November 24, 2024

Tanzania kupiga mnada asilimia 10 ya mamba kuokoa maisha ya raia

Ni hatua ya kukabiliana na ongezeko la wanyama wakali na wanaovamia maeneo ya watu na kufanya uharibifu ikiwemo kusababisha vifo.

  • Ni hatua ya kukabiliana na ongezeko la wanyama wakali na wanaovamia maeneo ya watu na kufanya uharibifu ikiwemo kusababisha vifo. 
  • Pia unaanzishwa mradi wa kuweka uzio kwenye maeneo yenye historia ya matukio ya mamba kudhuru watu.
  • Mauzo ya wanyama hao yatafanyika kwa njia ya mnada kuanzia wiki ijayo.

Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema Serikali inauza asilimia 10 ya mambo wote nchini ikiwa ni hatua ya kukabiliana na ongezeko la wanyama wakali na wanaovamia maeneo ya watu na kufanya uharibifu ikiwemo kusababisha vifo. 

Dk Kigwangalla ametoa taarifa hiyo leo (Agosti 17, 2019) katika ukurasa wake wa Twitter, amesema pamoja na kuamua kuuza asilimia 10 ya mamba wote nchini, pia unaanzishwa mradi wa kuweka uzio kwenye maeneo yenye historia ya matukio ya mamba kudhuru watu, kama Maleza mkoani Mbeya na Ruvu (Pwani)

“Uhifadhi na ulinzi wa maliasili nchini umeimarika na tumepata mafanikio makubwa sana. Ujangili tumeudhibiti kwa mafanikio makubwa sana. Changamoto mpya imezaliwa, wanyama wakali/waharibifu wamezidi na wanavamia maeneo ya watu. Tumeamua kuuza asilimia 10 ya mamba wote nchini,” amesema Waziri huyo. 

Amewataka wananchi wasifanye mauaji ya wanyama kulipiza kisasi wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo na kuepukana na tabia hatarishi.

Uaamuzi ya kupiga mnada maliasili hizo ili kupunguza migogoro kati ya wanadamu na wanyamapori, amesema umekuja baada ya kukamilika kwa utafiti nilioafanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI). 


Soma zaidi: Tanzania yaangalia uwezekano wa kuwavuna mambo kuokoa maisha ya raia


Mauzo ya wanyama hao yatafanyika kwa njia ya mnada kwa utaratibu ambao utatangazwa wiki ijayo. 

Aidha, Kigwangalla ambaye ni Mbunge wa Nzega Vijijini amesema watauza viboko wote waliopo kwenye maeneo yenye maji kama maziwa, mabwawa na mito iliyopo mjini, kama vile pale Mpanda mkoani Katavi, Mafia (Pwani) na Babati (Manyara).

“Sambamba na maamuzi haya, tunaanzisha vituo vya kudumu vya ulinzi kwenye maeneo yote korofi, ambapo wanyama wakali/waharibifu kama tembo na simba wamekuwa wakileta shida kwa wananchi. Tutaendelea pia kufundisha wananchi namna ya kujisalimisha kama wakikutana na wanyamapori,” amesema Kigwangalla. 

Kwa mujibu wa taasisi ya Crocodiles of the World ya nchini Uingereza, imeeleza kuwa katika bara la Afrika pekee kuna mamba kati ya 250,000 hadi 500,000.