October 6, 2024

CITES ilivyojipanga kukomesha biashara ya viumbe vilivyo hatarini kutoweka duniani

Mkataba huo wa kimataifa wa viumbe vilivyo hatarini kutoweka (CITES) unakusudia kupitisha mapendekezo yenye lengo la kubadili na hatimaye kuimarisha kanuni za kulinda viumbe vya porini.

  • Inakusudia kupitisha mapendekezo yenye lengo la kubadili na hatimaye kuimarisha kanuni za kulinda viumbe vya porini.
  • Wawakilishi wa nchi 183 wanachama wa mkataba wa kimataifa wa viumbe vilivyo hatarini kutoweka (CITES) watajadili mapendekezo hayo leo Uswisi. 
  • Wajumbe pia wataamua iwapo ala za muziki zitengenezwazo kwa miti ya thamani zitolewe kwenye udhibiti.

Wawakilishi wa nchi 183 wanachama wa mkataba wa kimataifa wa viumbe vilivyo hatarini kutoweka (CITES) wanaanza mkutano wao wa siku 11 hii leo huko Geneva, Uswisi kwa lengo la kujadili na kuimarisha mikakati ya kulinda viumbe hao.

Baadhi ya viumbe ambao wako hatarini kutoweka ambao hata Tanzania imekuwa ikipambana kuwalinda ni pamoja na ndovu, twiga, kakakuona na punda. 

Taarifa ya Umoja wa Mataifa (UN) iliyotolewa leo (Agosti 17, 2019) imeeleza kuwa tayari nchi hizo wanachama zimewasilisha mapendekezo 56 yenye lengo la kubadili na hatimaye kuimarisha kanuni za kulinda viumbe vya porini wakiwemo wanyama pamoja na maua, ambavyo vinauzwa kwenye soko la kimataifa.

“Mapendekezo mengi yanalenga kuhakikisha kuwa viumbe hivyo vilivyoko hatarini na ambavyo vinaendelea kuuzwa, vinasalia endelevu na hivyo mapendekezo yanataka vibali kutoka CITES ili kuruhusu biashara yao,” amesema Katibu Mkuu wa CITES, Ivonne Higuero katika taarifa hiyo. 

Amesema mapendekezo mengine yanataka kupigwa marufuku kwa biashara za viumbe vilivyoko kwenye orodha ya I ambapo mengine yanataka kuwa viumbe ambavyo tayari idadi yao imekaa sawa vihamishwe kutoka orodha ya I kwenda orodha ya II ya mkataba wa CITES.

“CITES inaweka kanuni za biashara ya kimataifa kwa mimea na wanyama. Ni mbinu nzuri ambayo inalenga kuhakikisha uwepo endelevu wa viumbe hivyo na kukabiliana na upotevu wa bayonuai,” amesema Katibu Mkuu huyo.


Soma zaidi:


Amebainisha kuwa kanuni zilizo wazi na zinazotekelezeka kwa kuzingatia sera thabiti ni muhimu katika kulinda utajiri wa asili na kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ambayo yalipitishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 2015.

Ripoti iliyotolewa Mei mwaka huu na jopo la kiserikali la masuala la sayansi na bayonuai (IPBES) ilieleza kuwa takribani aina milioni moja ya viumbe viko hatarini kutoweka ndani ya miongo kadhaa ijayo kutokana na  kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo matumizi kupita kiasi , uwindaji na uvuvi haramu na ukataji magogo.

Wajumbe pia wataamua iwapo ala za muziki zitengenwazo kwa miti ya thamani zitolewe kwenye udhibiti kwa mujibu wa CITES.

Baadhi ya viumbe ambao wako hatarini kutoweka ambao hata Tanzania imekuwa ikipambana kuwalinda ni pamoja na ndovu, twiga, kakakuona na punda. Picha|Mtandao. 

Wanyama na mimea iliyo hatarini kutoweka

Kwa mujibu wa UN, miongoni mwa wanyama wanaopendekezwa kuwa wahamishiwe kutoka orodha ya II hadi ya I ili udhibiti uwe wa juu zaidi ni kakakuona ambaye magamba yake yenye kemikali ya Keratini hutumika kutengeneza dawa za kienyeji za kichina.

Mwingine ni Markhor, ambaye ni aina ya mbuzi wa kienyeji kutoka eneo la Asia ya Kati ambapo nchi ya Tajikistan inataka mnyama huyu ahamishwe kutoka orodha ya I iliyowekwa mwaka 1975 na kuwekwa orodha ya II kwa kuwa idadi yao imeongezeka.

Afrika Kusini inapendekeza mmea aina ya Bitter Aloe unaotumika kwenye dawa na ambao sasa uko kwenye orodha ya II, usiguswe na CITES kwa maelezo kuwa mbegu yake inasaidia kukuza vipato.

Nayo Kenya, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Mali, Niger na Senegal zinapendekeza twiga ajumuishwe kwenye orodha ya II kwa kuwa idadi yao inapungua sana