October 6, 2024

Kila sekunde 40 mtu mmoja anapoteza uhai kwa kujiua-WHO

Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Kujiua, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kila sekunde 40 mtu mmoja anafariki kwa kujiua, licha ya kuwa matukio hayo yanaweza kuzuilika ikiwa elimu itatolewa kwa jamii.

  • Njia ambazo zimezoeleka zaidi kwa watu kujitoa uhai ni kujinyong’a, kunywa sumu ya kuulia wadudu na matumizi ya silaha.
  • Sababu ya watu kujiua ni magonjwa ya akili, msongo wa mawazo, ugumu wa maisha na majanga. 
  • Serikali zashauriwa kuongeza mikakati ya kunusuru uhai wa watu wake. 

Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Kujiua, Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kila sekunde 40 mtu mmoja anafariki kwa kujiua, licha ya kuwa matukio hayo yanaweza kuzuilika ikiwa elimu itatolewa kwa jamii. 

Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Kujiua huadhimishwa Septemba 10 kila mwaka ikiwa ni hatua ya kutathmini hatua zinazochukuliwa kudhibiti visa vya watu kujiua wenyewe. 

Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus iliyotolewa jana inaeleza kuwa kifo cha aina yoyote ni pigo kwa familia na jamii hasa kama mtu aliyefariki alikuwa akitegemewa kuwasaidia wengine.  

“Pamoja na hatua zilizopigwa, mtu mmoja bado anafariki dunia kwa kujiua kila sekunde 40,” amesema Dk Ghebreyesus na kuongeza kuwa.

“Kila kifo ni janga kwa familia, marafiki na jamaa. Wakati huo huo kujiua kunazuilika. Tunatoa wito kwa nchi zote kuingiza mikakati ya kuzuia kujiua katika programu za kitaifa za afya na elimu kwa namna endelevu.”

Njia ambazo zimezoeleka zaidi kwa watu kujitoa uhai ni kujinyong’a, kunywa sumu ya kuulia wadudu na matumizi ya silaha.

Bosi huyo wa WHO amesema idadi ya visa vya kujiua viko juu katika nchi zenye kipato cha juu ambapo ni sababu ya pili inayosababisha vifo miongoni mwa vijana. 

“Kiwango cha wastani cha kujiua ulimwenguni kwa mwaka 2016 kilikuwa ni watu 10.5 kwa kila watu 100,000,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo. 

Hata hivyo,  viwango vilikuwa na tofauti kati ya nchi na nchi kutoka kwa watu watano wanaojiua kati ya watu 100,000 hadi kufikia zaidi ya watu 30 kwa watu 100,000. 

Wakati asilimia 79 ya visa vya kujiua kote duniani vilitokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati, huku nchi za kipato cha juu zilikuwa na viwango vya juu kwa watu 11.5 kati ya watu 100,000.

Njia ambazo zimezoeleka zaidi kwa watu kujitoa uhai ni kujinyong’a, kunywa sumu ya kuulia wadudu na matumizi ya silaha. Picha|Mtandao.

Sababu za watu kujiua

Mtaalam wa saikolojia kutoka kampuni ya DM Saikolojia Limited, Dosi Said Dosi  anasema kujiua ni kitendo cha mtu kujitoa uhai ambapo hupelekea kufariki. 

Anasema watu wengi huamua kujiua kwasababu hukosa tumaini na kushindwa kuona suluhu ya changamoto za maisha zinazowakabili. Hivyo wazo la kujiua huja kama njia ya mkato ya kutatua changamoto zinazowakabili.

“Mtu ambaye anahuzunika sana na kukosa raha kwa muda mrefu hupelekea kuwa na mawazo ya kujaribu kujiua. Mfano mtu kila akifanya jambo halifanikiwi kila analofanya halileti mrejesho mzuri na kumfanya maisha yake kuwa na changamoto juu ya changamoto hadi anapata sonona,” amesema Dosi.

Matumizi ya vilevi kama pombe, bangi na dawa za kulevya humuweka mtu katika hatari ya kujaribu kujiua kutokana na akili yake kutawaliwa na vilevi anavyotumia.

Historia kujiua katika familia pia inaweza kuchangia watu kujiua kutokana na kuona baadhi ya wanafamilia wamefanya hivyo. 

“Kuona (Suicide contagion), baadhi ya watu huamua kujiua kutokana na wao kuona mtu kajiua au wameona watu wamejiua kwenye mitandao ya kijamii, habari au tamthilia. Hii hutokea kwa kasi kwenye jamii na idadi huwa ni kubwa ya watu kujiua,” anabainisha mtaalam huyo.

Dosi ambaye amekuwa akitoa ushauri wa saikolojia anasema baadhi ya watu ambao zamani walishawahi kujaribu kujiua nao wapo katika hatari ya kujaribu tena kujiua.


Soma zaidi:


Utamjuaje mtu mwenye dalili za kujiua?

Kwa mujibu wa taaluma ya saikolojia ya mwanadamu, kile anachokitamka mtu anaweza kukiweka katika matendo kiwe ni kibaya au kizuri. 

“Mtu anayetaka kujiua huanza kuzungumza kuhusu kifo na baadaye hujaribu kitendo chenyewe. Pia mtu huwa hana hamu ya kufanya kazi, kujumuika na watu na kufanya mambo ya kijamii,” anasema Dosi.  

Dalili nyingine ambayo Dosi ameweka mbali ni mtu anayetaka kujiua hujishusha na kujiona hana thamani, hana faida  kwa jamii na kuona aibu lakini anaweza kukosa hamu ya kula kabisa au akawa anakula kupita kiasi. 

Pia mtu huyo anaweza kukosa usingizi nyakati za usiku au akawa na mazoea ya kulala muda mrefu kuliko kawaida.

Hata hivyo,  siyo kila mtu anayeonyesha dalili hizo hapo juu anataka kujiua, zinaweza kusababisha jambo lingine ambalo halihusiani na kifo.

Wanaojiua zaidi ni wanaume au wanawake?

Dosi anasema wanawake wengi hujaribu kujiua kuliko wanaume lakini wanaume wengi hujiua zaidi kuliko wanawake.

Taarifa ya WHO inaeleza kuwa kwa viwango vya wastani vya kujiua ulimwenguni kwa mwaka 2016 visa vya kujiua kwa wanaume wa nchi zilizoendelea ilikuwa ni mara tatu ya wanawake katika nchi hizo.

Lakini ni tofauti katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati ambapo viwango vya visa kati ya wanawake na wanaume vinalingana. Kujiua kulikuwa sababu ya pili baada ya ajali za barabarani inayosababisha vifo miongoni mwa vijana wa umri wa miaka 15 hadi 29. 

Dalili nyingine ambayo Dosi ameweka mbali ni mtu anayetaka kujiua hujishusha na kujiona hana thamani, hana faida  kwa jamii na kuona aibu lakini anaweza kukosa hamu ya kula kabisa au akawa anakula kupita kiasi. Picha|Mtandao.

Serikali na wadau wapunguze matukio ya kujiua

Kwa mujibu wa WHO, njia ambazo zimeonesha kusaidia kupunguza visa vya kujiua ni pamoja na kuzuia kuweza kufikia vitu vya kutumia kujiua, kuelimisha vyombo vya habari kuhusu namna ya kuripoti matukio ya kujiua.

Pia kufanya programu miongoni mwa vijana katika kujenga stadi zinazowawezesha kukabiliana na msongo wa mawazo katika maisha, utambuzi wa mapema na  jinsi ya kuwafuatilia watu walioko hatarini kujiua.

Udhibiti wa manunuzi ya sumu za kuulia wadudu unasaidia sana kupunguza uwezekano wa watu kujiua. 

Lakini mikakati ya kitaifa ni muhimu zaidi ili kuhakikisha Serikali za nchi mbalimbali zinalipa kipaumbele suala hilo katika sera na sheria zitakazosaidia kupunguza matukio ya watu kujiua. 

Hata hivyo,  WHO imesema nchi ambazo zina mikakati ni 38 na bado ni chache hivyo Serikali zinatakiwa kuhakikisha zinaanzisha mikakati hiyo.

Hatua ya kwanza ni kutambua kama kujiua ni tatizo, anasema Dosi kuwa baadhi ya watu hawafahamu kama kujiua ni tatizo na hivyo hujikita katika masuala mengine tu. 

Unatakiwa ufahamu ujuzi na njia mbalimbali za kukabiliana na changamoto za maisha ili kuepuka kuingia kwenye msongo wa mawazo na baadaye kujiua. 

“Uwe na mahusiano mazuri na marafiki na familia. Hii itakusaidia kuweza kuwasiliana nao pale unapokuwa na changamoto au unapoona mwenzako au mtoto wako ana changamoto za kimaisha,” ameshauri Dosi.

Tunakumbushwa kuweka mbali vitu hatarishi kama visu, mapanga, silaha na bastola, zinazoweza kutumiwa katika wakati tusioutegemea.  

Upatikanaji rahisi wa huduma za kisaikolojia kwenye jamii unaweza kuwasaidia watu kufahamu suluhisho pale wanapokumbana na changamoto za maisha.