October 6, 2024

Rais Ramaphosa aahidi kuliboresha eneo la wapigania uhuru Morogoro

Eneo hilo la Mzambu lipo Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), mkoani Morogoro waliishi wapigania uhuru wa Afrika Kusini.

  • Eneo hilo la Mzambu lipo Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), mkoani Morogoro ili liwe la kisasa. 
  • Eneo hilo waliishi wapigania uhuru wa Afrika Kusini. 
  • Pia itajengwa shule na kutoa fursa kwa walimu wa nchi hizo mbili kubadilishana uzoefu. 

Dar es Salaam. Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema watashirikiana na Serikali ya Tanzania kuliboresha eneo Mzambu lilipo Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), mkoani Morogoro ili liwe la kisasa ikizingatiwa kuwa limebeba historia kubwa ya ukombozi wa nchi za Afrika. 

Kiongozi huyo ambaye kwa mara ya kwanza amefika mkoani Morogoro leo ametembelea eneo hilo ili kujionea sehemu ambazo waliishi wapigania uhuru wa nchi yake wakati wakipanga mikakati ya kukomesha utawala wa wakoloni. 

Rais Ramaphosa alikua akizungumza leo (Agosti 16, 2019) alipofanya ziara katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), kampasi ya Mazimbu Morogoro, amesema Tanzania . 

Amesema anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa mchango mkubwa ulioutoa kwa nchi ya Afrika Kusini wakati wa harakati za kupigania uhuru wa nchi hiyo, hivyo wataendelea kuimarisha ushirikiano.

Amebainisha kuwa watashirikiana na Tanzania kuliboresha eneo la Mazimbu ili liwe la kisasa na wanakusudia kujenga shule kwa ajili ya kumbukumbu itakayodumu kwa muda mrefu ujao.

“Tutaboresha na shule katika eneo hili na kuweka utaratibu wa walimu wake kutembeleana na wa Afrika Kusini kwa ajili ya kubadilishana uzoefu,” amesema Rais huyo. 


Soma zaidi:


Katika hatua nyingine, amesema nchi yake iko tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha masuala mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo kubadilishana uzoefu katika ukuzaji wa teknolojia.

Rais Ramaphosa aliwasili katika uwanja wa ndege wa Morogoro saa 4.21 asubuhi na kupokelewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kujionea maeneo ambayo wapigania uhuru wa Afrika Kusini walikuwa wakikutana na kupanga mipango mbalimbali.

Akizungumzia kuhusu eneo la Mazimbu, Majaliwa amesema kuwa lina uhusiano mkubwa na historia ya nchi hizo mbili kwa sababu huwezi kuulezea vizuri uhusiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini pasi na kulitaja eneo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, eneo la Mazimbu limebeba historia muhimu ya kumbukumbu ya vuguvugu la ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika pamoja na mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

“Mheshimiwa Rais, Tanzania ikishirikiana na nchi tano zilizokuwa katika kundi la mstari wa mbele (Angola, Tanzania, Zambia, Botswana na Msumbiji) ilijishughulisha sana katika ukombozi kusini mwa Afrika na katika kukomesha sera za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini,” amesema Majaliwa.  

  Rais wa Afrika Kusini, Cyril Matamela Ramaphosa, akiangalia moja ya kaburi la Wapigania Uhuru wa Afrika Kusini, katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Mazimbu Campus mjini Morogoro. Agosti 16.2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.                                             

Sera za ubaguzi wa rangi zilikoma Februari 1994 na kufuatiwa na uchaguzi huru na wa haki uliopelekea kupatikana kwa Rais wa kwanza mzalendo wa nchi hiyo, Hayati Mzee Nelson Mandela mwezi Mei 1994.

“Tunapoongelea kukoma kwa sera za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, siku zote tutawakumbuka Hayati Baba wa Taifa Mwal. Julius Nyerere na Hayati Mzee Nelson Mandela kwa utumishi wao uliotukuka kwa kujenga misingi imara ya umoja katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini,” amesema Majaliwa. 

Waziri Mkuu amesema namna pekee ya kuwaenzi viongozi wetu hao ni kuendelea kujenga umoja na kushirikiana katika kuimarisha Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa ajili ya maslahi ya wananchi.

Ramaphosa aliondoka uwanja wa ndege wa Morogoro saa 1:59 na kurejea  jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kushiriki mkutano wa wakuu wa nchi za SADC kesho.