October 6, 2024

Halmashauri zatakiwa kujenga miradi ya kimkakati kwa mapato ya ndani

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi na Halmashauri ya Mji wa Mafinga wahakikishe wanajenga mradi wa kimkakati kwa kutumia fedha za mapato ya ndani na si kusubiri miradi kutoka Serikali Kuu

  • Ni halmashauri za Mfundi na Mafinga ambazo zinakusanya zaidi ya Sh7 bilioni kwa mwaka.
  • Zimeonywa zisisubiri fedha kutoka Serikali Kuu kutekeleza miradi ya maendeleo. 
  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aendelea kuwabana viongozi wa mkoa wa Iringa. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi na Halmashauri ya Mji wa Mafinga wahakikishe wanajenga mradi wa kimkakati kwa kutumia fedha za mapato ya ndani na si kusubiri miradi kutoka Serikali Kuu. 

Amesema halmashauri hizo zinakusanya zaidi ya Sh7 bilioni saba kwa mwaka, lakini matumizi yake si mazuri kwa sababu hazina mradi wowote wa kimkakati wanaoutekeleza ambao ungewaongezea mapato.

”Nataka kuona mradi wa kimkakati ukitekelezwa kwa fedha mnazokusanya kutoka kwa wananchi,” amesema Majaliwa aliyekuwa akizungumza jana (Septemba 26, 2019) katika mkutano wa hadhara wilayani Mufindi mkoani Iringa.  

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu inaeleza kuwa viongozi hao wanaweza kutenga Sh1 bilioni kwa mwaka na kujenga hospitali au wakatenga fedha na kujenga barabara za lami kwa awamu.


Soma zaidi: 


Amesema ujenzi wa barabara za lami mijini ni Sh300 milioni kwa kilomita moja, hivyo wangeweza kutekeleza ujenzi huo kutokana na fedha wanazokusanya.

“Msitegemee fedha kutoka Serikali Kuu tu jengeni wenyewe barabara zenu kuzunguka Mji wa Mafinga kwa kiwango cha lami kwa sababu mna fedha za kutosha tena mnaweza kutumia fedha za mapato ya ndani mnazokusanya kutoka kwa wananchi badala ya kuzitumia kwa kulipana posho tu,” amesema Majaliwa.