October 6, 2024

Kampuni tatu zilizopoteza soko la hisa Dar

Ni Acacia, EABL na JHL ambazo thamani ya hisa zake zimeshuka kwa viwango tofauti.

  • Ni Acacia, EABL na JHL ambazo thamani ya hisa zake zimeshuka kwa viwango tofauti. 
  • kampuni ya Jubilee Holdings Limited (JHL) ndiyo iliyofanya vibaya zaidi baada ya thamani ya hisa zake kushuka kwa asilimia 5.49.
  • Kampuni ya uwekezaji ya NICO yaongoza kwa kuuza kiwango kikubwa cha hisa. 

Dar es Salaam. Wawekezaji wa kampuni tatu katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ikiwemo Acacia leo wamepoteza baada ya thamani ya hisa za kampuni hizo kushuka kwa viwango tofauti ikilinganishwa na ilivyokua ijumaa ya Agosti 16, 2019.

Ripoti ya soko ya siku ya DSE ya Agosti 19 inaonyesha kuwa hadi soko linafungwa jioni ya leo kampuni ya Jubilee Holdings Limited (JHL) ndiyo iliyofanya vibaya zaidi baada ya thamani ya hisa zake kushuka kwa asilimia 5.49 ambapo wawekezaji wake wamepoteza Sh450 kwa kila hisa moja. 

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa hadi soko linafungwa thamani ya hisa moja ya JHL ilikuwa ni Sh7,750 kutoka Sh8,200 iliyorekodiwa ijumaa.

Kampuni nyingine ambayo thamani ya hisa zake zimeshuka ni pamoja na Acacia ambayo imeporomoka kwa asilimia 0.74 ambapo hadi soko linafungwa hisa moja ya kampuni hiyo ilikuwa inauzwa Sh6,750 ukilinganisha na Sh6,800 ya ijumaa.  

Pia thamani za hisa za kampuni ya bia ya Afrika Mashariki (EABL) zimeshuka kiduchu kwa asilimia 0.67 ambapo wawekezaji wake wamepoteza Sh30 kwa kila hisa. 


Zinazohusiana: 


Wakati kampuni hizo tatu zikipoteza, hakuna hata kampuni moja ambayo thamani ya hisa zake imepanda katika soko hilo huku nyingi zikibaki katika viwango vilivyokuwepo Ijumaa iliyopita  zikiwemo Vodacom, na benki ya CRDB na DCB. 

Hata hivyo, kampuni ya uwekezaji ya NICO ndiyo iliyofanya vizuri zaidi leo baada ya kuongoza kwa kuuza kiwango kikubwa cha hisa. 

NICO imeuza hisa 17,200 sawa na asilimia 58.5 ya hisa zote zilizouzwa sokoni leo huku ikifuatiwa kwa mbali na benki CRDB ambayo imeuza hisa 12,000 na Soko la Hisa la Dar es Salaam hisa 133.