Jinsi ya kudhibiti matumizi mabaya ya pesa zako
Tengeneza mpango kazi unaoainisha mahitaji na matumizi ya kila pesa unazopata huku ukitumia data kufanya maamuzi ya fedha zako.
- Tengeneza mpango kazi unaoainisha mahitaji na matumizi ya kila pesa unazopata.
- Tumia data kufanya maamuzi ya fedha zako.
- Jipende mwenyewe na jikubali kwa fedha ulizonazo huku ukibuni vyanzo vipya vya mapato.
Maisha ni kutumia ulivyonavyo ili kutengeneza furaha yako binafsi. Kutumia pia kunaambatana na usimamizi mzuri wa fedha unazopata katika shughuli mbalimbali za kuajiriwa au biashara.
Kama huna usimamizi mzuri wa pesa zako mwenyewe ni rahisi kupoteza mwelekeo na kushindwa kutimiza malengo ya maisha yako.
Ufanye ni basi ili kipato unachopata kiwe sehemu ya kukuhamasisha na kukupa furaha? Jaribu kufuata dondoo hizi ambazo zinaweza kukusaidia:
Tengeneza mpango kazi
Unahitaji motisha ya kuanza kuwa na tabia njema ya matumizi ya pesa. Tengeneza mpango kazi utakaokusaidia na kukumbusha wakati ukitumia pesa zako kulingana na malengo uliyojiwekea.
Mpango wa matumizi unakuepusha kufanya tofauti ulivyopanga na ikiwezekana uweke kwenye mfumo wa kidijitali ambao utakua unakukumbusha kila unapopata pesa.
Weka malengo halisi ya fedha zako
Tumia namba, data na tarehe siyo tu maneno kuelezea nini unataka kufanikisha kwa pesa zako. Ni kiasi gani cha madeni unataka kulipa na kwa muda gani?
Ni kiasi gani cha pesa utaweka akiba na kwa muda gani na ili itumike kwa malengo gani? Nidhamu ya matumizi ya pesa ni zaidi tu ya kuongea mdomoni, tumia namba kwa sababu wanasema namba hazidanganyi.
Soma zaidi: bajeti inavyookoa matumizi mabaya ya pesa ngazi ya familia
Buni na tumia misemo ya matumizi
Wataalam wa masuala ya fedha wametengeneza misemo mbalimbali ya fedha ambayo unaweza kuitumia ili kukumbusha au kukuhamasisha namna nzuri ya kutumia pesa zako.
Unaweza kuipata mtandaoni lakini pia unaweza kubuni ya kwako na kubandika katika eneo ambalo ni rahisi kuona ili ukumbuke na kubaki kwenye mstari sahihi.
Misemo hiyo ni kama ‘kata bila senti’, ‘aliweka pesa zake ambapo mdomo wake ulipo na akapa nyingi’, ‘pesa itakuja yenyewe kama utaitengenezea mazingira’
Jipende mwenyewe
Kujipenda mwenyewe ni njia mojawapo ya kutumia pesa vizuri. Anayejipenda hatakubali kusumbuliwa na madeni. Utahakikisha pesa inayoingia unaitumia vizuri ili uendelee kupendeza na kuepuka madhara ya kiafya na hata kiakili. Kujipenda ni pamoja na kujijali yaani muonekano wako wa nje. Pesa nayo ina sehemu kubwa ya kukupendezesha, itumie vizuri.
Unahitaji motisha ya kuanza kuwa na tabia njema ya matumizi ya pesa. Tengeneza mpango kazi utakaokusaidia na kukumbusha wakati ukitumia pesa zako kulingana na malengo uliyojiwekea. Picha|Mtandao.
Ondoa mawazo hasi kuhusu fedha
Wapo baadhi ya watu katika mawazo yao hawaamini kuwa kuna siku wanaweza kupata fedha itakayowasaidia kukidhi mahitaji yao. Badilika na tengeneza mawazo chanya kila unapopata fedha.
Itakusaidia kuondokana na changamoto na kukutengenezea muamko ndani yako wa kufanya mambo makubwa huku ukibuni vyanzo vipya vya mapato.
Jifunze kukubali ulichonacho
Jikubali na pesa uliyonayo kuliko kuanza kukimbizana na kile usichonacho au kutamani vitu vilivyo nje ya uwezo wako wa sasa. Epuka kufanya matumizi yaliyo nje ya uwezo wako ili kuepuka madeni.
Kukubali ulichonacho ni njia nyingine ya kupata amani ya moyo.
Lakini uamuzi ni wako wa kutumia utakavyo kwa sababu fedha ni zako. Fedha usikufanya ukapoteza mwelekeo wa maisha!