October 7, 2024

Sekretalieti SADC yajipanga kuimarisha biashara ya mazao Tanzania

Inakusudia kuimarisha utekelezaji wa sera za maendeleo hasa katika ukuzaji wa biashara ya mazao ya kilimo na mifugo kwa kutoa wataalam na ushauri ili kuwafaidisha wakulima.

  • Ni sekretalieti ya Chakula, Kilimo na Malisili ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini Mwa Afrika (SADC).
  • Inakusudia kuimarisha utekelezaji wa sera za maendeleo hasa katika ukuzaji wa biashara ya mazao ya kilimo na mifugo.
  • Pia itatoa wataalam na ushauri wa biashara ya mazao ili kuwanufaisha wakulima wa kanda hiyo. 

Dar es Salaam. Sekretalieti ya Chakula, Kilimo na Malisili ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini Mwa Afrika (SADC) imesema itaendelea kufanya kazi karibu na wananchi walioko kwenye ukanda wa Jumuiya hiyo ikiwemo Tanzania ili kuimarisha utekelezaji wa sera za maendeleo hasa katika ukuzaji wa biashara ya mazao ya kilimo na mifugo. 

Kwa sasa SADC inatekeleza Sera ya Maendeleo ya 2015-2020 SADC ambayo inagusa zaidi sekta ya biashara ya mazao mbalimbali ya kilimo na mifugo.

Mkurugenzi wa Chakula, Kilimo na Maliasili, Domingos Dove amesema ni vyema kuhusisha vyombo vya habari katika sekta hiyo ili kutoa habari zilizohakikiwa, kuona changamoto wanazokumbana nazo wakulima, mafanikio  ili kila mmoja ajue sekritarieti inakoenda katika kuimarisha biashara na soko la SADC kwenye mazao ya kilimo na mifugo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam jana, amesema kuwa sekretarieti hiyo ina dhamira kubwa ya kutoa wataalam kutekeleza sera za maendeleo endelevu za ukanda huo wa Afrika ili kuinua maisha ya wananchi. 

“Kama Sekritarieti ya SADC tunafanya kazi kubwa kimkakati kwenye nchi wanachama na tuna matarajio makubwa ya kuona na kugusa sehemu zote kuanzia ngazi ya Taifa mpaka ngazi ya kanda na kazi hii inahakikisha kwamba sera zote kwenye nchi 16 za Jumuiya hii zinaunganishwa  ili kuwezesha kufanya kazi pamoja, hii ndiyo kazi yetu”, amesema, Gove. 


Soma zaidi: Maagizo matano ya Magufuli kukuza uchumi wa viwanda nchi za SADC


Amesema kuwa malengo ya sekritarieti hiyo kwa nchi wanachama ni kutangaza na kuwezesha uunganishwaji wa Sera  na miradi mbalimbali ya maendeleo miongozi mwa nchi 16 wanachama wa SADC.

Aidha,katika kutekeleza sera ya maendeleo SADC, Sekritarieti hiyo inafanya kazi katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuimarisha kilimo na uzalishaji wa mazao ya chakula, kuimarisha eneo la kutangaza biashara na kuwaunganisha wananchi kwenye nchi 16 za SADC ili kuweza kupata soko la watu zaidi ya milioni 300.

“Tunatakiwa kuwa na uwezo wa kutangaza na kuwahamasisha wananchi katika nchi wanachama wa SADC kuzalisha na kuchangamkia soko la zaidi ya watu milioni 300 na hii ndiyo kazi yetu kama Sekritarieti.

“Tutazidi kutangaza, kuboresha na kuhamasisha biashara miongoni mwa nchi wanachama kwenye mazao ya kilimo na mifugo, kwa  hiyo wananchi wanatakiwa kuzalisha  kulingana na soko la SADC litakavyokuwa,” amesema Gove. 

Mkurugenzi wa Chakula, Kilimo na Maliasili kutoka Sekritarieti ya SADC, Damingos Dove akifafanua Jambo kwa Waandishi wa Habari (Hawapo pichani) Kuhusu malengo ya Sekritarieti hiyo katika mkutano na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam. Picha|Habari Maelezo.

Katika hatua nyingine, Gove amesema kuwa Sekritarieti hiyo ina jukumu kubwa la kulinda maliasili zilizoko ukanda huo wa afrika na alitolea mfano kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika ulinzi wa maliasili ikiwemo wanyama pori.

“Tunajivunia kuwa Serengeti na Kilimanjaro zipo kwenye Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini Mwa Afrika (SADC) na zinawavutia watu wengi kutoka nchi mbalimbali duniani, tunafurahi kuona Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizofanikiwa  kwa kiasi kikubwa kwenye ulinzi wa Maliasili ikiwemo mbuga za wanyama Serengeti na Ruaha,” amesema Gove.