October 7, 2024

Majaliwa atoa maagizo makuu matatu kwa Miss Tanzania 2019

Amemtaka Miss Tanzania 2019, Sylivia Bebwa ahakikishe anakuwa balozi mzuri wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, shughuli za maendeleo zinazofanywa na Serikali na aishi kwa kuzingatia utamaduni wa Mtanzania.

  • Amemtaka Miss Tanzania 2019, Sylivia Bebwa ahakikishe anakuwa balozi mzuri wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, shughuli za maendeleo zinazofanywa na Serikali na aishi kwa kuzingatia utamaduni wa Mtanzania.
  • Miss Tanzania anajiandaa kwenda kushiriki katika mashindano ya “Miss World” yanayotarajiwa kufanyika London, Uingereza Desemba 14 mwaka huu.
  • Sylivia asema yuko tayari kutekeleza maagizo yote aliyopewa na Waziri Mkuu. 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemtaka Miss Tanzania 2019, Sylivia Bebwa ahakikishe anakuwa balozi mzuri wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, shughuli za maendeleo zinazofanywa na Serikali na aishi kwa kuzingatia utamaduni wa Mtanzania.

Waziri Mkuu amezungumzia masuala hayo Septemba 11, 2019 wakati alipokutana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, waandaaji wa mashindano ya Miss Tanzania na mshindi wa pili na watatu wa shindano hilo, ofisini kwa Waziri Mkuu Mlimwa Jijini Dodoma.

Amesema Miss Tanzania anatakiwa kutumia fursa hiyo kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini, shughuli zinazofanywa na Serikali katika kukuza uchumi pamoja na kuhamasisha wananchi washiriki katika kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa.

“Miss Tanzania lazima awe mbunifu na uelewa mpana katika masuala mbalimbali zikiwemo jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha maendeleo ya wananchi kama kuhamasisha elimu hususan kwa watoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao,” amesema

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Miss Tanzania pamoja na washiriki wengine wa mashindano hayo wanatakiwa waishi kwa kuzingatia utamaduni wa Mtanzania ikiwemo kuwa na nidhamu katika jamii ili waweze kuwashawishi wengine kushiriki.


Zinazohusiana: 


Kwa upande wake, Dk Mwakyembe amemshukuru Waziri Mkuu kwa kukubali kuonana na ujumbe huo hususani Miss Tanzania ambaye anajiandaa kwenda kushiriki katika mashindano ya mlimbwende wa dunia (Miss World) yanayotarajiwa kufanyika London, Uingereza Desemba 14 mwaka huu.

Waziri huyo amesema miaka ya nyuma Serikali haikuridhishwa na namna mashindano hayo yalivyokuwa yakiendeshwa lakini kwa sasa hali ni tofauti na yamekuwa na viwango vya kimataifa. 

Mashindano hayo kwa sasa yanasimamiwa na aliyekuwa Miss Tanzania 2008, Basilla Mwanukuzi kupitia kampuni ya The Look.

Naye, Mwandaaji wa Mashindano hayo, Basilla Mwanukuzi ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa ushirikiano inaoutoa kwao na pia ameiomba izidi kuwaunga mkono kwa kuwa watatumia mashindano hayo katika kulitangaza Taifa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Miss Tanzania 2019, Sylivia Sebastian, nje ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa, jijini Dodoma, Septemba 11.2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.

Awali, Miss Tanzania 2019, Sylivia ameishukuru Serikali kwa fursa aliyopewa ya kukutana na Waziri Mkuu na amesema kuwa atajitahidi katika kuhakikisha anatekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwemo kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Miss World na kwamba anakwenda kutumia lugha ya kiswahili.

“Nimefurahi kwa heshima hii niliyopewa na Serikali ya kukutana na Mheshimiwa Waziri Mkuu, naahidi kwamba niyatekeleza maagizo yote aliyoyatoa ikiwa ni pamoja na kuishi kwa kuzingatia maadili ili wazazi wengine waweze kuwaruhusu watoto wao washiriki katika mashindano haya kwani urembo ni heshima,” amesema Sylivia