October 7, 2024

Tume yaanza kuchunguza chanzo cha mlipuko wa lori la mafuta Morogoro

Tume hiyo maalum iko kwa ajili ya kubaini chanzo cha ajali ya moto iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 69 na wengine 70 kujeruhiwa.

  • Tume hiyo maalum iko kwa ajili ya kubaini chanzo cha ajali ya moto iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 69 na wengine 70 kujeruhiwa.
  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema lazima wajiridhishe kama Serikali ilitekeleza vizuri jukumu lake. 
  • Vyombo vya habari vyaonywa kutoa takwimu zisizo sahihi.

Dar es Salaam. Serikali imeunda tume maalum kwa ajili ya kubaini chanzo cha ajali ya moto iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 69 na wengine 70 kujeruhiwa wakati lori la mafuta lililopinduka na kulipuka katika eneo Msamvu mkoani Morogoro juzi. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameunda tume hiyo jana (Agosti 11, 2019), wakati akizungumza na waombolezaji waliofika katika hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kutambua miili ya ndugu zao. 

“Hii tume inaanza kazi leo (Agosti 11, 2019), hadi ijumaa inipe taarifa yake na hata kama mimi sijawajibika initaje,” amesema Majaliwa aliyemwakilisha Rais John Magufuli kuwafariji wafiwa katika msiba huo ambao umeligusa Taifa.  

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, amesema lazima wajiridhishe kama Serikali ilitekeleza vizuri jukumu lake kwa sababu ajali ilitokea saa mbili asubuhi katikati ya mji, hivyo wanataka kujua ajali ilipotokea kila mmoja alitumiza jukumu lake.

“Najua pale ajali inapotokea trafiki wanawahi haraka hata kama kwa gari la kukodi. Watu walikuja na madumu, wengine kuchomoa betri nani aliwazuia. Je lilipoanza kuungua gari la zima moto lilikuja kwa wakati gani,” amehoji Majaliwa na kuongeza kuwa,

“Kuna vitu vingi lazima tuviangalie tujue nani hakutimiza majukumu yake. Nadhani ujumbe mnaupata si vyema tutakimbilia vitu badala ya watu. Tunasikitika sana kwa yaliyotukuta hata upande wa Serikali tunasikitika kuwapoteza Watanzania.”


Soma zaidi: Zaidi ya watu 57 wafariki dunia baada ya lori la mafuta kuwaka moto Morogoro


Pia, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu jitihada za kuokoa waliopata majeraha kwamba zinaendelea vizuri na jukumu lao kubwa kuwaombea marehemu wapumzike kwa amani na pia wawaombee wajeruhi waweze kupona.

Aidha, Rais Magufuli tayari ameshatoa kibali cha kutolewa fedha kwa ajili ya kununuliwa vifaa tiba na dawa zinazohitajika ili kufanikisha matibabu ya majeruhi wote waliolazwa hospitalini. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika ibada ya kuwaombea marehemu waliofariki katika ajali ya moto wa lori la mafuta lililoanguka katika eneo la Msamvu mjini Morogoro. Ibada hiyo ilifanyika  kwenye viwanja vya hospitali ya mkoa wa Morogoro, Agosti 11, 2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.

Vyombo vya habari vyaonywa

Akizungumzia kuhusu idadi ya vifo na majeruhi waliotokana na ajali hiyo ambayo inatangazwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari, Waziri Mkuu amesema ni vema takwimu hizo wakaacha zikatolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe.

“Kwenye vyombo vya habari tuelewane kwenye takwimu za vifo na majeruhi. Msiseme suala la takwimu anayetoa ni Mkuu wa Mkoa na matukio haya yapo chini yake. 

Nimeamua kusema hivi hizi takwimu zikitajwa nyinginyingi mnajenga hofu na taharuki kwa wananchi. Hili halikubaliki mkitaka taarifa mtafuteni Mkuu wa Mkoa,” amesema Majaliwa.

Ajali hiyo ilitokea Agosti 10 majira ya  saa 2:00 asubuhi ambapo lori hilo lililokuwa likitoka Dar es Salaam lilipinduka jirani na kituo cha mabasi cha Msamvu baada ya dereva wa lori kumkwepa mwendesha pikipiki na kisha mafuta yaliyokuwa yakimwagika kushika moto na kuunguza watu waliokuwa wanayachota.