Wekeni mikakati kudhibiti uhalifu-Majaliwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa polisi katika nchi za mashariki mwa Afrika waweke mikakati thabiti ya kukabiliana na magenge ya uhalifu unaovuka mipaka ikiwemo kuimarisha ushirikiano.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akihutubia kwenye ufunguzi wa Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Polisi wa Nchi za Mashariki mwa Afrika (EAPCCO), katika ukumbi wa AICC Arusha, Septemba 19.2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.
- Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa polisi katika nchi za mashariki mwa Afrika waweke mikakati thabiti ya kukabiliana na magenge ya uhalifu unaovuka mipaka.
- Mikakati hiyo ni pamoja na mafunzo, upelelezi wa pamoja na ubadilishanaji wa taarifa za kiintelijensia.
- Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro akabidhiwa uenyekiti wa EAPCCO.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa polisi katika nchi za mashariki mwa Afrika waweke mikakati thabiti ya kukabiliana na magenge ya uhalifu unaovuka mipaka ikiwemo kuimarisha ushirikiano ili wahalifu hao wasipate mahali salama pa kufanya uhalifu.
Majaliwa aliyekuwa akizungumza leo (Septemba 19, 2019) wakati akifungua mkutano mkuu wa 21 wa Shirikisho la Wakuu wa Oolisi Mashariki mwa Afrika (EAPCCO) jijini Arusha, amesema wahalifu wanatumia udhaifu wa kukosekana ushirikiano madhubuti miongoni mwa nchi hizo.
“Ili kutokomeza uhalifu wa aina yoyote utashi wa kisiasa unahitajika sana. Lengo ni kuvipatia nguvu vyombo vya dola katika kusimamia sheria.
“Niwatake wanasiasa wengine tutoe ushirikiano kwa vyombo hivi ili viwe na meno kwa kutunga sheria zitakazowawezesha kufanya kazi zao ipasavyo,” amesema Majaliwa.
Ushirikiano unaohitajika katika kuzuia uhalifu ni pamoja na mafunzo kwa watendaji, operesheni za pamoja, upelelezi wa pamoja na ubadilishanaji wa taarifa za kiintelijensia ili kuyasaka, kuyabaini na kuyakamata magenge ya watuhumiwa wanaofanya makosa katika nchi moja na kwenda kujificha katika nchi nyingine.
Soma zaidi:
- Majaliwa: Nawaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii waache
- Majaliwa aagiza elimu itolewe upangaji madaraja ya korosho
Amesema mfumo wa uhalifu duniani kwa sasa unachukua sura mpya kufuatia kukua kwa teknolojia hususani ya habari na mawasiliano, uhuru wa watu na bidhaa kuvuka mipaka pamoja na kuondolewa vikwazo vingi visivyo vya kiforodha.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, maendeleo hayo kwa upande mwingine yameleta athari za kiusalama kwani wahalifu nao wanatumia fursa hiyo kuimarisha magenge yao ya uhalifu unaovuka mipaka ikiwemo biashara ya dawa za kulevya.
“Uhalifu mwingine ni wizi wa magari, ujangili, utoroshaji madini na biashara haramu ya binadamu, ugaidi, utengenezaji na uuzaji wa bidhaa bandia na uharamia katika maziwa na baharini, utakatishaji wa pesa zinazotokana na uhalifu huo na vitendo vya rushwa,” amesema Majaliwa. Katika hatua nyingine, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Simon Sirro aliekabidhiwa uenyekiti wa EAPCCO ameahidi kutoa ushirikiano mzuri kwa viongozi wenzake ili kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kuwepo katika nchi zao.
Amekabidhiwa uenyekiti wa shirikisho hilo na Mkuu wa Jeshi la Polisi la Sudan na mwenyekiti wa shirikisho la wakuu wa polisi mashariki mwa Afrika anayetoka kitini, Luteni Jenerali Adil Mohammed.