November 24, 2024

Viwanda vya ndani kupewa kipaumbele ununuzi wa korosho 2019

Serikali imesema itatoa nafasi ya kwanza ya ununuzi wa korosho msimu huu kwa wenye viwanda nchini ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na zao hilo.

  • Serikali imesema itatoa nafasi ya kwanza ya ununuzi wa korosho msimu huu kwa wenye viwanda nchini ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na zao hilo.
  • Serikali imepanga kuimarisha mifumo ya ununuzi wa zao hilo ili kuwanufaishja wakulima na wanunuzi. 
  • Wizara ya Kilimo na Biashara zatakiwa kusaka masoko ya korosho iliyopo ghalani.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema katika msimu wa ununuzi wa korosho wa mwaka huu, Serikali imepanga kuimarisha mifumo ya ununuzi wa zao hilo na kipaumbele kitatolewa kwa wenye viwanda vya ndani. 

Amesema Serikali itatoa nafasi ya kwanza ya ununuzi kwa wenye viwanda nchini, hivyo amewataka waandae mahitaji yao na kuyawasilisha kwenye mamlaka husika ili wawe na uhakika wa kupata malighafi ya kutosheleza mahitaji ya viwanda vyao.

Majaliwa aliyekuwa akizungumwa leo (Septemba 13, 2019) wakati akiahirisha mkutano wa 16 wa Bunge la 11, Bungeni jijini Dodoma, amesema wakulima wataarifiwa kuhusu utaratibu wa uuzaji wa zao hilo kwenye kikao cha wadau kitakachofanyika hivi karibuni.

Amesema Serikali imepanga kupanua soko la korosho kwa kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kutengeneza bidhaa nyingine zitokanazo na zao hilo zikiwemo siagi, maziwa, mvinyo na sharubati.

Ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa, Waziri Mkuu ameielekeza Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhakikisha zinasimamia upatikanaji wa masoko mapya ya korosho.  


Zinazohusiana:


Waziri Mkuu amesema katika msimu wa 2018/2019 jumla ya tani 224,964 za korosho ghafi zenye thamani ya sh729.90 bilioni  zilikusanywa. Kati yake tani 222,825 zilikusanywa na Serikali.

 “Korosho zilizolipwa ni tani 197,547 na Serikali inakamilisha malipo ya kiasi kilichobaki cha tani 25,278. Hivi sasa, korosho yote imenunuliwa na inasafirishwa. Aidha, baada ya zoezi hilo Bodi ya Mazao Mchanganyiko itarudi kulipa madeni yaliyobaki kwa wakulima na wenye maghala,” amesema Majaliwa.  

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo ihakikishe inawasimamia ipasavyo mawakala waliopewa jukumu la kusambaza pembejeo kwa wakulima ili ziwafikie wakulima kwa wakati na kwa bei inayohimilika na ubora unaohitajika.

Amesema katika kipindi cha kuanzia Septemba 2019 maeneo mengi nchini huanza kupata mvua za vuli ambazo ni ishara ya kuanza kwa msimu mpya wa kilimo, hivyo Serikali lazima ihakikishe wakulima wanapata pembejeo za kilimo ikiwemo mbegu bora, mbolea na viuatilifu kwa ajili ya msimu huu mpya wa kilimo.