Faida ya Swissport Tanzania yashuka
Kampuni ya Swissport Tanzania inayotoa huduma za ndege imeripoti kushuka kwa faida inayotengeneza kwa asilimia 50 katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo wa mwaka 2019.
- faida za kampuni ya Swissport Tanzania imeporomoka kutoka Sh4.9 bilioni mwaka 2018 hadi Sh2.3 bilioni katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka huu.
- Sababu za kushuka kwa mapato hayo ni pamoja na kung’atuka kwa kampuni ya FastJet Tanzania kwenye utoaji huduma za usafiri wa anga nchini.
- Sambamba na faida, mapato na gharama za uendeshaji pia zimeshuka ikilinganishwa kwa mwaka 2018.
Dar es Salaam. Kampuni ya Swissport Tanzania inayotoa huduma za ndege imeripoti kushuka kwa faida inayotengeneza kwa asilimia 50 katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo wa mwaka 2019.
Kampuni hiyo ya Swissport inajishughulisha na upakuaji na utumaji wa mizigo katika viwanja vya ndege kama Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Swissport Tanzania imeeleza chanzo kikubwa cha kushuka kwa nusu ya mapato yake ni kusimamishwa kwa kampuni ya FastJet Tanzania kutoa huduma za usafiri wa ndege.
Fastjet iliondoka sokoni mwishoni wa Decemba 2018 baada ya kukosa sifa ya kuendelea kutoa huduma za usafiri wa anga Tanzania ikiwemo madeni na kukosa menejimenti ya kuongoza kampuni.
Kwa mujibu wa ripoti ya nusu mwaka ya Swissport iliyowekwa katika tovuti ya Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), faida za kampuni ya Swissport Tanzania imeporomoka kutoka Sh4.9 bilioni mwaka 2018 hadi Sh2.28 bilioni katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka huu.
Kushuka kwa faida ya Swissport kumechangiwa na kushuka kwa mapato na gharama za uendeshaji wa kampuni hiyo.
Katika kipindi hicho mapato yameshuka kutoka Sh25 bilioni hadi Sh17.2 bilioni na gharama za uendeshaji zimeshuka kutoka Sh17.6 billioni hadi Sh14bilioni .
Aidha, kampuni hiyo imehusisha kushuka kwa mapato yake na kupungua kwa biashara ya usafiri wa anga ikiwemo kupungua kwa safari za ndege.
Swissport Tanzania imeeleza chanzo kikubwa cha kushuka kwa nusu ya mapato yake ni kusimamishwa kwa kampuni ya FastJet Tanzania kutoa huduma za usafiri wa ndege. Picha| Mtandao
Ifahamike kuwa, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, (TCAA) ilitoa kibali kwa kampuni ya NAS-Dar Airco kufanya shughuli za kudhibiti mizigo kwenye uwanja wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kushughulikia udhibiti wa mizigo ya wasafiri wote wanaotumia ndege za Shirika la Ndege la “Air Tanzania” ikiwa ni kuongeza ufanisi wa shughuli hizo.
Hatua hiyo imeiacha kampuni ya “Swissports” ikichechemea na kukosa soko hasa baada ya mdau wake mkubwa “FastJet” kung’oka katika utoaji huduma za usafiri wa anga nchini.
Zinazohusiana:
- Air Tanzania kuajiri wahudumu wa ndege 88 kuimarisha uendeshaji
- Nini kinafuata baada ya Fastjet kusitisha safari zake?
- Mamlaka ya anga Tanzania yakusudia kulifuta shirika la ndege la Fastjet
Mwanyekiti wa Swissport Tanzania, Mark Skinner amesema kukoma kwa biashara ya Fasjet nchini ni pigo kubwa kwa biashara ya kampuni hiyo.
Pamoja na hayo, Skinner amesema hawakusudii kusitisha biashara nchini badala yake kampuni imejipanga kurudi kwenye chati yake kwa kuanzia na ubanaji wa matumizi kwa ajili ya kuimarisha hali ya kiuchumi ya kampuni hiyo.
“Kuendana na mabadiliko na mahitaji ya mazingira ya biashara, tutaendelea kuongeza utendaji kazi, udhibiti wa gharama za operesheni na kuwekeza kwenye vifaa, teknolojia na ukuaji wa nguvukazi ili kuhakikisha tunazidi matarajio ya wateja wetu na kuweka mazingia bora ya wafanyakazi wetu,” amesema Skinner