October 6, 2024

Vijana wapewa mbinu za kujikomboa kiuchumi

Baadhi ya wadau wasema mafanikio hayaangalii historia ya mtu bali bidii na ubunifu.

  • Wameshauriwa kutumia changamoto za jamii kama fursa ya kutoka kimaisha. 
  • Pia watakiwa kujifunza vitu vipya kila siku ili kujifungulia fursa za kiuchumi. 
  • Baadhi ya wadau wasema mafanikio hayaangalii historia ya mtu bali bidii na ubunifu.

Dar es Salaam. Vijana nchini Tanzania wametakiwa kuacha kulalamika juu ya ukosefu wa ajira, badala yake watumie changamoto zilizopo katika maeneo yao kama fursa ya kutengeneza miradi ya kiuchumi itakayowatoa kimaisha. 

Ushauri huo umetolewa na wazungumzaji mbalimbali katika kusanyiko la vijana la “Zijue Fursa” lililofanya jijini Dar es Salaam Agosti 31, 2019 na kuwakutanisha vijana kujadili njia mbadala za kutatua changamoto na kuinua maisha yao. 

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Coconut Foundation, Frank Mushi amesema vijana wanapaswa kutumia changamoto zinazowakabili katika jamii au sehemu zinazowazunguka kuzitatua ili wajiendeleze kiuchumi. 

“Vijana wengi siku hizi hawako creative (siyo wabunifu), lakini ukitumia changamoto zilizopo kujinyakulia fursa ni moja ya maendeleo katika ngazi ya mtu binafsi mpaka jamii,” amesema Mushi.

Amesema kukosa ubunifu na kutumia vizuri uwezo walionao wa kuleta mabadiliko katika jamii, unawakamishwa vijana wengi kufikia ndoto zao za maisha na kubaki katika umaskini wakati wote.


Zinazohusiana:


Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Nukta Africa, Nuzulack Dausen amesema vijana wanakwama katika fikra walizonazo zinazohusisha mazingira waliyokulia huku wengi wakiamini hawawezi kufanikiwa katika maisha. 

“Vijana wengi wamekwama kwa namna wanavyojiangalia na kujitathmini, wanashindwa kujichanganya, maisha ya nyumbani kwenu yasikukatishe moyo kwamba umefika,” amesema.

Lakini amewataka kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza mbele yao na zile zinazoendana na vipaji na taaluma zao.

Aidha,  Mwenyekiti wa  taasisi ya Tanzania Youth Vision Association (TYVA), Selemani Makwita amesema vijana wanapaswa kutumia nafasi wanazopata kujifunza vitu vipya vinavyoweza kuwaletea matokeo chanya katika maisha yao.

“Mimi sikuwahi kufundishwa namna ya kupambana na nilianza kujitegemea katika umri mdogo, hivyo ni vyema vijana wakatumia muda mwingi katika kujifunza ili kujiendeleza,” amesema.