October 6, 2024

Dk Kalemani aagiza bei ya gesi asilia ipitiwe upya

Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani ameziagiza mamlaka zote zinazohusika na upangaji wa bei ya gesi asilia, kufanya mapitio upya ili kuja na bei itakayozinufaisha pande zote yaani Serikali na wawekezaji.

  • Hatua hiyo inakuja baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wawekezaji kuwa gharama ya gesi asilia iko juu.
  • Pia kutofautiana kwa bei ya gesi katika maeneo mbalimbali Tanzania.
  • Ametoa muda wa mwezi mmoja kwa mamlaka husika kukamilisha zoezi hilo. 

Dar es Salaam. Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani ameziagiza mamlaka zote zinazohusika na upangaji wa bei ya gesi asilia, kufanya mapitio upya ili kuja na bei itakayozinufaisha pande zote yaani Serikali na wawekezaji.

Dk Kalemani alikuwa akizungumza Septemba 24, 2019 alipofanya ziara katika kiwanda cha kutengeneza vigae cha Goodwill na kiwanda cha kufua vyuma cha Lodhia, vilivyopo Mkuranga, Mkoa wa Pwani.

Katika kutekeleza agizo hilo, ametoa muda wa mwezi mmoja kuanzia siku hiyo kwa uongozi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na wataalamu wa Wizara, kufanya mapitio ya bei za gesi viwandani ili ziwawezeshe wawekezaji kuzalisha kwa tija.

“Lengo la Serikali ni kujenga mazingira rafiki ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji zaidi kuwekeza nchini hivyo naagiza muanze mara moja kufanya mapitio ya bei husika. Mje na bei linganifu ili kila upande unufaike,” amesema Waziri huyo.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Nishati, Veronica Simba ameiambia nukta.co.tz  leo kuwa kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wawekezaji mbalimbali wenye viwanda kuwa gharama ya gesi asilia iko juu hivyo wanaomba Serikali iangalie uwezekano wa kuipunguza ili wazalishe kwa tija zaidi.

Katika kufanya mapito husika, Waziri amewataka wataalam hao, pamoja na mambo mengine, kuangalia pia uzoefu wa nchi nyingine zenye gesi asilia.

Sababu za bei ya gesi kutofautiana

Waziri Kalemani amefafanua sababu za kutofautiana kwa bei ya gesi katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania, ni kutokana na gharama ya kazi inayofanyika katika kuitafuta, kuichimba na hatimaye kuileta juu ya ardhi. 

Amesema teknolojia ya kufanya hayo yote ina gharama kubwa, jambo linaloongeza gharama za uendeshaji mitambo na bei ya gesi. 

Pia, amesema sababu nyingine ni gharama ya usafirishaji wa gesi kutoka kwenye kisima kwenda kwenye mtambo maalum wa kuchenjulia pamoja na gharama ya kufanya zoezi hilo la uchenjuaji.

“Sasa, kadiri unavyokuwa mbali kutoka kwenye eneo la kuchakata gesi, ndivyo gharama inavyoongezeka. Bei ya gesi kwa yule aliye karibu na eneo la uchenjuaji haiwezi kulingana na aliye mbali,” amesema Waziri huyo. 


Zinazohusiana: 


Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, bei ya sasa ya gesi asilia inaanzia Dola 4.7(Sh10,801) hadi 7.72 (Sh17,741) kwa uniti moja.

Gesi asilia inayozalishwa katika visima vya Songo Songo na Mnazi Bay hutumika katika shughuli mbalimbali za uzalishaji viwandani, majumbani na katika uzalishaji wa umeme unaotumiwa na gridi ya Taifa.

Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2018, kinaeleza kuwa takribani theluthi mbili ya umeme uliozalishwa katika gridi ya Taifa mwaka 2018 ulitokana na gesi asilia. 

Uzalishaji wa gesi asilia katika visima vya Songosongo na Mnazi Bay ulifikia futi za ujazo milioni 59.1 mwaka 2018 ikilinganishwa na futi za ujazo milioni 47.5 mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 24.6.