Makumbusho inavyogeuka Kariakoo ndogo ya simu za mkononi Dar
Kituo hicho cha daladala ambacho kiko karibu na barabara ya Bagamoyo kimezungukwa na maduka ya simu yanayoongezeka kwa kasi lakini Ongezeko la maduka ya simu limeibua ushindani na kuzidi kushusha bei za baadhi ya bidhaa.
- Kituo hicho cha daladala ambacho kiko karibu na barabara ya Bagamoyo kimezungukwa na maduka ya simu yanayoongezeka kwa kasi.
- Wingi wa watu na ofisi za makampuni wawavutia wauzaji wa simu kuanzisha biashara katika eneo hilo.
- Ongezeko la maduka ya simu limeibua ushindani na kuzidi kushusha bei za baadhi ya bidhaa.
Dar es Salaam. Ni majira ya saa 12:00 jioni katika kituo cha daladala cha Makumbusho, Wilaya ya Kinondoni, Jijini Dar es Salaam. Katika kituo hiki kuna umati mkubwa wa watu wakiwa ndani na nje ya kituo hicho wakisubiri daladala kurejea makwao baada ya mihangaiko ya siku nzima.
Kituo hicho cha daladala, licha ya kuwa ni kiunganishi muhimu cha usafiri jijini hapa na soko la bidhaa muhimu, siku za hivi karibuni kimejipatia umaarufu baada ya kugeuka moja ya maeneo muhimu ya kununua simu za mkononi na vifaa vyake kama ilivyo kwa Kariakoo.
Maduka ya kuuza simu sasa yanajengwa kila kukicha kuzunguka kituo hicho, jambo linaloashiria kuwa bidhaa hizo za kielektroniki zinahitajika zaidi na watu wanaopita katika eneo hilo.
Uchunguzi uliofanywa na www.nukta.co.tz umebaini kuwa mpaka Septemba 1, 2019 kulikuwa na maduka zaidi ya 13, jambo ambalo lilikuwa vigumu kuliona mwaka mmoja uliopita.
Maduka mengi yaliyopo Makumbusho yamejengwa nusu ya kwanza ya mwaka huu na yanazidi kuongezeka kila siku, kwa mujibu wa wafanyabiashara waliokuwepo eneo hilo kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.
Maduka hayo yana muonekano wa aina yake huku yakiwa yamepambwa kwa vioo angavu na nashki za rangi zenye kumvutia kila mtu anayepita nje kujua nini kilichopo ndani.
Sehemu kubwa ya simu zinazouzwa eneo hili ni Iphone na Samsung ambazo kwa kawaida bei zake huwa juu kidogo, huku baadhi yakiuza Huawei, Techno na Infinix .
Kwa kawaida simu aina ya Iphone na Samsung huuzwa bei ya juu kulingana na sifa zake lakini Makumbusho baadhi ya wanunuzi wanaamini bei zake zipo chini kidogo kuliko wastani wa bei ya soko.
Mbali na kuuza simu, maduka hayo yamekuwa ni makao makuu ya mafundi wa vifaa vya kielektroniki wanaorekebisha simu na kuingiza nyimbo kwenye simu.
Mbali na kupanuka kwa biashara katika eneo hilo la Makumbusho na Kijitonyama, wafanyabiashara wanaeleza kuwa uamuzi wa Serikali kuwaondoa wamachinga katika eneo la Mwenge umechangia kufanya Makumbusho kuwa moja ya maeneo maarufu ya biashara jjijini hapa. Picha|Nukta.
Kasi ya kuongezeka kwa maduka ya simu Makumbusho siyo ya bahati mbaya
Mfanyabiashara wa simu katika eneo hilo, Tony Mlangila ameiambia nukta.co.tz kuwa muingiliano wa watu wa rika mbalimbali katika kituo hicho cha daladala na soko umesaidia watu wengi kulifanya eneo la Makumbusho kama kituo cha kujipatia mahitaji mbalimbali ikiwemo simu.
Mlangila, ambaye amejikita kuuza simu aina za Samsung na Iphone, amesema wengi wamevutiwa kuanzisha biashara ya simu katika eneo hilo kutokana na kubadilika kwa tabia za wanunuzi hasa wale waliokuwa wanakwenda kununua simu Kariakoo.
Amedai kuwa kwa sasa watu hawaendi Kariakoo kwa sababu ya imani waliyojijengea wenyewe ya kuogopa kutapeliwa au kuuziwa simu zisizo na ubora.
Amebainisha kuwa wafanyabiashara wana tabia ya kuambiana maeneo yenye soko, hata kuongezeka kwa maduka Makumbusho pia kumechangiwa na wafanyabiashara kufunguliana fursa za biashara.
Zinazohusiana:
- Matumaini makubwa kuzaliwa mji wa Silicon Dar
- Apple waingiza sokoni simu mpya zinazotumia mfumo wa ‘eSIM’
- Usiyoyajua kuhusu mtandao wa 5G
Mbali na kupanuka kwa biashara katika eneo hilo la Makumbusho na Kijitonyama, wafanyabiashara wanaeleza kuwa uamuzi wa Serikali kuwaondoa wamachinga katika eneo la Mwenge umechangia kufanya Makumbusho kuwa moja ya maeneo maarufu ya biashara jjijini hapa.
Andrew Thomas, mfanyabiashara wa simu Makumbusho amesema uwepo wa miundombinu ya barabara, ofisi za kampuni na mashirika mbalimbali katika eneo hilo, kumewafanya wafanyakazi kupata urahisi wa kununua simu wanazozitaka.
“Ofisi nyingi ziko eneo hili, kwa hiyo wafanyakazi wake wanapotoka ofisini hawalazimiki kwenda Kariakoo kuchukua simu, wanakuja hapa,” anasema Thomas.
Thomas aliyeingia Makumbusho miezi mitatu iliyopita anasema kuondolewa kwa wamachinga na soko eneo la Mwenge na kuhamishiwa Makumbusho, pia kumesaidia kuongeza idadi ya watu wanaotafuta bidhaa mbalimbali ikiwemo simu.
“Ni kuwepo kwa hii stendi, utakumbuka wakati stendi inahamishwa toka Mwenge watu walilalamika sana lakini kama unavyoona sasa wameshakubaliana na mabadiliko,” anasema Thomas.
Makumbusho siyo tu inaibukia kama kituo cha simu, huenda siku zijazo itakuwa kituo muhimu cha mafundi wanaotengeneza simu zilizoharibika.
Maumivu kwa wauzaji, ahueni kwa wateja
Wakati kuongezeka kwa maduka ya simu kunawarahisishia wanunuzi na hata wanaotekeleza miradi ya teknolojia kama Silicon Dar, wafanyabiashara wa bidhaa hiyo ya kielektroniki wamekuwa na maoni tofauti huku wengi wakisema biashara kwa sasa siyo ya kuridhisha.
“Kwa upande wa biashara sasa hivi imekuwa ngumu sana tofauti na mwaka jana mwezi wa tisa, biashara ilikuwa nzuri kwa sababu maduka hayakuwa mengi kama ilivyo sasa,” anasema John ambaye hakutaka kutaja jina lake la pili.
Amesema wauzaji wakiwa wachache wanaweza kupanga bei waitakayo na kujipatia faida nono, lakini ongezeko la maduka linawafanya wanyang’anyane wateja wanaokuja mahali hapo.
Wafanyabiashara wengine wamelalamikia uwepo kodi nyingi, jambo linalowafanya kukosa faida wanayoikusudia hasa pale wanaoingiza mzigo mpya kupitia wasambazaji wao.
Siku ambayo watu wanakua wengi basi na mauzo huongezeka, wakipungua mauzo yanashuka lakini biashara ya simu katika eneo hilo siyo nzuri sana, anasema mmoja wa wafanyabiashara ambaye hakutaka jina liandikwe mtandaoni.
“Biashara huwezi kusema inaenda vizuri au inaenda vibaya ni 50/50 kwa sababu biashara yoyote katika nchi inategemea na hali ya uchumi wa nchi husika,”
“Kama uchumi wa nchi unakuwa mzuri basi wafanyabiashara hasa sisi wadogo itakuwa nzuri lakini kama uchumi wa nchi uko chini unakuja kutuathiri moja kwa moja na sisi wafanyabiashara,” anasema mfanyabiashara huyo.
Mbali na kuuza simu, maduka hayo yamekuwa ni makao makuu ya mafundi wa vifaa vya kielektroniki wanaorekebisha simu na kuingiza nyimbo kwenye simu. Picha|Nukta.
Silicon Dar nayo yaipaisha Makumbusho
Umaarufu wa Makumbusho unachangiwa pia na uwepo wa mradi wa Silicon Dar ambao unatekelezwa katika Jiji la Dar es Salaam kando kando mwa barabara ya Old Bagamoyo na Ali Hassan Mwinyi na maeneo ya jirani hasa Morocco, Victoria, Bamaga na Makumbusho.
Eneo hilo limeanza kujipatia umaarufu kutokana na kuwepo kwa majengo marefu ya kifahari ambayo yanatumiwa na kampuni za teknolojia zikiwemo za mawasiliano ya simu kama Vodacom, Tigo, Halotel na Airtel.
Pia eneo hilo kunapatikana vituo vingi vya kijamii na atamizi za kukuza ubunifu wa teknolojia, ujasiriamali ikiwemo Buni hub, Sahara Ventures, Atamizi ya Biashara na Teknohama (DTBi), Smart Lab, SeedSpace wakiongozwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
Eneo la Silicon Dar linafikika kirahisi kwa sababu ya uwepo wa miundombinu mizuri ya barabara ya Old Bagamoyo na usafiri ikiwemo mabasi yaendayo haraka (DART) unaoanzia Morocco kwenda katikati ya Jiji na Kimara Mwisho.
Wakati maduka ya simu yakiongezeka Makumbusho na wafanyabiashara wakilalamikia ushindani, wanazingatia ubora wa simu wanazouza? Uelewa wa wanunuzi wa simu ukoje? Ni simu zipi zilizotawala mauzo ya maduka hayo? Je, ni kweli iPhone za Makumbusho ni bei ya chini kuliko maeneo mengine? Kwanini?
Maswali yote haya na mengine ni katika makala nyingine itakayokuwekea mambo yote hadharani.