October 6, 2024

TCU yaongeza muda wa udahili wanafunzi elimu ya juu 2019-2020

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua dirisha la awamu ya nne ya udahili wa wanafunzi katika vyuo mbalimbali nchini ili kutoa nafasi kwa vyuo kukamilisha udahili na waombaji ambao mpaka sasa hawajapata nafasi katika vyuo hivyo.

  • Imefungua dirisha la awamu ya nne ya udahili wa wanafunzi itakayoanza Oktoba 1 hadi 4, 2019.
  • Waombaji, vyuo watuma maombi ya kuongezewa muda ili kujaza nafasi kwa programu ambazo hazina watu. 
  • Mpaka sasa,  waombaji 82,758 sawa na asilimia 85.9 wamedahiliwa katika vyuo hivyo.

Dar Es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua dirisha la awamu ya nne ya udahili wa wanafunzi katika vyuo mbalimbali nchini ili kutoa nafasi kwa vyuo kukamilisha udahili na waombaji ambao mpaka sasa hawajapata nafasi katika vyuo hivyo.

Dirisha hilo litakuwa wazi kuanzia Oktoba 1 hadi 4, 2019 huku waombaji wakitakiwa kuchangamkia fursa hiyo ya kusoma elimu ya juu Tanzania. 

Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Profesa Charles Kihampa aliyekuwa akizungumza na Wanahabari leo (Septemba 25, 2019) jijini Dar es Salaam,  amesema wameongeza muda wa udahili kwa wanafunzi waliokosa kudahiliwa katika awamu zote tatu na vyuo kuomba kuongezewa muda kwani bado vina nafasi.

“Ili kutoa fursa kwa wananchi ambao ama hawakuweza kudahiliwa au hawakuweza kuomba udahili katika awamu tatu zilizopita, na kwa kuzingatia maombi ya baadhi ya vyuo kwamba bado wanazo nafasi za udahili, Tume imeongeza muda kwa kufungua dirisha la awamu ya nne,” amesema Prof. Kihampa. 

Amesema kutokana na mahitaji hayo, wameamua kufungua dirisha la awamu ya nne litakaloanza Oktoba 1 hadi 4 mwaka huu. 


Zinazohusiana: 


Prof. Kihampa amevitaka vyuo vya elimu ya juu kubainisha programu zenye nafasi ili kuwawezesha waombaji kufanya maamuzi sahihi wakati wa kutuma maombi ya udahili na kuepusha usumbufu kwa waombaji kuomba programu ambazo hazina nafasi.

TCU imebainisha kuwa utaratibu wa kutuma maombi ni ule ule wa kutuma maombi moja kwa moja vyuoni kama ilivyokuwa katika awamu zilizopita za udahili.

Waombaji hao wapya watakaopatikana katika awamu ya nne wataambatana na wenzao katika  vyuo  vikuu vya umma na binafsi waliopatikana katika awamu tatu zilizopita. 

Waliodahiliwa mpaka sasa

Kwa mujibu wa TCU, waombaji 96,338 walituma maombi katika awamu zote tatu katika vyuo 75 vilivyoruhusiwa kudahili kwa mwaka wa masomo 2019/20, kati yao waombaji 82,758 sawa na asilimia 85.9 wamedahiliwa katika vyuo hivyo.

Waombaji 37,450 sawa na asilimia 45 ya wadahiliwa wote, walidahiliwa na chuo zaidi ya kimoja. 

Mpaka sasa waombaji 33,453 sawa na asilimia 89.3 wameshajithibitisha katika chuo kimoja na wengine wanaendelea na zoezi hilo hadi Septemba, 30, 2019. 

“Tume inaendelea kuwasisitiza waombaji waliodahiliwa zaidi ya chuo kimoja ambao hawajajithibitisha, wathibitishe katika vyuo wanavyopenda kusoma mapema iwezekanavyo ili kuepuka usumbufu usio wa lazima,” amesema Kihampa.