October 6, 2024

Serikali kuweka mtandaoni leseni za uchimbaji madini zilizofutwa

Imesema mpaka sasa imebaini leseni zaidi ya 18,000 zenye makosa ambazo zimeanza kufutwa kwenye mfumo wa wizara hiyo ili kutoa fursa kwa wawekezaji kuomba upya.

  • Imesema mpaka sasa imebaini leseni zaidi ya 18,000 zenye makosa ambazo zimeanza kufutwa kwenye mfumo wa wizara hiyo. 
  • Zitawekwa mtandaoni ili kutoa fursa kwa wawekezaji kuchimba madini na kuendeleza maeneo yaliyobaki wazi.
  • Watanzania washauriwa kuchangikia fursa hiyo ili kufaidika na sekta ya madini. 

Dar es Salaam. Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema wizara yake kwa kushirikiana na Tume ya Madini Tanzania wataanza kuweka mtandaoni leseni za madini zilizofutwa ili kutoa fursa kwa wawekezaji kuchimba madini na kuendeleza maeneo yaliyobaki wazi. 

Amesema mpaka sasa wamebaini leseni zaidi ya 18,000 zenye makosa ambazo zimeanza kufutwa kwenye mfumo wa wizara hiyo. 

“Ni muhimu sasa Watanzania wote wenye nia ya kuchimba madini, wachangamkie hizi fursa na baada ya muda tutaweka public (wazi) kwenye tovuti ya tume na wizara kwamba leseni gani tumefuta na ziko maeneo gani ili Watanzania wanaotaka kuchimba waweze kuziomba,” amesema Biteko.

Biteko aliyekuwa akizungumza leo (Septemba 5, 2019) nje ya Bunge na Idara ya Habari-Maelezo, amesema katika uchambuzi waliofanya wa leseni zaidi ya 33,000 wamebaini kuwa leseni zaidi ya 18,000 zina makosa na zitafutwa. 

“Lakini tutafuta kwa awamu, awamu ya kwanza tayari ambazo zimefutwa kwenye mfumo ni zaidi ya leseni 1,000 ambazo tumezifuta katika mikoa mbalimbali nchini,” amesema Biteko. 


Soma zaidi:


Amesema leseni hizo zilikuwa za watu ambao hawajawahi kuwaona na walikuwa wanawazuia wachimbaji wadogo kuchimba madini katika maeneo ambayo walikuwa wanayashikilia kinyume na sheria. 

“Sasa sehemu zile tumezifuta na tutawapatia wachimbaji wadogo,” amesema Biteko. 

Hatua hiyo itafungua fursa kwa Watanzania na wawekezaji kufaidika na sekta ya madini kwa kuomba leseni za maeneo yaliyobaki wazi ili wayaendeleze kwa kuchimba madini.  

Amesema baada ya Serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani, mpango mkubwa ulikuwa ni kuwawezesha Watanzania kuingia katika uchumi wa madini kwa kuwapatia maeneo watakayoweza kuendeleza shughuli za uchimbaji. 

Pia kuwapatia fursa mbalimbali ambazo ni masoko ya kuuza madini lakini kuwapa mitaji na kuwafanyia utafiti.