November 24, 2024

Majaliwa aagiza ujenzi viwanda vya kusokota nyuzi za pamba

Amesema vitasaidia kuondoa changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa soko la uhakika wa zao hilo.

  • Amesema vitasaidia kuondoa changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa soko la uhakika wa zao hilo.
  • Kwa sasa kuna viwanda viwili tu vya kusokota nyuzi katika mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wafanyabiashara wa zao la pamba Tanzania kujenga viwanda vya kusokota nyuzi na kutengeneza nguo ili kuondokana na tatizo la upatikanaji wa soko la uhakika wa zao hilo kwa wakulima. 

Majaliwa amesema kama viwanda vya kusokota nyuzi na kutengeneza nguo vitajengwa nchi kutakuwa hakuna haja ya kusafirisha pamba nje kwa sababu wakulima watapata soko la uhakika na kupunguza changamoto za ununuzi zinazojitokeza sasa. 

“Natoa wito kwa wafanyabiashara nchini wajenge viwanda vya kusokota nyuzi na kutengeneza nguo. Leo tumenunua pamba lakini tutaanza kupata changamoto ya usafirishaji wa kuipelekea nje ya nchi kuiuza. 

“Tukiwa na viwanda hapa ndani, tatizo la soko halitakuwepo,” amesema Majaliwa wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa nane inayolima pamba ya Mara, Mwanza, Simiyu, Geita, Kagera, Shinyanga, Singida na Tabora pamoja mwishoni mwa juma. 


Soma zaidi:


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa sasa kuna viwanda viwili tu vya kusokota nyuzi ambapo kimoja kiko Dar es Salaam na kingine kiko Shinyanga ambavyo uwezo wake ni mdogo kukidhi mahitaji yote malighafi ya pamba.

Pamba ni miongoni mwa mazao ya biashara yanayoiingizia Tanzania mapato mengi ya kigeni kutokana na usafirishaji wa zao hilo nje ya nchi kila mwaka lakini mapato hayo yamekuwa yakiathiriwa na kupanda na kushuka kwa bei ya pamba katika soko la dunia. 

Mathalan, mwaka jana tani 47,400 ziliuzwa nje ya nchi na ikilinganishwa na tani 25,300 mwaka 2017.