October 6, 2024

Serikali yawataka watendaji kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa Serikali kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato kwani ujenzi wa miradi ya maendeleo zikiwemo shule na hospitali haiwezi kutekelezwa bila mapato ya uhakika.

  • Wametakiwa kuhakikisha suala la ukusanyaji wa mapato linapewa kipaumbele katika maeneo yao.
  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema bila mapato ya uhakika, miradi ya maendeleo haitatekelezwa kwa wakati.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa Serikali kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato kwani ujenzi wa miradi ya maendeleo zikiwemo shule na hospitali haiwezi kutekelezwa bila mapato ya uhakika.

Amesisitiza kuwa watendaji wahakikishe suala la ukusanyaji wa mapato linapewa kipaumbele katika maeneo yao ikiwemo ukusanyaji wa kodi na tuzo mbalimbali.

“Ukusanyaji wa mapato ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa kwa sababu miradi ya maendeleo kama ujenzi wa shule haiwezi kutekelezeka bila ya kukusanya mapato,” amesema Majaliwa jana (Septemba 24, 2019) wakati akipokea taarifa ya mkoa wa Iringa alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Iringa kwa ajili ya ziara ya kikazi.

Katika hatua nyingine amesema mahusiano kati ya Serikali na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa kidini, kimila ni muhimu yakaimarishwa.


Zinazohusiana: 


Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ni lazima mahusiano hayo yakadumishwa katika ngazi zote kwa sababu Serikali ipo kwa ajili ya wananchi wote na inawahudumia bila ya ubaguzi.

Amewataka viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia maeneo mbalimbali nchini wahakikishe wanatekeleza majukumu yao ipasavyo na uwajibikaji wao uwe na tija.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amesema mkoa huo umepewa zaidi ya Sh7 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Kilolo na Mufindi.

Mkuu huyo wa mkoa amesema mbali na fedha hizo za ujenzi wa hospitali pia Serikali imetoa zaidi ya Sh3 bilioni kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya.