November 24, 2024

Tanzania yapewa jukumu la kuongoza kamati ya hali ya hewa SADC

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk Agnes Kijazi ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo.

  • Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk Agnes Kijazi ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo. 
  • Ataongoza kamati hiyo kwa kipindi cha miaka miwili. 

Dar es Salaam. Tanzania amekabidhiwa uenyekiti wa kamati ndogo ya sekta ya hali ya hewa ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kipindi cha miaka miwili, jambo linalofungua fursa za kufaidika zaidi na huduma za hali ya hewa katika jumuiya hiyo.  

Makabidhiano hayo yamefanyika katika mkutano wa kamati hiyo (SADC-SCOM) jijini Windhoek, Namibia Agosti 13, 2019 ambapo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk Agnes Kijazi ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA, Dk Kijazi amepita bila kupingwa na atashikilia nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka huu wa  2019.

Dk Kijazi anachukua nafasi ya Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Hali ya Hewa ya Namibia, Franz Uirab ambaye ameiongoza kamati hiyo kwa miaka miwili. 

Sambamba na makabidhiano hayo, mkutano huo umejadili masuala mbalimbali ya uendelezaji wa sekta ya hali ya hewa katika eneo la SADC pamoja na kupitia hatua za utekelezaji wa maamuzi ya mkutano wa Mawaziri uliopita na kutoa mapendekezo yatakayjadiliwa Septemba, 2019 Jijini Dar es Salaam.