November 24, 2024

Kesi ya mwanahabari Erick Kabendera yapigwa kalenda

Amerudishwa rumande hadi Agosti 30, 2019 baada ya Hakimu anayesikiliza kesi yake kupata udhuru huku upande wa mashtaka ukisema bado haujakamilisha upelelezi wa kesi hiyo.

  • Alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu ya Mkazi Kisutu leo (Agosti 19, 2019) lakini kesi yake haikusikilizwa. 
  • Amerudishwa  rumande hadi Agosti 30, 2019 baada ya Hakimu anayesikiliza kesi yake kupata udhuru.
  • Upande wa mashtaka bado haujakamilisha upelelezi wa kesi hiyo.  

Dar es Salaam. Mwandishi habari za uchunguzi, Erick Kabendera anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kutakatisha pesa amerudishwa  kwa siku 12 baada ya hakimu anayesikiliza kesi yake kupata udhuru. 

Kabendera alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu ya Mkaazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo (Agosti 19, 2019) lakini kesi yake haikusikilizwa baada ya mahakama hiyo kueleza kuwa Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwezile amepata udhuru. 

Hata hivyo, upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili Wankyo Simon nao umesema haujakamilisha upelelezi na kuomba kesi hiyo ipangiwe siku nyingine wakati wakikamilisha uchunguzi. 

Kutokana na sababu hizo mbili, Kabendera amerudishwa rumande hadi Agosti 30, 2019  kabla ya kupandishwa tena kizimbani.


Soma zaidi: 


Akizungumza nje ya Mahakama, Wakili wa Kabendera, Jebra Kambole amesema hawana tatizo na hakimu kupata udhuru lakini wanauomba upande wa jamhuri kukamilisha upelelezi kwa wakati ili kesi iendelee kwa sababu mashtaka yanayomkabili mteja wake hayana dhamana. 

Mashtaka yanayomkabili mwanahabari huyo ni kuongoza kundi la uhalifu kwa lengo la kupata faida au manufaa mengine, kutokulipa kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya zaidi ya Sh173.24 milioni na utakatishaji wa fedha kiasi cha  zaidi ya Sh173.24 milioni.

Kabendera, ambaye anaandikia  vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi alichukuliwa kwa nguvu nyumbani kwake Mbweni Jijini Dar es Salaam Julai 29, 2019 na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi na tangu wakati huo amekuwa akishikiliwa na polisi.