October 6, 2024

Wakuu wa nchi SADC walivyoshikilia fursa za Kiswahili

Wanasubiriwa kutoa uamuzi kama lugha ya Kiswahili inaweza kutumika kama lugha rasmi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

  • Wanasubiriwa kutoa uamuzi kama lugha ya Kiswahili inaweza kutumika kama lugha rasmi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
  • Kama kitaidhinishwa basi kitaifungulia Tanzania fursa mbalimbali kama utengamano wa kibiashara, ajira na ukuaji wa sekta ya mawasiliano.
  • Pia kitawaongezea viongozi ujasiri wa kushiriki katika majadiliano na majukwaa ya kimataifa. 
  • Vyombo vya kuendeleza lugha hiyo vyapewa changamoto ya kukukiza zaidi. 

Dar es Salaam. Kufuatia lugha ya Kiswahili kupendekezwa kuwa lugha rasmi ya nne itakayotumiwa katika shughuli za mawasiliano za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wadau wamesema hatua hiyo ni fursa muhimu kwa Tanzania kufaidika na utengamano wa kibiashara na kuwaongezea viongozi wake ujasiri katika majukwaa ya kimataifa. 

Jana (Agosti 14, 2019) Baraza la Mawaziri la SADC lilipendekeza Kiswahili kuwa lugha ya nne ambapo pendekezo hilo litafikishwa ili kutolewa uamuzi katika mkutano wa Wakuu wa nchi 16 za SADC utakaofanyika Agosti 17 na 18 mwaka huu jijini Dar es Salaam. 

Iwapo kitapitishwa mwishoni mwa wiki hii na Wakuu wa nchi za SADC, Kiswahili kitaungana na lugha za Kifaransa, Kiengereza na Kireno zinazotumika katika shughuli rasmi za jumuiya hiyo. 

Huenda hatua hiyo akakifanya Kiswahili ambacho ni lugha ya Taifa kuzidi kutanua wigo wa wazungumzaji na matumizi yake duniani, ikizingatiwa kuwa kinatumiwa na jumuiya mbalimbali za kimataifa ikiwemo Umoja wa Afrika (AU) katika shughuli zake. 

Mwishoni mwa mwaka 2018, Afrika Kusini ilitangaza kuanza kufundisha lugha hiyo katika shule zake na mwaka huu imeingia makubaliano na Tanzania ili kuwapeleka walimu watakaofundisha Kiswahili katika nchi hiyo. 

Lakini Namibia nayo imeonyesha nia ya kukichangamkia Kiswahili ambapo wakati wa ziara ya Rais John Magufuli nchini humo Mei, 2019 alipokutana na mwenyeji wake, Rais Dk Hage Geingob walijadili namna ya itakayosaidia lugha hiyo kufundishwa katika nchini hiyo. 

Wachambuzi wa masuala ya mawasiliano na lugha wameiambia www.nukta.co.tz kuwa kama Kiswahili kitaridhiwa kuwa lugha rasmi ya SADC kitaweza kufungua fursa mbalimbali ambazo Tanzania bado haijazifikia katika nchi za Kusini mwa Afrika. 

Mhadhiri wa Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Faraja Lugome ameiambia www.nukta.co.tz kuwa Kiswahili kitawaongezea ujasiri viongozi wa Tanzania kuwa huru kushiriki katika mijadala na majukwaa ya kimataifa kwa sababu wataweza kuwasilisha mawazo yao kwa lugha wanayoimudu kwa ufasaha. 

“Kikwazo kitaondoka hasa kwa wale wanaokionea aibu Kiswahili hasa katika mikutano ya kimataifa kwa sababu watafikiri kwa Kiswahili na kuongea Kiswahili,” amesema Lugome. 


 Soma zaidi:


Mhadhiri huyo ambaye ni miongoni mwa watu wanaoshiriki mkutano wa SADC mwaka huu, amesema itawarahisishia pia Watanzania kuyafikia masoko ya bidhaa na huduma katika nchi za SADC kwa kutumia mawasiliano ya lugha ya Kiswahili.

Pia itakuwa ni fursa kwa wananchi wa nchi zingine kujifunza Kiswahili ili kuhakikisha wanaendana na mahitaji ya wazungumzaji wa Tanzania katika kubadilishana uzoefu na mawazo mbalimbali ya maendeleo. 

Lugome amesema Kiswahili kitaimarisha mtengamano wa kibiashara katika nchi za SADC na kuzifanya zifaidike zaidi katika kuuziana bidhaa na huduma kupitia biashara ya mipakani na hata kukuza diplomasia ya nchi hizo kwa lugha anayoeleweka kwa pande zote. 

“Hiyo ni fursa ya kukuza na kupanuka kwa Kiswahili katika mataifa mbalimbali, jambo linaloweza kuchangia katika utengamano wa kibiashara na kuinua mifumo ya elimu katika jamii zetu,” amesema Mhadhiri huyo. 

Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 150 hutumia Kiswahili kwa ajili ya mawasiliano Afrika Mashariki na Kati ikiwemo lugha ya kwanza huku mataifa mengine wanakitumia Kiswahili kama lugha ya pili au ya tatu.

Mwanzilishi wa tovuti ya Daily Life Talk, Jane Susha naye ameiambia www.nukta.co.tz  kuwa itawasaidia zaidi Watanzania wafanyabiashara hasa ambao wana changamoto ya kuzungumza lugha za kimataifa kama Kiengereza kuongeza mawanda ya kufanya biashara za mipakani na nchi za SADC kwa kutumia lugha wanayoimudu. 

“Nafikiri inaweza kusaidia kwa kiasi fulani, nikimaanisha kwamba kama Watanzania wengi Kiingereza ni tatizo basi Kiswahili kikitumika inaweza kuwa mkombozi wao hasa katika kufanya biashara baina ya mataifa haya,” amesema Susha.

Jopo la Wakuu wa nchi walioshirika mkutano wa SADC mwaka jana nchini Namibia. Picha|Mtandao. 

Lakini bado kuna kazi ya kufanya

Susha ambaye ni mtaalamu wa mawasiliano na tafiti za jamii, anasema Tanzania kufaidika na fursa hizo kutategemea utayari na utashi wa nchi za SADC kutekeleza pendekezo hilo la matumizi ya Kiswahili linalosubiriwa kutolewa uamuzi na Wakuu wa nchi za jumuiya hiyo.  

“Kikubwa ambacho watu tunahitaji kufahamu ni kwamba lugha ya Kiswahili inakuwa hivyo fursa nyingi pia zinaongezeka,” amesema Susha. 

Kwa upande wake, Lugome anasema ni wakati sasa kwa taasisi zinazosimamia maendeleo ya lugha ya Kiswahili likiwemo Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) kuhakikisha kunakua na matumizi sahihi na fasaha ya lugha hiyo katika maeneo mbalimbali ya shughuli za mawasiliano.

Mkutano wa Wakuu wa nchi 16 za SADC ambazo zina watu zaidi ya milioni 300 utakaofanyika mwishoni mwa wiki, ulitanguliwa na Wiki ya Viwanda ya SADC ambayo pia imetoa fursa mbalimbali za utalii, biashara kwa Watanzania.