Fanya haya kupunguza ongezeko la lehemu mbaya mwilini
Katika sehemu hii ya pili, utaifahamu lehemu mbaya na vyanzo vyake na namna gani unaweza kuishinda kwa njia rahisi ambazo mtu yeyote anaweza kufanya.
- Baadhi ya mambo hayo ni kufanya mazoezi, badili mtindo wa nmaisha ikiwemo kula vizuri.
- Lehemu mbaya ikijikusanya kwenye mishipa mikubwa ya damu (arteries) husababisha kuziba kwa mishipa ya damu kiharusi.
- Lehemu mbaya ikizidi mwilini inaweza kusababisha kiharusi na unene uliopitiliza.
- Unashauriwa kumuona daktari ili kufahamu kiasi cha lehemu kilichopo mwilini na jinsi ya kudhibiti.
Dar es Salaam. Katika makala iliyopita tulikufahamisha maana ya lehemu na ipi ni nzuri katika mwili wako na vyanzo vya kuipata.
Katika sehemu hii ya pili, utaifahamu lehemu mbaya na vyanzo vyake na namna gani unaweza kuishinda kwa njia rahisi ambazo mtu yeyote anaweza kufanya.
Lehemu mbaya inatokana na vyakula ambavyo vina wapenzi wengi. Kati ya vyakula hivyo ni pamoja na nyama nyekudu, siagi, mafuta ya mawese na baadhi ya vyakula vinavyotengenezwa viwandani.
Jambo lakushangaza zaidi, vyakula vingi ambavyo vina lehemu nzuri sio vya gharama kama vile vyenye lehemu mbaya. Hivyo ni kusema lehemu mbaya ni ghari kuliko lehemu nzuri.
Mfiziotherapia, Dk Joshua Sultan ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Tiba na Afya cha KCMC Moshi anasema lehemu mbaya (Low density lipoproteins) huzunguka ndani ya damu huku ikijikusanya kwenye mishipa mikubwa ya damu (arteries) na hivyo kupelekea kuziba kwa mishipa hiyo.
Mishipa hiyo ikiziba huwa mikavu ndani na kubana (arteriosclerosis). Hali hiyo ina sababisha mzingo wa mshipa kuwa mdogo na mshipa hupungua uwezo wake wa kutanuka kuruhusu damu kupita bila nguvu ya ziada hivo mfumo huulazimisha moyo kuongeza nguvu ya mapigo ili damu ipite vizuri.
Mwendelezo wa hali hiyo inaweza kufanya chembe chembe za mafuta hayo kumeguka na kuingilia mfumo wa mzunguko wa damu (emboli) kisha kuziba eneo fulani na kusababisha kushindwa kufika kwa damu eneo hilo.
“Chembe chembe hizi za cholesterol hujikusanya na huongeza hatari ya damu kushindwa kufika eneo husika. Wakati hushindwa kuifikia baadhi ya maeneo ikiwa imeziba na hivo kupelekea shambulio la moyo (heart attack),” amesema Dk Sultan.
Soma zaidi:
- Jilinde dhidi ya ongezeko la mafuta mwilini kuepuka gharama kubwa za matibabu.
- Jinsi unavyoweza kuishinda sonona isiharibu maisha binafsi, kazi
- Mambo yatakayokusaidia kupunguza hatari ya kupata saratani
Mbali na shambulio la moyo, mafuta mabaya mwilini pia huweza kubana mishipa iendayo kwenye ubongo na kuziba na kusababisha shambulio la kiharusi (stroke).
Sultan amesema madhara ambayo mtu anaweza kuyapata baada ya lehemu hii kujikusanya ni mengi na tiba yake ni gharama kuliko hata mtu anavyoweza kujikinga hivyo ni bora kujiweka katika mazingira ya afya nzuri kwa kula mboga za majani, mboga jamii ya kunde na nyama nyeupe kama samaki.
Kwa mtu ambaye tayari ameshapata madhara ya uwepo wa lehemu mbaya nyingi mwilini anashauriwa kuonana na daktari kwa ajili ya kuandikiwa dawa za matibabu.
Kama ilivyozungumziwa katika sehemu ya kwanza ya makala hii, matibabu ya kiharusi na shambulio la moyo ni kati ya matibabu yenye gharama kubwa hivyo kinga ni bora kuliko tiba.
Vyakula vingi ambavyo vina lehemu nzuri sio vya gharama kama vile vyenye lehemu mbaya. Picha| Mtandao.
Mbali na dawa za hospitalini, zipo njia zingine mbali na chakula ambazo mtu anaweza kuzitilia maanani kwa ajili ya kuhakikisha hapati madhara yanayotokana na wingi wa lehemu mbaya mwilini.
Badilisha lishe yako
Unahitaji kupunguza kiasi cha vyakula vyenye mafuta ghafi ikiwemo nyama ya ng’ombe, mbuzi na baadhi ya bidhaa zilizookwa. Pia unahitaji kutumia mafuta yenye lehemu ndogo kwa kupikia chakula chako kwa kutumia mafuta ya alizeti badala ya mafuta ya mawese.
Punguza uzito wako
Kuna namna nyingi za kupunguza uzito ikiwemo kula kwa mpango na kufanya mazoezi. Sultan anasema mtu mwenye uzito uliozidi “hasa wenye BMI zaidi ya 30” ni hatari hivyo kuna haja ya kuupunguza kwa namna yeyote ile ikiwemo kufanya mazoezi.
Badili mtindo maisha wako
Kuna haja ya kuepuka mambo mbalimbali ikiwemo uvivu, kunywa pombe uvutaji wa sigara kwani kwa kuvuta sigara, mtu anasababisha kupanda kwa kiwango cha lehemu mbaya mwilini.
Endelea kufuatilia makala za afya mbalimbali kupitia ukurasa huu.