October 6, 2024

Wataalam wa uchumi watoa suluhisho la biashara kufungwa Tanzania

Kutokana na ushindani na mabadiliko ya mazingira ya biashara, baadhi ya kampuni zimesitisha kutoa huduma. Lakini watalaam wa uchumi watoa suluhisho ikiwemo kufanya tafiti za masoko kabla ya kuanzisha biashara.

  • Washauri kufanya utafiti wa masoko na mazingira ya biashara kabla ya kufungua kampuni. 
  • Pia zatakiwa kuzingatia sheria za nchi na kuepuka “ujanja ujanja”.
  • Serikali imesema imeanza kuboresha mazingira ya biashara ikiwemo miundombinu na kodi na tozo mbalimbali.

Dar es Salaam. Kila mara jambo lenye umuhimu na manufaa kwa Tanzania linapoanzishwa, ni matarajio ya watanzania wengi kuwa jambo hilo litaendelea kuwepo kwa muda mrefu ili wanufaike na kuboresha maisha yao.

Kuanzishwa kwa miradi, makampuni na mifumo mbalimbali ya teknolojia ya ndani na nje ya nchi kumesaidia kupunguza changamoto zinazomkabili Mtanzania.

Kutokana na ushindani na mabadiliko ya mazingira ya biashara, baadhi ya kampuni zimesitisha shughuli na zile za kimataifa zimefunga virago na kurejea katika nchi zao. 

Hivi karibuni, Tala ambayo ni kampuni ya kidijitali ya kutoa mikopo kwa njia za simu za mkononi imesitisha shughuli zake nchini Tanzania kwa ajili ya kufanya tathmini ya soko kama iendelee kutoa huduma au iache. 

“Tunasikitika kukutaarifu kuwa kwa sasa Tala haitoi mikopo nchini Tanzania,” imeandikwa na kampuni hiyo kupitia ukurasa wake mtandao wa instagram.

Kufungwa kwa huduma iliyonufaisha zaidi ya Watanzania milioni tatu kwa mitaji midogo midogo, huenda ikawa ni pigo kwa wananchi waliokuwa wanategemea huduma hiyo.

Emmanuel Sungwa ni mmoja ya watumiaji wa huduma za Tala, yeye anasema Tala ilimsaidia kumalizia malipo ya ada ya chuo wakati mzazi wake aliposhindwa kumlipia.

“Kuna kipindi baba alipeleza kama Sh50,000. Nilijaribu kuomba kwa washikaji lakini sikupata. Mmoja wa marafiki zangu alinielezea kuhusu Tala na ndipo nilipo pata mkopo na kumalizia malipo ya ada,” anasema Sungwa.

Baadhi ya kampuni zimesitisha shughuli na zile za kimataifa zimefunga virago na kurejea katika nchi zao. Picha| Mtandao

Mdau wa teknolojia na Mkurugenzi wa kampuni ya Nala Benjamin Fernandes amehusisha tukio la Tala kushitakiwa kwa kosa la uhujumu uchumi pamoja na Vodacom Tanzania na kesi ambayo ilikabiri kampuni ya Tala na Vodacom mapema 2019.

Kupitia ukurasa wake wa twitter, @Benji_Fernandes amesema “miezi michache iliyopita, Tala Tanzania yenye makao yake California inayotoa mikopo Tanzania ilikabiliwa na kesi ya kisheria. Hakuna mshangao, miezi minne baadaye, Tala imejitoa kwenye masoko ya Tanzania”

Fernandes amesema hatua hiyo siyo dalili njema hasa kwa kampuni  za teknolojia zinazochipikia ambazo zinatoa huduma nchini.

Pia mwishoni mwa mwaka 2018 kampuni ya usafiri wa ndege ya FastJet pia ilishitisha safari zake kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo madeni na ukosefu wa menejimenti madhubuti ya kuongoza kampuni. 

Biashara zingine zilizofungwa ni maduka makubwa ya Nakumatt, Uchumi na sasa maduka ya Choppies nayo yanasua sua.

Hivi karibuni, duka la Choppies la Makumbusho limefungwa na hata tawi lake la Mlimani City la jijini Dar es Salaam, halina muonekano ulioshiba kama maduka mengine.


Zinazohusiana


Nini kifanyike kuokoa biashara zisifunge?

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Profesa Damian Gubagambi amesema suala la makampuni kufunga biashara ni jambo la kawaida.

Mtaalamu huyo wa masuala ya uchumi, amesema pale biashara moja inapofungwa ni fursa kwa biashara nyingine kufunguliwa na siyo kitu cha ajabu pale kampuni linapoamua kufunga biashara yake.

Amebainisha kuwa zipo baadhi ya kampuni zinashindwa kuendana na sheria za nchi ikiwemo kukwepa kodi, jambo linalozifanya zikwame  pale zinapotakiwa kufanya hivyo.

“Cha msingi wafuate sheria za nchi, walipe kodi wasifanye janja janja,” amesema Prof. Gubagambi.

Aidha, Serikali imeanza kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara (BluePrint) ulioidhinishwa mwaka 2017/18 kwa kuanza kupitia mfumo wa tozo na ada mbalimbali zinazotozwa na Mamlaka za Udhibiti kwa lengo la kupunguza au kuzifuta baadhi ya tozo na ada, kupunguza na kuondoa muingiliano katika kutoza tozo hizo.

Mhadhiri wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), Dk John Msumba amesema kinachowakwamisha wawekezaji wengi na hadi kusababisha kufunga biashara ni pamoja na kushindwa kufanya utafiti wa masoko kabla ya kuwekeza.

Amesema, makampuni mengi “yanakurupuka” bila kutumia tafiti za muda mrefu na hivyo kupelekea kampuni hizo kufeli katika biashara.

Ameshauri makampuni kufanya tafiti kabla ya kuwekeza na pia kutoa mafunzo kwa watu ili watu wafahamu ni nini wanafanya. Kinyume na hapo, ni rahisi kwa kampuni yeyote kupoteza mwelekeo na hivyo kufunga biashara.

“Wawekezaji hawafanyi tathmini ya masoko. Lazima uwekeze kwenye kutoa mafunzo ili wateja wako waifahamu bidhaa yako,” amesema.