October 7, 2024

Majaliwa aeleza msimamo bei elekezi ya pamba

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wakulima wa zao la pamba nchini wasikubali kuuza pamba yao chini ya bei elekezi ya Sh1,200 ikizingatiwa kuwa soko la uhakika la zao hilo lipo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama kinu cha kuchambua pamba  wakati alipotembelea  Kiwanda cha Kuchambua pamba cha Chama Kikuu cha  Ushirika cha Chato , Septemba 21, 2019. Wengine pichani kutoka kushoto ni Waziri wa Nishati na mbunge wa Chato, Dkt. Medard Kalemani, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi, Robert Gabriel  na kulia ni Meneja   wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Chato, Charles Nyasi. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Amewataka wakulima wa zao la pamba nchini wasikubali kuuza pamba yao chini ya bei elekezi ya Sh1,200 ikizingatiwa kuwa soko la uhakika la zao hilo lipo.
  • Amesema wanunuzi wana fedha za kutosha kununua pamba kwa bei elekezi.
  • Amewashauri wafanyabiashara wa zao hilo waungane na kuanzisha viwanda vya kutengeneza nyuzi na nguo

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wakulima wa zao la pamba nchini wasikubali kuuza pamba yao chini ya bei elekezi ya Sh1,200 ikizingatiwa kuwa soko la uhakika la zao hilo lipo. 

Majaliwa aliyekuwa akizungumza jana (Septemba 21, 2019) na viongozi na wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Chato  (CCU) mkoani Geita, amesema wakulima waendelee kuwa na subira kwa sababu wanunuzi wamepewa fedha za kutosha kununua pamba yote kwa bei ya 1,200 na si vinginevyo.

“Hata mkiwa na shida msikubali kuuza pamba yenu chini ya sh. 1,200 kwa kuwa haitachukua muda mrefu mtakuwa mmeshapata fedha zenu. Tuna taarifa kuwa kuna wanunuzi wamepata fedha na wanawatumia watu kwenda kuwalaghai wakulima kwa kutaka kununua kwa bei ya sh. 800, msikubali na mkiwaona mtupe taarifa,” amesema Majaliwa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewashauri wafanyabiashara wa zao hilo waungane na kuanzisha viwanda vya kutengeneza nyuzi na nguo ili kuongeza thamani kabla ya kuuza pamoja na kuwahakikishia wakulima soko.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, viwanda vya nyuzi na nguo vikijengwa nchini vitakuwa na uhakika wa soko kwani hivi sasa Tanzania  haina viwanda vya kutosha vya nguo. 

Amesema Serikali ipo tayari kuwaunga mkono Watanzania wote au mwekezaji yeyote atakayekuwa tayari kuanzisha viwanda vya aina hiyo kwa sababu mahitaji ni makubwa. 

“Tuna shule zaidi ya 18,000 Tanzania na wanafunzi wote wanavaa sare zinatokanazo na pamba, tukisema majora ya sare yasukwe humu humu ndani na kisha kusambazwa mikoa yote bado nguo za watu wanaovaa mitaani, watapata faida tu,” amesisitiza Majaliwa.


Soma zaidi:


Pia, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wote wa vyama vya ushirika katika maeneo yanayolima pamba kuwaelimisha wakulima kuhusu umuhimu wa kuzalisha pamba safi ili walinde heshima ya pamba Tanzania ambayo duniani inasifika kuwa ni dhahabu nyeupe.

Awali, Meneja wa CCU, Charles Nyasi amemwambia Majaliwa kuwa makampuni ya METEL, KCCL na FRESHO yamejitokeza kununua pamba kupitia AMCOS na tayari kilo milioni 9.611 zimenunuliwa  kati ya kilo 11.1 zilizokusanywa.

Pia Meneja huyo aliiomba Serikali  isaidie kuwalipia deni la Sh696.8 milioni ili kumaliza tatizo la madai ya watumishi na wadai wengine na deni la Sh102.9 milioni la ardhi waliyotumia kujengwa kiwanda chao.

Akijibu maombi hayo Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli haiwezi kulipa deni hilo hadi itakapopewa maelezo ya kina ni nani aliyesababisha deni hilo.