November 24, 2024

Rais Kenyatta apokea tausi aliozawadiwa na Magufuli

Hafla ya mapokezi ya tausi hao imefanyika katika Ikulu ya Nairobi, Kenya.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya (Kulia) akiwa na Balozi wa Tanzania  nchini Kenya,  Dk Pindi Chana  Ikulu jijini Nairobi wakati akipokea tausi kutoka Tanzania. Picha|Ikulu ya Nairobi.


  • Hafla ya mapokezi ya tausi hao imefanyika katika Ikulu ya Nairobi, Kenya. 
  • Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk Pindi Chana ndiye aliyeongoza ujumbe wa Rais Magufuli.
  • Rais Kenyatta amesema tausi hao ni ishara ya kuendeleza undugu na ujirani baina ya nchi hizo mbili. 

Dar es Salaam. Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya leo amepokea tausi wanne aliozawadiwa na  jirani yake, Rais John Magufuli alipofanya ziara binafsi nchini Julai mwaka huu. 

Rais Magufuli alitoa zawadi hiyo Julai 6, 2019 katika makazi yake yaliyopo katika kijiji cha Mlimani , Wilaya ya Chato mkoani Geita alipokutana na Kenyatta wakati wa mapumziko, ikiwa ni ishara ya heshima kuu na ujirani mwema wa nchi hizo mbili. 

Tausi hao ambao hutumika kama mapambo wamewasilishwa na Balozi wa Tanzania  nchini Kenya,  Dk Pindi Chana katika Ikulu ya Nairobi leo (Agosti 2, 2019) pamoja na ujumbe wa heri njema uliotolewa na Dk Magufuli. 

Kwa mujibu wa taarifa  iliyotolewa  na kitengo cha mawasiliano cha Ikulu ya Nairobi, Kenyatta ameeleza furaha yake kuu na shukrani kwa Rais Magufuli akisema ndege hao wanaashiria thamani ya upendo, umoja na undugu miongoni mwa raia wa mataifa haya mawili. 

“Kwa niaba yangu na pia raia wa Kenya, napokea zawadi hii maalum. Ni heshima kuu, sio tu kati yetu kama Marais, bali kama raia wa Afrika Mashariki. Uhusiano huu wa dhati na undugu sharti uendelee ili kunufaisha vizazi vyetu vya sasa na vile vijavyo,” ” amesema Rais Kenyatta katika taarifa hiyo. 


Zinazohusiana: 


Amesema Kenya haioni Tanzania kuwa jirani tu, bali jirani wa karibu huku kukiwa na maono sawa ya ustawi wa kanda hasa katika kukabiliana na uharifu.  

“Kwa kutegemea umoja uliopo kati ya mataifa yetu mawili tutakabiliana na maovu yote yanayowaathiri watu wetu pamoja na changamoto nyingine inayoweza kutokea hadi tutakapoafikia undugu na urafiki dhabiti ambao utawezesha watu wetu nchini Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi kutambuliwa kuwa raia wa Afrika Mashariki,” amesisitiza Rais.  

Ameukikishia ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Dk Chana kuwa Kenya itahakikisha tausi hao wanne wanatunzwa kwa ustadi ili wazaliane. 

Balozi Chana amempongeza Rais Kenyatta kwa uongozi wake wa ustadi na kuongeza kuwa tausi hao  wanaashiria upendo, heshima na urafiki uliodumishwa kati ya nchi hizo mbili.