November 24, 2024

Walichokisema mashabiki wa Nicki Minaj baada ya kuachana na muziki

Rapa huyo wa muziki wa Hiphop nchini Marekani ametangaza kuacha muziki rasmi na kuhamishia nguvu zake katika kujenga na kuimarisha familia yake.

  • Ametangaza kuacha muziki rasmi na kuhamishia nguvu zake katika kujenga na kuimarisha familia yake.
  • Mashabiki wake wagawanyika kimtazamo huku wengi wakisema wameumizwa na uamuzi wake. 

Dar es Salaam. Baada ya Rapa wa kike wa muziki wa hiphop wa nchini Marekani, Nicki Minaj kutangaza kuachana na muziki,  mashabiki wake wamekuwa na maoni tofauti huku wengi wakiumia kwamba watamkosa mwanadada huyo kwenye muziki kutokana na mashairi yake kugusa maisha yao. 

Minaj ametangaza kuacha muziki rasmi na kuhamishia nguvu zake katika kujenga na kuimarisha familia yake.

Minaj ambaye jina lake halisi ni Onika Tanya Maraj ametangaza uamuzi huo jana (Septemba 6, 2019) kupitia ukurasa wake wa Twitter huku akisisitiza kuwa bado yuko kwenye tasnia ya muziki lakini atatumia muda wake mwingi zaidi kwenye familia yake na siyo muziki.

“Nimeamua kustaafu na kutengeneza familia yangu. Najua nina furaha sasa. Kwa mashabiki zangu, endeleeni kuniwakilisha, fanyeni hivyo hadi kifo changu,” ameandika Minaji kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Hata kwenye ukurasa wa Twitter sasa anajiita Mrs Petty kuonyesha dhahiri amedhamiria kujenga familia. 

Rapa huyo ambaye amegusa mioyo ya mashabiki wake na nyimbo nyingi zikiwemo “Pills and Portions”, “Only” na “Anaconda” amefanikiwa kuwa miongoni mwa marapa wa kike wanaowika zaidi duniani kwani hadi sasa, rapa huyo alikua na mshindani mmoja tu ambaye ni Cardi B.


Zinazohusiana:


Minaj mwenye umri wa miaka 36 ana wafuasi zaidi ya milioni 19 kwenye chaneli yake ya YouTube na wafuasi zaidi ya milioni 100 kwenye ukurasa wake wa Instagram na hivyo kumwacha mpinzani wake Cardi B kwa takribani wafuasi milioni 50 kwani Cardi B ana wafuasi milioni 50.6 Instagram.

Hadi sasa, minaj ana tuzo zaidi ya 150 huku akiwa ametajwa kuwania tuzo zaidi ya 400 kimataifa. 

Kuacha mziki kwa msanii huyo, huenda kukamuinua kwa kiasi fulani Cardi B na wasanii wengine wa kike wanaofanya Hiphop kwani alikuwa ni mshindani mkubwa kwao.

Japo Minaj anajulikana kwa Hiphop, msanii huyo amefanya nyimbo za mienendo ya Rnb na Pop. Hadi sasa, Minaj amefanya kazi na lebo ya Young money, Cash Money na Republic.

Minaj aliyezaliwa Desemba 8, 1982 nchi Uispani amekuwa akifanya pia na wanamuziki nguli wa Marekani kama Ariana Grande na Lil Wyne.

Japo Minaj anajulikana kwa Hiphop, msanii huyo amefanya nyimbo za mienendo ya Rnb na Pop. Hadi sasa, Minaj amefanya kazi na lebo ya Young money, Cash Money na Republic. Picha|Mtandao.

Walichokisema mashabiki wa Nicki Minaj 

Baada ya Minaj kutangaza nia yake ya kuacha muziki, mashabiki wake wamekuwa na maoni tofauti huku wengi wakiumia kwamba watamkosa mwanadada huyo kwenye muziki wake kutokana na mashairi yake kugusa maisha yao. 

Frida Amani ni msanii wa kike ambaye anafanya muziki wa Hiphop nchini Tanzania, amesema Minaj ni kati ya wanawake wenye mafanikio makubwa duniani na amechangia kuwainua wanawake wengi wanaoingia kwenye muziki. 

““Binafsi naumia na naamini muziki wake ni mkubwa na bado tunautaka muziki wake lakini kama anafanya kwa sababu ya kujenga familia basi kila la kheri kwake kwani anastahili. 

“Tunapoteza kitu kikubwa kwa sababu Nicki Minaj amefanikiwa kwa asilimia 100 kuwa kwenye ngazi moja na marapa wakubwa duniani,” amesema Frida.

Shabiki wake wa Twitter, @CALLM3CHUNLI amesema Minaj hajawahi kuwaumiza tangu aanze muziki lakini tangazo lake litawaacha na maumivu makubwa ambayo yatachukua muda kupona. 

Naye @johnPaulHit5 amesema maisha yake bila muziki wa Minaj hayana maana huku akimuomba na Mwanamuziki huyo kuendelea kuweka nyimbo zake mtandaoni ili waendelee kumfaidi. 

Hata hivyo, mashabiki wengine wamesema watu wanapaswa kuheshimu uamuzi wa Minaj kwa sababu hatma ya maisha yake iko mikononi mwake na hakuna wa kumzuia kufanya lile linalompa furaha katika maisha. 

“Hatuwezi kumlaumu ataka kuwa bora zaidi yeye na familia,” ameandika @passion92602595.