November 24, 2024

Filamu za kimataifa zitakazoingia sokoni mwishoni mwa 2019

Miongoni mwa filamu hizo ni pamoja na “Cats” iliyosheheni mastaa wengi wa filamu kama Taylor swift, Jennifer Hudson na Idris Elba.

  • Miongoni mwa filamu hizo ni pamoja na “Cats” iliyosheheni mastaa wengi wa filamu akiwemo Taylor swift, Jennifer Hudson na Idris Elba. 
  • Filamu za “Jumanji” na “Frozen” nazo zitakuwa sehemu ya kufunga mwaka. 
  • Staa wa filamu Marekani, Will Smith kwa mara nyingine tena atakuwepo katika filamu ya Gemini Man.

Dar es Salaam. Filamu ni burudani lakini ni sehemu ya kujifunza na kufahamu dunia na tamaduni za watu zinavyoendeshwa. Filamu ni maisha yanayojieleza kwa namna tofauti tofauti. 

Wiki iliyopita tulikuletea orodha ya filamu nne ikiwemo ya Fast and Furious (Hobbs and Shaw) ambazo zinaendelea kuonyeshwa katika kumbi mbalimbali za Sinema Tanzania. Lakini unahitaji kufahamu mengi zaidi ya filamu hizo. 

Leo tunakuletea orodha ya filamu kali ambazo ziko mbioni kutolewa kabla ya mwaka huu wa 2019 kuisha. Kama wewe ni mpenzi wa filamu basi kaa mkao wa kula ili usipitwe na filamu hata moja itakayoingia sokoni.

1. Jumanji The Next level 

Kikundi cha marafiki kinaamua kurudi kwenye mchezo wa Jumanji ili kumuokoa rafiki yao. Hata hivyo, kinachowakuta mbeleni ni tofauti na mazingira waliyoyazoea. 

Milima, barafu na jangwa ni kijiko kimoja tu cha asali kutoka kwenye mtungi mzima. Je Dwayne Johnson (Dr. Bravestone), Kevin Hart ( Franklin), Karen Gillan (Martha) na marafiki wengine watafanikiwa kumuokoa rafiki yao?

Filamu hii yenye vionjo vya aina yake imesimamiwa na kuongozwa na  Jake Kasdan ambaye ni kinara nyuma ya filamu zilizofanya vizuri kama Bad teacher iliyotoka mwaka 2011,  The Dewey Cox Story (2007), Zero Effect (1998), The TV Set (2006) na Jumanji Welcome to the Jungle (2017). Kaa tayari kuupokea mkasa huu ifikapo Desemba 12 mwaka huu.

Jumanji ni kati ya filamu zenye masimulizi ya kusadikika. Picha|Mtandao.

2. Gemini Man

Baada ya Muigiza filamu wa Marekani, Will Smith kuhusika kwenye filamu ya “Alladin (2019)” pamoja na filamu ya katuni ya “Spies in Disguise(2019)”, anaigiza kama Henry Brogan ambaye ni muuaji anayegeuka kuwa “target” ya muuaji ambaye ni mdogo zaidi na mwenye kasi ambaye kwake (Henry). 

Henry ambaye ameigiza filamu takribani 50, unapatwa na mshangao pale anapogundua kuwa muuaji  ni  mtu anayefanana naye wakati akiwa mdogo. 

Fuatilia mkasa huu ulioongozwa na Ang Lee anayeshikilia tuzo zaidi ya 30 za uongozaji filamu ambaye pia ni kichwa nyuma ya filamu kama Hulk ya mwaka 2003 na Crouching Tiger (2000) utakaoweza kuuona katika  kumbi za sinema ifikapo Disemba 12 mwaka huu.


Zinazohusiana:


3. Frozen II

Elsa ambaye ni Malia wa theluji anaambatana na dada yake Anna kwenye safari ya mbali zaidi na ufalme wao. Wakisindikizwa na marafiki zao, yaani Olaf, Kristoff na Sven laki ni wataweza kukabiriana na  vizingiti na ubaya wote unaotawala nje ya ufalme wao?

Ikiwa chini ya Jenifer Lee na Chris Buck ambao wamehusika katika utengenezaji wa filamu za “A Wrinkle in Time” na “Wreck it Ralph”, filamu hiyo mpya italeta wimbo gani utakaopindua  wimbo wa “Let it Go” uliotumika kwenye filamu ya Frozen sehemu ya kwanza ambao ndani ya miaka mitano umetazamwa na watu zaidi ya bilioni 1.7 kwenye mtandao wa YouTube? 

Filamu hii ya aina yake inatarajiwa kuingia sokoni ifikapo Novemba mwaka huu.  

4. Cats

Kama wewe ni mpenzi wa filamu za muziki au muziki wenyewe, basi hii ni kwa ajili yako. 

Kutana na mastaa wa filamu kama Taylor swift, Jennifer Hudson, Idris Elba, James Corden, Rebel Wilson, Jason Derullo, Judi Dench, Francesca Hayward na wengine wengi kwenye filamu itakayokuweka wazi  kisa kinachoikuta familia ya paka.

Filamu hii iko chini ya nguli Tom Hooper mshindi wa tuzo ya Academy ya Muungozaji Bora wa filamu mwaka 2011 ambaye pia ameongoza filamu ya “The King’s Speech” (2010) na “The Danish Girl” (2015).

Idriss Elba, Taylor swift na waigizaji wengine wanaoshiriki filamu ya “Cats” 2019.tandao Picha|Mtandao.

5. Star Wars, The rise of Skywalker

Filamu hii a,mbayo iko chini ya  ya Jeffrey Abrams ambaye ni kiongozi wa filamu ya “Mission Impossible” na “Overload” za mwaka 2018.

Star Wars ni mfululizo wa filamu tatu ambazo zinaelezea hadithi isiyo halisi. Kutana na Daisy Ridley, Carrie Fisher, Mark Hamill na John Boyega kujua kama kuna mwisho wa mapambano pale Rey, Fin na Poe walio na nguvu na maarifa kutoka vizazi vya zamani.

Adam Driver (Kylo Ren) ni kiongozi wa juu, Born Ben Solo ni mtoto wa  Leia Organa na Han Solo ni binamu yake na Luke Skywalker na mjukuu wa Darth Vader.  Mkasa huu utakufikia katika eneo lako ifikapo Desemba 18, 2019.

Hakika mwaka 2019 utakua wa burudani zaidi kwako, ikizingatiwa kuwa filamu zote zitaingia sokoni mwishoni mwa mwaka wakati watu wengi wakiwa katika mapumziko.

Endelea kufuatilia www.nukta.co.tz kufahamu kwa undani soko la filamu duniani na jinsi linavyobadilisha maisha ya watu katika maeneo mbalimbali.