October 6, 2024

Kristalina Georgieva bosi mpya IMF

Georgieva mwenye umri wa miaka 66 anachukua nafasi ya mtangulizi wake mwanamama Christine Lagarde ambaye amemaliza muda wake.

Kristalina Georgieva ametuliwa  kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF).


  • Uteuzi wake umefanyika Jumatano ya tarehe 25, Septemba 2019
  • Uteuzi wake unamfanya kuwa mwanamke wa pili kuwahi ongoza Shirka hilo.
  • Christine Lagarde anatarajiwa kuongoza Benki Kuu ya Ulaya kabla ya mwaka huu kuisha.

Mtaalamu wa uchumi ambaye ni raia wa Bulgaria, Kristalina Georgieva ameteuliwa  kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Fedha Duniani (IMF). 

Georgieva mwenye umri wa miaka 66 anachukua nafasi ya mtangulizi wake mwanamama Christine Lagarde ambaye amemaliza muda wake.

Uteuzi huo umefanyika Jumatano ya Septemba 25, 2019 na Georgieva anatarajia kuanza rasmi kuitumikia ofisi hiyo mapema Octoba 1, 2019.

Georgieva ameviambia vyombo vya habari vya kimataifa kuwa majukumu hayo ni makubwa kwani kuna mvutano wa kibiashara, madeni makubwa na mwenendo wa uchumi unaokatisha tamaa duniani kwa sasa.

Mwanamama huyo mwenye shahada ya Uzamivu (PHD) ya uchumi, atakuwa na kibarua kigumu cha kupambana na ukosefu wa ulinganifu, majanga ya hali ya hewa na mabadiliko ya kasi ya teknolojia.

Huenda kazi hiyo isimpe tabu Georgieva mwenye uzoefu wa muda mrefu kuongoza mashirika ya fedha ya kimataifa, kwani kabla ya kuteuliwa kushikilia cheo hicho alikuwa Kaimu Rais wa kampuni mama ya Benki ya Dunia (WBG)  kati ya Februari 1 na Aprili 8, 2019. 

Kabla ya hapo alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia tangu mwaka 2017. 

Uteuzi huo unamfanya Georgieva kuwa mwanamke wa pili kuongoza IMF tangu kuanzishwa kwake mwaka 1944.


Zinazohusiana


Kuondoka kwa Lagarde katika ofisi za IMF kumemfungulia mlango wa kuongoza Benki Kuu ya Ulaya (ECB) ambapo naye anatarajia kuanza majukumu hayo baadaye mwaka huu.

 Lagarde amempongeza Georgieva kwa nafasi aliyopata huku akimtakia mafanikio mema katika kutimiza majukumu ya shirika hilo la fedha duniani. 

Shirika la IMF lilianzishwa kwa shabaha ya kuboresha ushirikiano katika mambo ya fedhaduniani ambapo mpaka sasa lina nchi wanachama 189 na makao makuu yako Washington DC nchini Marekani.

Kazi kubwa ya IMF ni kuangalia siasa ya fedha na benki duniani na kuifanyia utafiti. Pia kutoa misaada na ushauri pale inapotakiwa. 

Siyo shirika halisi la Umoja wa Mataifa (UN), lakini hushirikiana kwa karibu na Un. Nchi tajiri za Ulaya pamoja na Marekani ndiyo zinaongoza IMF kwa sababu zimewekeza pesa nyingi katika taasisi hiyo ya kimataifa. 

Mwenyekiti wa IMF huwa anatoka katika nchi za Ulaya na makamu wake hutoka Marekani.