia kupata leseni na vibali mbalimbali kwa kuwa na taarifa sahihi kabla ya kuanza kuomba huduma husika.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya akisisitiza jambo katika kutano wa wadau (hawapo pichani), kuhusu Mfumo wa utoaji wa Taarifa za Kibiashara Nchini (TRADE INFROMATION MODULE) uliofanyika jana, jijini Dar es Salaam. Picha|Maelezo.
Utekelezaji wa mfumo huo ni hatua kubwa katika kuelekea kutimiza makubaliano ya utekelezaji wa kipengele cha 1.1 na 1.2 cha Mkataba wa Uwezeshaji Biashara (Trade Facilitation Agreement) chini ya Shirika la Biashara Duniani (WTO) ulioanza kutekelezwa tarehe Februari 22, 2017.
Hata hivyo, ameielekeza Wakala wa Usajili Biashara na Leseni (BRELA), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) na wadau wengine katika maeneo yao kuendelea kukusanya taarifa za mazao, bidhaa au taratibu za huduma wanazozitoa na kuzihusisha kwenye mfumo huo ili kuleta ufanisi zaidi.
Mfumo huo wa taarifa za kibiashara, ni muendelezo wa jitihada mbalimbali za kuboresha mazingira ya biashara nchini ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi ambao ,msingi wake ni Mpango wa Maboresho kwenye Mfumo wa Udhibiti wa Biashara Tanzania (Blueprint for Regulatory Reform to Improve Business Environment) ulioridhiwa na Serikali Mei, 2018.