November 24, 2024

Profesa Kitila awashauri Watanzania kutumia foleni ya magari Dar kusoma vitabu

Amesema foleni ya magari Jijini Dar es Salaam ni fursa ya kusoma vitabu kwa mtu akiwa kwenye gari badala ya kuperuzi mitandao ya kijamii kama WhatsApp.

  • Amesema foleni ya magari Jijini Dar es Salaam ni fursa ya kusoma vitabu kwa mtu akiwa kwenye gari badala ya kuperuzi mitandao ya kijamii kama WhatsApp. 
  • Ushauri huo umeibua mjadala kwa watumiaji wa Twitter.   

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo amewashauri Watanzania kutumia fursa ya foleni ya magari Jijini Dar es Salaam kusoma vitabu wakiwa kwenye magari badala ya kuperuzi mitandao ya kijamii kama WhatsApp. 

Prof. Mkumbo ametoa ushauri huo leo asubuhi (Agosti 27, 2019) katika ukurasa wake wa Twitter na kusema kuwa akiwa kwenye foleni ya magari wakati  anaelekea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) amefanikiwa kusoma  sura mbili za kitabu. 

“Foleni ya magari jijini Dar inaweza kudhibitisha fursa nzuri ya kusoma kitabu. Nikiwa njiani kuelekea uwanja wa ndege nilisoma sura mbili za kitabu,” ameandika Prof. Mkumbo. 

Amesema ili mtu afanikiwe kusoma kitabu itamlazimu kuzima intaneti ya simu yake ili asivutwe kuperuzi kwenye mitandao ya kijamii kama WhatsApp.

Suala la foleni kubwa ya magari hasa nyakati za asubuhi na jioni wakati watu wakitoka kwenye shughuli za uzalishaji mali limekuwa changamoto kwa wakazi wa jiji hilo linalokuwa kwa kasi Afrika.

Serikali na wadau wa maendeleo wameendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha miundombinu ya barabara ikiwemo utekelezaji wa mradi wa magari yaendayo haraka (DART) katika barabara ya Morogoro inayounganisha maeneo ya Kimara hadi Kivukoni katikati ya jiji. 

Pia Serikali imejenga daraja la juu la Mfugale katika eneo la Tazara na sasa inaendelea kujenga ‘flyover’ ya Ubungo na upanuzi wa barabara ya njia sita ya Ubungo hadi Kibaha mkoani Pwani yenye urefu wa kilomita 16. 


 Zinazohusiana: 


Hata hivyo, baadhi ya watu ambao wamechangia ujumbe wa Prof. Mkumbo wamekuwa na maoni tofauti huku wengine wakisema ni njia nzuri ya kuhimiza usomaji wa vitabu na kujipatia maarifa. 

“Thanks you @kitilam  Uwa Nasoma Ninapokosa Data Tuu Ntafanyia Kazi Njia hii. Ni offline For 45 Nitakuwa Nimepata Kitu,” amesema @Nenethefirst1 katika mtandao wa Twitter. 

Wengine wamesema  mtumishi huyo wa umma angeshauri njia mwafaka za kupunguza foleni ikizingatiwa kuwa imekuwa changamoto katika shughuli za maendeleo kwa sababu watu wengi wanatumia muda mwingi barabarani. 

“PhD imeona Traffic jam n opportunity (PHD imeona foleni ya magari ni fursa) kusoma vitabu, ila haioni kuna watu inawachelewesha kwenda mahali wanataka waende kwa haraka kwa ajili ya vipato vyao au hata emergency (dharura). Ila sishangai kila mmoja huvutia kwake. Leo yeye hana haraka,” @godmankulawa3