October 6, 2024

Anachokitaka Magufuli jengo la tatu la abiria Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Tanzania

Ameagiza jengo hilo alilozindua leo litunzwe ili kuepusha uharibifu. Pia ameitaka Wizara ya Ujenzi kuwapata kipaumbele wazawa kutokana na fursa za uwekezaji zitakazopatikana.

Jengo jipya la tatu la  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA). Picha|Mtandao.


  • Ameagiza jengo hilo alilozindua leo litunzwe ili kuepusha uharibifu.
  • Ameitaka Wizara ya Ujenzi kuwapata kipaumbele wazawa kutokana na fursa zitakazopatikana. 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhakikisha jengo jipya la tatu la  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) linatunzwa na kuwa fursa kwa Watanzania kufaidika na shughuli za jengo hilo. 

Dk Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Agosti 1, 2019) wakati wa uzinduzi wa jengo hilo (Terminal 3) la JNIA Jijini Dar es Salaam, amesema Terminal 3 imejengwa kwa kodi za Watanzania na hategemei kuona fedha zao zinapotea kwa uharibufu utakaojitokeza wakati wa matumizi yake. 

“Niwaombe wizara ambao ndiyo wasimamizi wa jengo hili pamoja Watanzania wote watakaokuwa wanalitumia hili jengo ambalo linatoa taswira ya Watanzania na jiji letu la Dar es Salaam tulitunze tusiliharibu,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, amewataka Watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali ikiwemo za kibiashara zitakazopatikana kutokana na uwepo wa jengo hili huku Wizara ya Ujenzi akitakiwa kuwapa kipaumbele wazawa kufaidika na fursa hizo.

“Ninafahamu patakuwepo na maduka, patakuwepo na mabenki na huduma zingine mbalimbali, niwaombe Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi haya wapewe wazawa. Hatuwezi tukajenga jengo kama hili vitu vilivyomo mule vikamilikiwa na watu ambao siyo wazawa. Ni lazima wazawa waanze kufaidika na fedha walizozitumia kujenga jengo hili,” amesisitiza Rais.  


Soma zaidi: 


Katika hatua nyingine, amewataka wananchi kuwapokea wageni wakiwemo marais 16 wanaokuja kushiriki mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kwa shangwe na ukarimu mkubwa. 

Ujenzi wa jengo hilo unatekelezwa na kampuni ya Bam International ya Uholanzi ikisaidiwa na kampuni nyingine takribani 21 za ndani na nje ambapo ujenzi huo ulianza mwaka 2013 kwa gharama ya Sh560 bilioni.

Jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege 17 hadi 19 zikiwemo kubwa kwa wakati mmoja na kumudu abiria milioni sita kwa mwaka ambapo katika eneo la nje ya uwanja kuna nafasi ya kuegesha magari 2,000 ya watu wanaotumia uwanja huo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema kukamilika kwa jengo la tatu la JNIA kunatoa fursa ya ukarabati wa jengo la pili ambalo lilikuwa linatumika hapo kabla ili kuongeza idadi ya wasafiri wanaotumia majengo matatu yaliyopo uwanjani hapo.

“Sasa hivi Terminal 1, terminal 2 na terminal 3 zinapitisha abiria milioni tano kwa mwaka na ongezeko la abiria liko kati ya asilimia 2.5 na asilimia tatu kwa mwaka. Moja kwa moja unaona kwamba haitachukua muda Terminal 1, terminal 2 na hata terminal 3 itajaa,” amesema Mhandisi Kamwelwe.