October 6, 2024

Dk Mpango aitaka jumuiya ya kimataifa ijitathmini utekelezaji wa malengo ya maendeleo

Ameitaka ziwajibika ipasavyo ili kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya mwaka 2030.

  • Ameitaka ziwajibika ipasavyo ili kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya mwaka 2030. 
  • Ameshauri  pia wadau kufunguka juu ya mambo mbalimbali yanayoendelea katika nchi zao ili kuwaokoa wananchi. 

Dar Es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amezitaka jumuiya za kimataifa ikiwemo Tanzania kuwajibika ipasavyo ili kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya mwaka 2030.

Amesema lengo kubwa la uwajibikaji huo ni kutimiza malengo hayo kwa pamoja kwani nchi moja ikishirikiana na nyingine, kuna uwezekano wa kupata kitu kinacholeta maana kubwa kwa jumuiya nzima.

Dk Mpango ametoa wito huo kando ya jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa (HLPF) jijini New York Marekani linalotathmini utekelezaji wa malengo hayo kwa nchi wanachama 50 waliojitolea kufanyiwa tathimini ikiwemo Tanzania.

“Ni muhimu jumuiya ya kimataifa itambue kwamba wajibu wa kutekeleza haya malengo ni ya ulimwengu mzima, na hususani baadhi ya nchi ambazo zinaonekana zinavuta miguu hasa katika suala la kupunguza hewa ya ukaa ambayo inatuathiri wote,” amesema Dk Mpango wakati akihojiwa na radio ya Umoja wa Mataifa (UN).


Soma zaidi: 


Dk Mpango amewasihi pia wadau kufunguka juu ya mambo mbalimbali yanayoendelea ili kuwaokoa wananchi na Watanzania juu ya mambo yanayowatatiza na kukwamisha maendeleo katika nchi zao.

“Wafunguke, wasipofunguka ulimwengu wetu huu unazidi kuharibika. Kuna nchi mimi nimeenda hata kupumua ni shida. Yaani unaona kama hewa yote imejaa moshi. Kwa hivyo ni vizuri kila nchi ione dhamana kwamba binadamu tunao wajibu wa kutunza hii dunia ili itutunze,” amesema waziri huyo.