Kutana na hifadhi ya jamii yenye mandhari nzuri ya utalii Tanzania
Inasifika kwa wanyama mbalimbali wanaotoka katika mbuga za wanyama za Tarangire na Lake Manyara.
- Ni hifadhi ya jamii ya Randilen nayopatikana Wilaya ya Monduli , mkoani Arusha.
- Inasifika kwa wanyama mbalimbali wanaotoka katika mbuga za wanyama za Tarangire na Lake Manyara.
Dar es Salaam. Kama wewe ni miongoni mwa watu wanaopenda kutembelea mbuga mbalimbali za wanyama na kuangalia wanyama tofauti na ndege, basi hifadhi ya jamii ya Randilen inaweza kukufurahisha katika utalii wako kwa idadi ya wanyama na ndege iliyobarikiwa kuwa nayo.
Inapatikana Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha ikiwa na imezungukwa na vijiji vya Mswakini, Mswakini Juu na Naitolia.
Randilen ni miongoni mwa hifadhi tano za jamii za Ipole, Ikone, Mbonipa na Enduimet zilizopo Tanzania, enye mandhari nzuri kwa ajili ya shughuli za utalii.
Hifadhi hiyo ni maarufu kwa makazi ya wanyama mbalimbali wanaotoka katika mbuga za wanyama za Tarangire na Lake Manyara wanasogea mpaka eneo hilo lenye mandhari kubwa ya misitu.
Wanyama kama Pundamilia, Tembo, Viboko, Simba na wanyama wengine wengi pamoja na familia ya ndege mbalimbali wanaovutwa na mimea na vyanzo vya maji vinavyochangia kuwepo kwa viumbe hao kwa idadi kubwa katika eneo hilo Randilen.
Zinazohusiana
- Fahamu nyumba ya mazalia ya nyuki hifadhi ya jamii Ipole.
- Mbomipa: Fahari ya utalii nyanda za juu kusini Tanzania
Hifadhi ya Randilen ni muhimu kwa wageni kutembelea na kupata nafasi nzuri ya kufurahia maliasili mbalimbali katika eneo hilo.
Shughuli zinazoweza kufanyika kama sehemu ya uwekezaji katika eneo hilo ni pamoja na kujenga nyumba za wageni watakaokua wanatembelea eneo hilo.
Ukitaka kufika Randilen itakulazimu usafiri urefu wa kilomita 85 kutoka jiji la Arusha karibu kabisa na njiapanda ya Makuyuni ikiwa ni mwendo takribani saa moja.
Kwa wanaotaka kufanya utalii katika eneo hilo zinapatikana nyumba za wageni kama Eco Science, Tarangire Treetops, Boundary Hill, Kirurumu, Elephant na Nimali.