Serikali ya Tanzania yasaini mkataba kununua ndege nyingine mbili
Wakala wa Ndege za Serikali nchini Tanzania na kampuni ya utengenezaji wa ndege ya Airbus wamesaini mkataba wa ununuaji wa ndege mbili aina ya Airbus A220-300 ambazo zitatumiwa na Shirika la ndege la Tanzania (ATCL).
- Ndege hizo ni aina ya Airbus A220-300 ambazo zitatumiwa na Shirika la ndege la Tanzania (ATCL).
- Kwa mujibu wa Airbus bei ya ndege hizo kwa mwaka 2018 ilikuwa ni Dola za Kimarekani milioni 91.5 kwa ndege moja hivyo kwa ndege mbili ni zaidi ya Sh420.5 bilioni.
- Tofauti na ndege za ATCL zilizopo sasa, zitakuwa na ‘screen’ ambayo itakuwa ni sehemu ya burudani kwa abiria.
Dar es Salaam. Wakala wa Ndege za Serikali nchini Tanzania na kampuni ya utengenezaji wa ndege ya Airbus wamesaini mkataba wa ununuaji wa ndege mbili aina ya Airbus A220-300 ambazo zitatumiwa na Shirika la ndege la Tanzania (ATCL).
Mkataba huo umesainiwa leo (Septemba 19, 2019) huku lengo kuu ikiwa ni kuimarisha na kuboresha utoaji huduma za usafiri wa anga nchini.
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali, Benjamin Ndimila amesema ndege hizo zitakua za kipekee na zitaandika historia nchini.
Ndege hizo ni sawa na zile zinatumiwa na ATCL ambazo zina uwezo wa kubebe abiria 142 lakini za sasa zitakuwa na tofauti ambapo kila kiti kitakuwa na ‘screen’ ambayo itakuwa ni sehemu ya burudani kwa abiria.
Naye, Makamu wa rais wa kampuni hiyo Africa, Hadi Akoum amesema licha ya kuwepo kwa oda nyingi za kutengeneza ndege kwenye kampuni yao, ana matumaini kuwa ndege hizo zitatengenezwa na kukamilika kwa muda muafaka.
“Uchongaji wa ndege sio jambo rahisi linachukua muda na kwa ndege za aiana hii kwa kawaida huchukua mwaka mmoja hadi mwaka mmoja na nusu na sasa tuna oda nyingi tunapaswa kutengeneza ndege walau ndege mbili na nusu za aina hiyo,” amesema Akoum aliponukuliwa na gazeti la Mwananachi.
Soma zaidi:
- Waziri azungumzia ndege za ATCL kuchelewa, kuahirisha safari
- Shirika la ndege la Ethiopia limesitisha safari zote za ndege aina ya Boeing 737
- ATCL inavyojitanua kimataifa
Kwa mujibu wa Airbus yenye, bei ya ndege hizo kwa mwaka 2018 ilikuwa ni Dola za Kimarekani milioni 91.5 kwa ndege moja hivyo kwa ndege mbili ni zaidi ya Sh420.5 bilioni.
Mkurugenzi mkuu wa Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) Ladislaus Matindi amesema ndege aina ya Airbus A220-300 imeonyesha mafanikio makubwa katika shirika katika suala la utumiaji wa mafuta na mengine.
Amesema pindi zitakapokuja ndege hizo, shirika litaongeza ufanisi na mtandao wake wa safari kama ambavyo mpango mkakati unaelekeza.
“Soko letu lina mahitaji makubwa kuliko uwezo wetu wa kulihudumia,” amesema Matindi.