October 6, 2024

Serikali yaeleza sababu za ATM kukosa miundombinu kwa wasioona

Yasema mashine za kutolea fedha (ATM) zilizopo nchini hazina mifumo inayoendana na watu wasioona.

  • Yasema mashine za kutolea fedha (ATM) zilizopo nchini hazina mifumo inayoendana na watu wasioona. 
  • Pia teknolojia ya ATM kwa watu wasioona ni ngeni kwa Tanzania. 
  • Yasema inalifuatilia suala hilo ili kukidhi mahitaji ya makundi yote kwenye jamii.

Dar es Salaam. Serikali imesema kukosekana kwa mifumo na miundombinu ya mashine za kutolea fedha (ATM) katika benki za Tanzania ambazo ni rafiki kwa watu wenye ulemavu wa macho kunatokana na teknolojia ya mashine hizo kuwa ni ngeni nchini. 

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji amelieleza Bunge leo (Septemba 9, 2019) wakati kuwa mpaka sasa benki zote za Tanzania hazijafanikiwa kuwa na mifumo rafiki kwa watu wenye ulemavu wa macho kutokana na ukweli kuwa ATM za kawaida zilizopo hazijatengenezwa mahususi kwa watu wasioona.

“Pamoja na Serikali kutoa mwongozo huo, benki zetu zote hapa nchini hazijafanikiwa kusimika ATM maalum na rafiki kwa watu wenye ulemavu hususan watu wenye ulemavu wa macho, hii ni kutokana na ukweli kwamba teknolojia ya ATM kwa  watu wenye ulemavu wa macho ni ngeni na pia ina mfumo wa mahitaji ya ziada ikilinganishwa na ATM za kawaida,” ameeleza Dk Kijaji.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Amina Mollel aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa ATM za mabenki  zinawekewa mifumo inayokidhi mahitaji ya watu wenye ulemavu.


Inayohusiana:


Amesema mwaka 2017,  Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilitoa muongozo wa mfumo wa malipo kwa njia ya mtandao ikiwa ni  mpango wa Serikali wa kuhakikisha kuwa huduma za malipo kwa njia ya mtandao yanafanyika kwa usalama na kukidhi mahitaji ya makundi yote.  

Miongoni mwa vipengele muhimu na nyeti hususan kwa walemavu vilivyoainishwa kwenye muongozo huo ni alama za utambuzi, usalama na uwezo wa mifumo kutunza siri za wateja.

Hata hivyo, amesema Serikali inafuatilia suala hilo kwa ukaribu ili kuhakikisha makundi yote katika jamii wakiwemo wasioona wanapata huduma za kibenki bila kipingamizi chochote. 

“Napenda kulihakikishia bunge lako tukufu Serikali itaendelea kulifuatilia kwa karibu suala hili ili kuhakikisha mifumo ya ATM inakuwa rafiki kwa makundi yote wakiwemo watu wenye ulemavu,” amesema Dk Kijaji.

Aidha, amebainisha kuwa changamoto ya uduni wa miundombinu kwa baadhi ya watu wenye ulemavu hususani walemavu wa miguu imetatuliwa kwa sehemu kubwa na hivyo kuwa rafiki katika maeneo mengi yanayotoa huduma za kibenki kwa kutumia mashine za ATM.